NAMLILIA Amina Chifupa. Nina kila sababu ya kumlilia Mheshimiwa huyu kijana aliyepewa dhamana ya kutuwakilisha vijana wenzake katika Bunge la Jamhuri ya Muungano.
Namlilia Amina kwa sababu mbali ya kuwa mwakilishi wa vijana, alikuwa mstari wa mbele kutetea na kupiga vita hadharani biashara na matumizi ya dawa za kulevya.
Namlilia, si kwa sababu alikuwa mbunge wa vijana, la hasha! Hilo peke yake halitoshi, Amina alikuwa hodari, mwenye kujiamini na kuthubutu kueleza hisia na mitazamo yake bila kujali kama atamkwaza mwingine.
Uthubutu na kujiamini aliokuwa nao ndio kiini cha mafanikio yake, aliamini kile alichoona kwake ni sahihi. Amina, alikuwa na marafiki wengi na wengine hakupata nafasi ya kuwafahamu hadi kifo chake.
Idadi ya marafiki aliokuwa nao ni kubwa hali inayonilazimu kuamini kwamba hakuna mkamilifu anayeweza kupendwa na wote ama kuchukiwa na wote. Nataka kuamini kuwa Amina, alikuwa na maadui, wapo aliowajua na wengine hakuwajua.
Nyota yake ilianza kung’aa akiwa mwanafunzi. Kwa miaka 26 aliyoishi duniani, alikumbana na vikwazo ambavyo kwa maoni ya wengine vilisababishwa na tabia yake ya kujiamini na kuthubutu kufanya kila alilohisi kuwa anaweza (binafsi niliipenda tabia hiyo) hali iliyowafanya wengine kumtafsiri tofauti.
Sitaki kutaja sifa za Amina baada ya kifo chake bali napenda kuelezea tabia ya uthubutu na kujiamini aliyokuwa nayo kama chanzo cha mafanikio yake mbele ya jamii.
Haya ninayoyasema nilikuwa nayasema pia enzi za uhai wake tena mara kwa mara, niliwahi kusema hivyo tangu akiwa mtangazaji.
Kwa mara ya kwanza, nilimuona Amina katika kipindi cha mgongano wa mawazo kinachorushwa hewani na kituo cha ITV wakati huo alikuwa kidato cha nne, Shule ya Sekondari ya Kisutu.
Nilivutiwa na sauti yake, ukapita muda nikaanza kuisikia sauti ile kwenye kituo cha Radio Clouds FM, alikokuwa akifanyia kazi. Hapo nikaanza kufuatilia vipindi vyake, nikajikuta nampenda bila yeye kujua.
Sifa mbaya dhidi yake zilivuma lakini hakukata tama, badala yake aliendelea na utaratibu wa maisha yake ambao aliamini kuwa unamfaa kuufuata bila kujali wala kuyumbishwa na maneno ya watu wengine.
Alipojiingiza kwenye siasa, wapo waliombeza na kusema kuwa anahitaji muda zaidi kabla hajajiingiza kwenye ulimwengu huo.
Amina, alipokea ushauri wa kila mtu kuhusu uamuzi wa kujitosa kwenye siasa na kusisitiza azima yake ya kuwa mwanasiasa huku akiamini kuwa ndoto zake zitatimia.
“Nimezaliwa kwenye familia ya mwanasiasa, hivyo nina kila sababu ya kuwa mwanasiasa…ni ndoto niliyokuwa nayo tangu utotoni,” alikaririwa Amina katika vyombo vya habari wakati wa kampeni za kugombea ubunge.
Lakini kwa Amina, haikuwa bahati mbaya wala hakuwa akijaribu, aliamini katika kila alilotaka na kulifanya kuwa lazima angefanikiwa. Hivyo ndivyo ilivyokuwa kwake.
Amina, alipenda kufanya shughuli za kijamii na kuudhihirishia umma kuwa anafanya nini, kwa nani na kwa wakati gani, yote hayo aliyafanya kwa kuwashirikisha wanataaluma wenzake wa habari.
Kwa mara ya kwanza kuonana na Amina ilikuwa wakati wa kikao cha sita cha Bunge la Jamhuri mjini Dodoma, ucheshi ni sehemu ya maisha yake, hakusita kuwasalimu waandishi wenzake na kuongea nao mawili, matatu kabla ya kurudi nyumbani kwake.
Tabia hiyo ilinijengea mazoea kwake, tena kwa kipindi kifupi. Siku ninayoikumbuka ambayo kwa mara ya kwanza Amina alizungumza jambo lililonifanya nimwone tofauti tulikuwa watatu, yaani mimi, yeye na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Daniel Nswanzugwanko na Mbunge wa Iramba Magharibi, Juma Killimbah.
Tulikuwa nje ya jengo la zamani la Bunge lijulikanalo kama Ukumbi wa Msekwa, nikizungumza machache kuhusu mustakabali wa muswada wa habari uliotarajiwa kujadiliwa wakati wa kikao cha saba cha Bunge na Mheshimiwa Nswanzugwanko.
Akaja Amina aliyevalia suti ya suruali na shati la mikono mirefu, rangi nyeusi, kitambaa cheusi kichwani, viatu aina ya travota vya kisigino kirefu kiasi. Mikononi mwake upande wa kushoto, alibeba mkoba mweusi, kulia alishika funguo za gari lake jeusi aina ya Land Cruiser alizokuwa akizichezesha chezesha.
