Na Waandishi Wetu Dar, Dodoma
KUMEKUWEPO na hali inayozua maswali kuhusu utata unaoibuka katika mkutano wa nane wa Bunge unaoendelea mjini Dodoma, hasa kutokana na hoja kali kuibuliwa na kisha kupooza haraka.
Baadhi ya mijadala ambayo imeibuliwa katika mkutano huu unaoendelea, inaonekana kuwa mizito sana na yenye maslahi ya taifa, lakini kila inapotolewa, linatokea tukio la kuifanya isijadiliwe kwa kina au kupoozeshwa kwa wachangiaji ambao ni wabunge na wafuatiliaji ambao ni wananchi.
Kupooza huko ama kusahaulika haraka kunazua maswali na kunaonyesha wazi kuwa, vikao vinavyoendelea huenda visiwe na hamasa kubwa kama ilivyotarajiwa kabla ya Bunge hili la Bajeti kuanza wiki mbili zilizopita.
Tukio la kwanza lilikuwa mjadala wa Bajeti ya serikali ya mwaka 2007/08, bajeti iliyobeba dhana ya kuongezeka kodi na kisha kukawepo mkakati wa wazi kutoka kwa wabunge wa CCM na wale wa upinzani kupanga kuikataa lakini kabla ya kufanya hivyo, kukaibuka tukio la kitaifa lililokata nguvu zao.
Tukio hilo ni kushinda timu ya Taifa dhidi ya Burkina Faso lililotokea usiku wa kuamkia Jumapili, Juni 17, 2007 na kufuatiwa na shamrashamra za mapokezi ya timu hiyo kuanzia Juni 18, 19 na 20.
Ushindi huu ni wazi ulimaliza kabisa utamu wa mjadala hasa baada ya Kambi ya upinzani ambayo kwa mara ya kwanza ilikuwa inatoa bajeti yake mbadala iliyosomwa na Kiongozi wa Upinzani bungeni, Hamad Rashid Mohamed.
Bajeti ya wapinzani ilisomwa Jumatatu Juni 18 huku ikifumbua mambo mengi ya kuiwezesha Tanzania kujiendesha kiuchumi.
Kabla ya kujadiliwa na mara tu baada ya kusomwa, kukafuatia tukio lisilo la kiutaratibu wa kawaida lililohusisha kubadili shughuli za Bunge ili kuwaruhusu wachezaji na viongozi wa timu ya taifa kuingia bungeni kupongezwa.
Tukio hili ni dhahiri liliua nguvu ya mjadala wa bajeti ya wapinzani, bajeti ambayo ilichangia kubadilishwa kwa baadhi ya mambo katika bajeti ya serikali hasa katika kodi za mafuta ya taa ambazo zilihamishiwa katika mafuta ya petroli.
Wananchi mbalimbali nchini walisikika wakizungumzia ushindi wa Stars kuwa, umekuja kuwasahaulisha machungu ya bajeti. Hata wabunge walionekana kupagawa na ushindi huo ambao ulielezwa baadaye kuwa, ulitumiwa na serikali kupunguza nguvu ya kuijadili bajeti ya Waziri Meghji.
Hoja nzito zilizofuata kama ile iliyotolewa na Mbunge wa Bukoba Mjini, Balozi Khamis Kagasheki, aliyemshambulia Waziri Juma Ngasongwa kwa kusema kuwa amesema uongo juu ya Uwanja wa Ndege Bukoba kwamba umezungushiwa uzio, ilifuatiwa na ile ya Mbunge wa Same, Anne Kilango Malecela.
Kilango aliwataka viongozi wa serikali hasa mawaziri kuacha tamaa na kumsaidia rais na kuepuka mikataba mibovu inayolimaliza taifa kwa hasara.
Kisha alifuata Balozi Getrude Mongela, Mbunge wa Ukerewe, aliyezungumzia uchungu katika bajeti ya mwaka huu na kueleza umuhimu wa kubana mkanda katika matumizi ya serikali.
Baadaye aliibuka Mbunge wa Nzega, Lucas Selelii, aliyetishia kutoa shilingi katika mshahara wa Waziri Mkuu na Wizara nyingine mbili, hadi hapo atakapohakikishiwa kuwa hakutakuwa na ahadi hewa katika bajeti hii ya sasa, ukilinganisha na ilivyotokea katika bajeti za huko nyuma.
