SAKATA la madai ya ubadhirifu ndani ya Benki Kuu (BoT), limezidi kuiandama serikali kwa wanasiasa wa kambi ya upinzani kuzidi kuibua hoja nzito.
Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Hamad Rashid Mohammed (Wawi-CUF), jana alieleza kushangazwa kwake na hatua ya serikali kulizuia Bunge kufanya kazi zake zilizoainishwa kikatiba.
Jitihada za jana za Waziri wa Fedha, Zakia Meghji, kutoa ufafanuzi zaidi kuhusu tuhuma kadhaa zinazomuandama Gavana wa Benki Kuu, Daudi Balali na Mbunge wa Kwela, Chrisant Mzindakaya, zilionekana dhahiri kugonga mwamba.
Maelezo ya Meghji, hayakuweza kumnyamazisha Hamad Rashid, ambaye wakati akichangia hotuba ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, alieleza wasiwasi wake kuhusiana na hatua ambazo serikali imeahidi kuzichukua kuhusu suala hilo.
Katika kauli yake aliyoitoa mara baada ya kipindi cha maswali na majibu jana asubuhi, Meghji alirejea kauli aliyoitoa wakati akifunga mjadala wa bajeti kuwa, serikali imeshamuagiza Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Setikali (CAG), kualika kampuni za kimataifa kuja kufanya ukaguzi huru BoT.
Meghji alisema kuwa, tayari zabuni zilikwishatangazwa na jana ndio ilikuwa mwisho wa kuwasilisha zabuni za kuomba kazi hiyo.
Kwa mujibu wa Meghji, ukaguzi huo utahusisha ufujaji au ubadhirifu wa fedha kwenye akaunti ya madeni ya biashara ya nje.
Kuhusu tuhuma zinazosambazwa kwa njia ya tovuti dhidi ya Balali, maofisa wengine wa umma na wafanyabishara kadhaa, Meghji aliwataka watu wenye taarifa za kina kuhusu tuhuma hizo, kujitokeza ili kuipatia serikali taarifa zitakazoisaidia kuanzisha uchunguzi.
Hata hivyo, Hamad Rashidi alisema katika mchango wake kuwa, kilichoahidiwa kuchunguzwa na serikali, ni sehemu ndogo tu ya jambo kubwa ambalo limekuwa likiitafuna nchi.
“External Auditor (mkaguzi wa nje) mnayemleta atafanya ukaguzi kuzingatia external debts (akaunti ya madeni ya nje). Sisi tunasema dola takribani milioni 800 zimepotea BoT,” alisema.
Alisema kiasi hicho cha fedha kimepotea katika ujenzi wa majengo ya minara miwili ya BoT, ujenzi ambao uliruhusiwa kuendelea licha baadhi ya wajumbe katika Baraza la Mawaziri kupinga ujenzi huo pale gharama zake zilipopanda.
Hamad Rashid, aliishangaa serikali kwa msimamo wake wa kukataa Bunge kuunda kamati teule ya kuchunguza kashfa hizo, wakati katiba inatoa haki kwa Bunge kufanya shughuli kama hizo.
“Hili si suala la kiitikadi. Benki Kuu ni pakacha letu sote… mkulina wa karafuu anayeanguka juu ya mti akaumia, fedha zake zipo pale, mkulima wa kahawa anayeumia, fedha zake zipo pale… linapovuja linatuathiri sote,” alisema kwa msisitizo.
Hamad Rashid, alizidi kuibana serikali kwa kueleza kuwa kila mwaka CAG amekuwa akifanya ukaguzi BoT na katika miaka yote, hakuna ripoti yoyote iliyoonyesha ubadhirifu BoT.
“Ndio maana tunasisitiza kuwa chombo pekee kitakacholinda maslahi ya wananchi ni Bunge. Bunge lina mamlaka ya kuisimamia serikali. Hatuoni sababu za msingi za serikali kukataa Bunge liunde kamati teule,” alisisitiza.
Hamad Rashidi alisema kuwa, anaelewa unyeti wa chombo kinachozungumziwa (BoT), lakini tuhuma za ubadhirifu wa dola milioni 800 ni kubwa mno kuachwa hivi hivi.
“Naelewa sensitivity (unyeti) wa Benki Kuu. Naelewa pia shida ya Watanzania wanaolima, hazina yao ikiliwa, hilo siwezi kulikubali hata kidogo, pamoja na sensitivity,” alisema.