Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Amina Chifupa ‘nabii’ wa kifo
Amina Chifupa ‘nabii’ wa kifo
By Habari Tanzania | Published  06/29/2007 | Habari za Kitaifa | Rating:

na Sophia Mpunga, Lupembe


MBUNGE WA Viti Maalum, Amina Chifupa, alizikwa nyumbani kwa mama yake mzazi jana, majira ya saa 9:00 alasiri, Lupembe Njombe na maelfu ya waombolezaji kutoka maeneo mbalimbali nchini.

Mazishi ya mbunge huyo aliyekuwa mdogo kuliko wote ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, yaligubikwa na vilio, simanzi na hali ya mshtuko kwa wakazi wengi wa eneo hilo na wale wa kutoka maeneo mbalimbali nchini.

Shughuli nzima ya kumuombea marehemu na mazishi ya mwanasiasa huyo kijana, aliyekuwa mjenzi mahiri wa hoja, iliongozwa na kaka yake aitwaye, Hussein Chifupa.

Akizungumza nyumbani kwake ambako ndiko ziliko shughuli zote za msiba, babu wa marehemu, Nurdin Mbanga, alimuelezea mjukuu wake huyo kuwa mtu aliyekuwa akisema na kutenda mambo kutokana na maono ambayo aliyarithi kwake.

Mbanga ambaye kwa sasa ni Diwani wa CCM, Kata ya Lupembe, aliwaeleza maelfu ya watu waliojitokeza kumsindikiza Amina katika safari yake hiyo ya milele kuwa, alikutana na mjukuu wake huyo miezi takriban miwili iliyopita, wakati alipofika huko kuwatembelea akiwa ameongozana na aliyekuwa mumewe, Mohammed Mpakanjia.

Alisema alipofika hapo, pamoja na mambo mengine aliyozungumza naye, ilikuwa ni dhamira yake ya kutaka azikwe eneo alilochagua wakati utakapofika.

Kwa mujibu wa Mbanga, mjukuu wake Amina alimweleza kuwa, alikuwa ameamua kuzikwa hapo, ili aweze kuwapa fursa ndugu zake ya kuliona kaburi lake mara kwa mara kuliko ambavyo ingekuwa kama angezikwa Dar es Salaam.

Mbali ya mzee huyo, shughuli nzima ya mazishi ya Amina yaliyohudhuriwa pia na Katibu Mkuu mstaafu wa CCM, Philip Mangula, ilitawaliwa na simanzi iliyokuwa ikionyeshwa na wanawake wa eneo hilo.

Wakizungumza kwa masikitiko makubwa, wanawake hao, walisema walikuwa wameguswa sana na msiba huu kwa sababu Amina alikuwa mtu mwenye msaada mkubwa kwao.

Wanawake hao walisema, katika kipindi cha mwaka huu peke yake, Amina alikwenda Lupembe mara nne na akatoa misaada mbalimbali kwa wanawake wa huko.

Mbunge wa Singida Kusini, Mohammed Misanga, ambaye ndiye aliyekuwa kiongozi wa wabunge na mwakilishi wa Spika wa Bunge, Samuel Sitta, alieleza kuguswa na kushtushwa na msiba wa mbunge mwenzao huyo.

Misanga alisema, Bunge lilikuwa limegharamia mazishi hayo kwa kulipia gharama za kusafirisha mwili wa marehemu, wabunge 13 pamoja na wafiwa wengine.

Alisema wabunge wote wa Bunge la Jamhuri ya Muungano kwa pamoja walitoa kiasi cha shilingi milioni tatu (sh 3,000,000) kama rambirambi zao kwa kumpoteza mbunge mwenzao.

Mbali ya wabunge, Umoja wa Vijana wa Wilaya ya Njombe ulikuwa umetoa ubani wa sh 300,000 kwa ajili ya kumlilia Amina aliyeingia bungeni akipitia katika umoja huo.

Miongoni mwa viongozi waliohudhuria mazishi hayo ni Waziri wa Sayansi, Teknolojia na Elimu ya Juu, Profesa Peter Msolla na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma na Mbunge wa Iringa, Monica Mbegha.

Wengine ni Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Erasto Mbwilo, Mkuu wa Wilaya ya Njombe, Darry Ibrahim Rwegasila na viongozi wa serikali na wa CCM wa Mkoa wa Iringa na Wilaya ya Njombe.

Akizungumza kabla ya mazishi, Mbunge wa Viti Maalum, Susan Lyimo (Chadema), alimuelezea Amina kuwa alikuwa mbunge aliyevuka mipaka ya kichama.

Alisema, Amina pamoja na kuwa mdogo kiumri, alikuwa akistahili kuitwa mbunge wa taifa kwani, alikuwa akifanya kazi kwa ushirikiano mkubwa na wabunge wenzake wote, pasipo kubagua kwa misingi ya kiitikadi.

Lyimo alisema Amina hakuwa mtu wa kuutumia u-CCM wake kuzungumzia jambo lililokuwa likimtatiza, kwani alikuwa ni mtu aliyekuwa aqkizungumza jambo kwa kuweka mbele maslahi ya taifa.

Amina Chifupa, alifariki dunia Jumanne majira ya saa 2:45 usiku katika Hospitali ya Jeshi ya Lugalo jijini Dar es Salaam, alikokuwa amelazwa kwa takriban wiki moja, akisumbuliwa na malaria na kisukari.

Pamoja na maelezo hayo, kikubwa kinachoonekana kuwaumiza kichwa watu wengi, ni mazingira ya kifo cha mwanasiasa huyo, kwani watu wengi wamekuwa hawataki kuamini iwapo kweli mwanasiasa huyo alikuwa amekumbwa na maradhi makubwa ambayo hatimaye yamesababisha yachukue maisha yake.

“Nini hasa kimemuua Amina jamani, ni kisukari kweli? Ni kitu gani hasa?” Ndilo swali kubwa ambalo limekuwa likiulizwa na watu mbalimbali kutoka sehemu mbalimbali nchini.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments
  • Comment #1 (Posted by Mohamed Kitenge)
    Rating
    Waandishi muwe wasaka ukweli,kwani mnaandika uongo sana,kwa akili ya mtu mzima,haiingii akili kuona eti Amina amekufa kwa ugonjwa wa sukari na malaria.Kwa nini mfiche ukweli kama kalogwa,mambo yenu hayo ndio yanaongeza hata huu ukimwi,kwani kuna waganga wanadai kuutibu,lakini ninyi hamuwapi nafasi,kazi yenu kubwa ni kuwakatisha tamaa tu.Hakuna hata Mtanzania mmoja asiejuwa kama kuna uchawi,yuwache unafiki.Kazi yenu waandishi ni kuficha ukweli na kuandika uongo tu,mnaniudhi sana.
     
Submit Comment


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.