Mbunge Mstaafu wa Lupa, Njelu Kasaka:
"Amina alikuwa jasiri ndani ya kundi la wabunge wachache wenye moyo wa ujasiri, aliyeweza kukemea ufisadi, tena ndani ya Bunge jambo ambalo hata wabunge wakongwe hawajawahi kushikia kidete vita ya dawa za kulevya. Hakika Amina alikuwa ni mfano ndani na nje ya CCM."
Mkuu wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Hamad Rashid Mohamed:
"Kila kifo kina upya wake na uchungu wake. Nasema kifo hiki ni kipya kwa sisi wahusika wa taifa hili, kilichobaki, sote pamoja tuige na kuendeleza yale yote mazuri aliyoyaacha. Kambi yetu ya upinzani ilipata faraja kuona mbunge wa CCM kijana, shujaa akiingia bungeni, lakini sasa tunasikitika kwamba ametutoka katika kipindi kifupi sana."
Rais wa Tanzania, Jakaya Kikwete:
"Wengi wetu tutamkumbuka marehemu Amina Chifupa kwa mchango wake muhimu alioutoa bungeni na katika jamii, hasa miongoni mwa vijana. Alikuwa hodari katika kujenga hoja na kutetea maslahi ya vijana wenzake na taifa kwa ujumla. Alikuwa kijana msema kweli na jasiri katika kutoa maoni yake kwa jambo aliloliamini."
Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa (UVCCM)-Taifa, Dk. Emmanuel Nchimbi:
"Sisi vijana wa CCM kamwe hatuwezi kumsahau Amina kwa uwakilishi wake bungeni, hasa katika kutetea haki na maslahi ya vijana nchini wakati wote wa uhai wake.
Marehemu alikuwa mchapakazi hodari, mkweli na ambaye siku zote alitetea masuala ya vijana na ni sifa ambayo ilimfanya apendwe na vijana."
Mbunge wa Same Mashariki, Anna Kilango:
"Msiba umenishtua sana na umeniumiza sana kwa kuwa nilikuwa karibu na Amina sana. Nilikuja Dar es Salaam, Ijumaa iliyopita kumwona alipokuwa mgonjwa, lakini sikuongea naye. Kwa hakika alikuwa ni mfano wa kuigwa."
Mbunge Ukerewe, Gertrude Mongela:
"Nilimfahamu Amina kama mchapakazi kwa kuwa alikuwa ni mtu ambaye haogopi na anajituma, alikuwa anajitahidi, haogopi, alikuwa anasema kile alichokuwa anakiamini. Tumempoteza mpiganaji hodari, umati huu wa watu unaonyesha alikuwa mtu wa watu."
Naibu Waziri Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Ritha Mlaki:
"Marehemu alipenda kazi. Alipiga vita dawa za kulevya, kusaidia watoto yatima na vijana, hasa kwenye sekta ya michezo."
Mbunge wa Viti Maalum, Mariam Kasembo:
"Nimejawa na majonzi ya kifo cha mbunge mwenzetu, alikuwa ananiita shangazi, alipenda ushauri na tuliamini angeishi muda mwingi ndani ya Bunge. Tumempoteza mtu ambaye kwa siku za usoni angeweza kuwa mfano wa kuigwa zaidi."
Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto (CHADEMA):
"Amina, maisha yako yana tafsiri nyingi. Umepitia mambo mengi sana. Ulitaka kuandika kijitabu kuhusu maisha yako ili watu wakujue vizuri. Wakati tunajiandaa kukusanya vya kukusanya, ukawa mgonjwa. Umeondoka kabla hujakamilisha azima yako. Bado watu hawakujui.
Amina niseme nini kukueleza wakati tunakupumzisha pumziko la kudumu? Maneno hayaji vidole vinatetemeka. Tutakukumbuka. Ucheshi wako na umahiri wako katika kuhakikisha unapata unachokitaka. Usiku wa Mei 6, ulinipigia simu kuniambia kuwa Mkwawa anakuita na kwamba Mwalimu Nyerere ananipa salamu. Mimi naomba uwape salamu. Uwaambie nchi yao inaendelea, na kwamba huna uhakika ndoto yako ya kujenga taifa imara itafikiwa karibuni. Waambie Mkwawa na Mwalimu kuwa siku hizi ili uwe kiongozi ni lazima upande mabegani mwa mwingine na kumwangusha na wala si uwezo wa mtu."
Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi (CUF), Seif Sharif Hamad:
"Amina amefariki akipambana licha ya umri wake mdogo bungeni, lakini ameweza kufanya mambo makubwa katika kipindi kifupi, vijana wana kitu cha kujifunza kutoka kwa marehemu kutokana na ukweli kuwa alikuwa akijiamini na mwenye kuongea bila soga. Kwa kweli ni pigo kubwa kwa taifa."