Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Serikali yajitetea bungeni
Serikali yajitetea bungeni
By Habari Tanzania | Published  06/29/2007 | Habari za Kitaifa | Unrated
na Mwandishi Wetu, Dodoma


SERIKALI jana ilitetea bungeni vitendo vya maofisa masuuli nchini wanaoshindwa kuwasilisha nyaraka kwa wakati zinapohitajiwa kwa ukaguzi.

Utetezi huo ulitolewa na Naibu Waziri wa Fedha, Abdisalaam Issa Khatib, licha ya Dk. Willibrod Slaa (Karatu – CHADEMA) kuonya kuwa, ucheleweshaji wa nyaraka hizo unaweza kuwa ni mbinu zinazotumiwa na maofisa hao kuficha wizi.

Katika swali la nyongeza, Dk. Slaa alisema kuwa, kutopatikana kwa nyaraka wakati wa ukaguzi, lakini zikaletwa baadaye na maofisa hao hao, ni dalili kuwa nyaraka hizo hazikuwepo kabisa na maofisa hao walizitafuta baada ya kuhojiwa.

“Kupotea nyaraka kunaendeleza wizi… kwa nini wasizionyeshe wakati wa ukaguzi na zije zipatikane baadaye?” alihoji.

Swali hilo la nyongeza la Dk. Slaa lilifuatia majibu ya Khatib yaliyoonyesha kuwa, kiwango cha fedha zinazotumika bila kutolewa kwa nyaraka, na kile kinachotolewa nyaraka pungufu, kimekuwa kikipungua.

Katika swali lake la msingi, Dk. Slaa aliitaka serikali ieleze tangu Julai 2001 hadi Juni 2006, ni kiasi gani cha fedha kimepotea wakati wa ukaguzi au wakati wa matumizi kutokana na vocha zisizo sahihi kwa upande wa serikali za mitaa.

Aidha, aliitaka serikali itoe tamko kuhusu upoteaji wa hati hizo au kutotunzwa vizuri wakati wote wa uandishi, ukaguzi na uhifadhi.

Alitaka pia kujua idadi ya watu, kati ya wale waliohusika na upotevu wa hati hizo, ambao wamechukuliwa hatua kutokana na makosa hayo katika kipindi cha kati ya mwaka 2001 hadi Juni 30, 2006.

Licha ya ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kila mwaka kuonyesha ubadhirifu wa aina hiyo, Khatib alibainisha kuwa, kumbukumbu zinaonyesha katika kipindi alichokitaja mbunge, hakuna ofisa yeyote aliyepoteza nyaraka za malipo kwa makusudi au uzembe.

Kuhusu kiasi cha fedha kinachoonekana kupotea kutokana na nyaraka pungufu au kutokuwepo kabisa, Khatib alisema kuwa tangu Julai 2001 hadi Juni 2006, hoja zinazohusu malipo yasiyo na nyaraka zilikuwa na thamani ya jumla ya zaidi ya sh bilioni 13.719.

Hata hivyo, alisema kuwa kiwango hicho kimepungua na kufikia zaidi ya sh milioni 43.485, sawa na asilimia 0.003 ya kiwango cha awali baada ya nyaraka husika kuwasilishwa kwa wakaguzi.

“Malipo yenye nyaraka pungufu yalikuwa sh 80,734,216,390.64 na sasa kiwango hiki kimepungua kufikia sh 1,550,059,502.42, sawa na asilimia 0.019 ya kiwango cha awali,” alisema.

Khatib alieleza kuwa, kwa upande wa serikali za mitaa, hoja zinazohusu vocha zisizo na nyaraka au zenye nyaraka pungufu zimekuwa zikipungua kutoka sh bilioni 11.66 mwaka 2000/01 hadi sh bilioni 5.26 mwaka 2005/06.

Khatib alisema kuwa, sababu kubwa ya mapungufu hayo kwa miaka kadhaa sasa ni kutokana na kutokuwepo kwa mawasiliano sahihi ya wakaguzi na wakaguliwa.

“Kwa mfano, fedha zinazohusu maendeleo ya halmashauri huwa ndani ya bajeti za mikoa. Lakini fedha halisi kutoka Hazina hupelekwa moja kwa moja kwenye halmashauri husika bila kupitia mikoani na hivyo halmashauri hupeleka Hazina stakabadhi ya kukiri kupokea fedha hizo,” alifafanua.

Alisema kutokana na hali hiyo, mkaguzi anayefika mkoani hatoweza kupata stakabadhi ya kukiri kupokea fedha hizo, na hiyo inamfanya aandikie matumizi hayo kuwa malipo yasiyo na nyaraka.

Katika jibu la nyongeza, Waziri wa Fedha, Zakia Meghji, alisema kuwa Sheria ya Fedha ya mwaka 2001, iliyorekebishwa mwaka 2004, inaitaka Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali, kutoa mapendekezo wizarani, juu ya hatua zinazopaswa kuchukuliwa kwa wahasibu wanaohusika na kasoro kama hizo.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.