Kujitokeza kwake kulidhaniwa kuungwa mkono, lakini suala la Stars bado lilikuwa na nguvu, likameza nguvu yake na kufanya hoja kuundwa ndani ya CCM kujadili msimamo wa mbunge huyo.
Wakati akifunga mjadala wa Bajeti, Waziri wa Fedha Zakia Meghji aliibua mjadala mpya, baada ya kuvishambulia vyombo vya habari na wahariri wake kwa kukosa uzalendo na kisha kuwabeza baadhi ya wabunge wenzake, hasa wa upinzani, akisema wana uelewa mdogo.
Majibu dhidi yake yalifuata baada ya Waziri Mkuu Edward Lowassa kusoma bajeti ya ofisi yake.
Safari hii muibua mjadala akawa Mbunge wa Karatu (Chadema), Dk Wilbroad Slaa aliyelipua bomu kuhusu ufisadi ndani ya Benki Kuu (BoT) na uchangiaji wenye kulinda maslahi binafsi kuhusu suala hilo uliofanywa na mbunge mkongwe, Chrisant Mzindakaya.
Ilikuwa ni Jumatatu Juni 25, wakati Slaa aliposimama na kumlipua Mbunge wa Kwela Chrisant Mzindakaya kwa kuitetea Benki Kuu, huku akitoa taarifa za Mzindakaya kupata udhamini wa mkopo kupitia BoT.
Mjadala ulikuwa mzuri, Dk Slaa akimtuhumu Mzindakaya kwa kujipatia mkopo Benki ya Standard Chatered kwa dhamana ya Benki kuu, suala lililomfanya aunganishwe katika tuhuma za ulaji wa mabilioni ya fedha kupitia ujenzi wa Jengo maarufu la Twin Tower, zilizokuwa zikimkabili Gavana wa Benki Kuu, Daud Balali ambaye kimsingi alitakiwa kujiuzulu ili kutoa nafasi kwa tume kuundwa kuchunguza kashfa hiyo ya ulaji.
Mzindakaya mwenyewe, alikiri kuwa hilo lilikuwa bomu kali kumtokea katika miaka 40 ya siasa. Wakati mjadala huo ukizidi kushika kasi, hali inabadilika ghafla, usiku wa Jumanne ambapo msiba wa Mbunge wa Viti maalum, Amina Chifupa unabadili anga ya mijadala bungeni, taifa zima linaelekeza macho na masikio kujua nini kilichotokea kwa Amina na kusahau kuwepo kwa hoja zinazotakiwa kuendelea kwenye kikao cha Bunge mjini Dodoma.
Hoja zote zilizoihusu Benki Kuu na Mzindakaya, zikapooza na kisha Bunge kuahirishwa, Jumatano Juni 27 ili kutoa nafasi kwa wabunge kuhudhuria msiba jijini Dar es Salaam.
Mwandishi wa gazeti hili, Ramadhani Semtawa aliyepo Dodoma, aliliambia Mwananchi Jumapili kuwa, bado kuna utulivu na umakini mkubwa kwa wabunge katika kujadili hoja na ni vigumu kuamini kuwa walikuwa wamepooza au kuwa na furaha pale matukio ya kitaifa yalipotokea.
Jijini Dar es Salaam, gazeti hili lilifanikiwa kuzungumza na wananchi mbalimbali ambao wengi walizungumzia kuhusu kuwepo mkosi fulani katika kikao hiki cha Bunge, huku pia wakieleza kuwa kuna matukio muhimu ambayo yameibuliwa lakini sasa yanajadiliwa kimya kimya bila kuwapo hamasa katika jamii kufuatia tukio la ushindi wa Stars na lile la msiba wa Amina.
Kikao hiki hadi sasa licha ya kujadili kwa kina kuhusu bajeti pia kimeonyesha hali tofauti ambapo wabunge wa upinzani na wa chama tawala, mara kadhaa wamesimama na kuizungumza serikali, hasa kuhusu matukio ya utoaji ahadi hewa.
Baadhi ya wabunge akiwemo Naibu Waziri wa zamani na Mbunge wa Mchinga, Mudhihir Mudhihir, waliwataka mawaziri wa serikali kuanza safari za kwenda kuwaeleza wananchi kuhusu ahadi hewa kufuatia wao kuchoka kufanya hivyo.
Swali kubwa lililopo katika jamii kwa sasa ni kuwa kunaibuka hoja nzito na kabla hazijajadiliwa kwa kina au kupata sura ya kitaifa, jambo jipya linajitokeza na kuzipooza kwa muda kabla hazijaibuka upya.