Alipofika tulipokuwa alitabasabu na kutoa salamu kwa kushikana mikono na kila mmoja. Kabla ya kusema lolote, Nsanzugwanko alimtania kwa kusema ‘sema mtoto mzuri…’ Amina alicheka akainamisha uso kwa haya kidogo, kisha akamwambia: “Acha utani mheshimiwa.”
Baada ya utani huo, Killimbah aliyekuwa akichangia hoja kuhusu muswada huo aliendelea kuongea, punde Amina, akamkatisha kwa kusema: “Huo muswada hauna faida wala masilahi kwa waandishi.”
Aliendelea kusema: “Nitahakikisha tunaupinga usipitishwe…kwa sababu serikali haijaandaa mazingira bora ya elimu kwa wanahabari, huwezi kusema lazima mwandishi awe na digrii wakati hakuna chuo kinachotoa digrii ya habari.
“…Mimi mwenyewe ni mwandishi Irene, nyie andikeni mabaya yote kuhusu muswada huo ili wabunge wahamasike kuukataa na sisi ukija tutaupinga (akamgeukia Killimbah aliyekuwa akimtizama) na kumuuliza au siyo?” Kabla ya kujibiwa, Amina akacheka tena kwa sauti ya juu kidogo na kumgonga begani Killimbah.
Kauli ya Amina kwake ilikuwa nyepesi lakini niliipokea kwa mtazamo mpana na kuichambua kwa sababu nilikuwa nikisikia maneno tofauti juu yake, kwa waliodai kumfahamu zaidi kwamba alikuwa na uwezo mdogo katika kufikiri na kutoa uamuzi wa jambo fulani.
Bila kujua, alinidhihirishia uwezo wake na kujionyesha kwangu yeye ni nani, kuanzia hapo nilipata kumwelewa mheshimiwa huyo kijana na mwakilishi wa vijana, hali iliyonifanya kufuta mawazo ya awali. Nina sababu ya kusema hivyo.
Mazoea kati yangu na Amina hayakuwa ya karibu sana, lakini hakusita kusimama na kunisalimu ama kutusalimu akiamini kuwa waandishi wa habari ni sehemu ya marafiki na ndugu zake.
Nakumbuka tena Aprili 20 mwaka huu siku ya Ijumaa, karibu saa tano usiku tukiwa Dodoma Hoteli kwenye hafla ya chakula cha usiku iliyoandaliwa kwa ajili ya waandishi wa habari, Amina alikuwapo.
Siku hiyo alivaa sketi ndefu na blauzi ya mikono kirefu rangi ya maziwa na nyeusi, kama kawaida yake alijifunga kilemba cheusi cha kung’aa na viatu vyeusi virefu (skuna), muda wote wa hafla hiyo Amina alikuwa anakunywa maji.
Tulikuwa waandishi watano kutoka vyombo tofauti tumekaa eneo la wazi ndani ya hoteli hiyo, ndipo alipojongea karibu nasi na kukaa kwenye mkono wa kulia wa kiti (sofa) cha mtu mmoja nilipokuwa nimekaa mimi.
Alishiriki katika mazungumzo yetu na kutuhakikishia kuwa hawezi kusahau alipotoka hata baada ya kufanikiwa kuwa mbunge. “Jamani, mie siwezi kubadilika, naamini na kuenzi nilikotoka,” alisema.
Akatabasamu na kuweka mkono wake wa kushoto kwenye bega langu la kulia ili akae sawa (balance), wakati huo miguu yake ilibebana na kuendelea kusema: “Mi najua bila vyombo vya habari nisingefika hapa nilipo…mmenisaidia sana kama mwenzenu, hivyo kuwachunia itakuwa ngumu,” alisisitiza Amina.
Kabla ya hapo nilipata kuzungumza naye mara kadhaa kwenye simu baada ya mkutano wa mwaka wa Chama cha Waandishi wa Habari Tanzania (TAJA) uliofanyika Septemba mwaka jana.
Nilikuwa nikiwasiliana na Amina nikiwa kama mjumbe wa chama hicho ili kuthibitisha kama atakuwa mlezi wetu, ahadi aliyoitoa kwa Katibu wa chama hicho, Hamza Kondo, akiwa bungeni na kuchangia sh 500,000 kama sehemu ya mchango wake kwa waandishi wa habari kupitia chama hicho.
Nadhani kutokana na kutingwa na majukumu ya hapa na pale na safari ya timu ya taifa (Taifa Stars) kuelekea Msumbiji, Amina hakuweza kufanya hivyo na badala yake aliamua kujitoa kwenye nafasi hiyo kwa maelezo ya kuwa ana mambo mengi.
Maisha ya Amina, binafsi nayachukulia kama kioo nitakachotumia kuniongoza, hasa tabia yake ya kujiamini na kuthubutu.
Kujitoa kwake nafananisha na mshumaa. Alikuwa tayari kuumia na mara kadhaa alisema yupo radhi kufa kwa ajili ya kutetea vijana wenzake.
Juni 26 kila mwaka kuanzia sasa, naishauri serikali na vijana wenzangu kuiadhimisha kwa kumkumbuka mwenzetu, Amina Chifupa.
Natoa pole kwa mtoto wake Abrahaman Mpakanjia, ndugu, jamaa na marafiki wote walioguswa na kifo cha Amina, kwa imani kuwa ipo siku tutakutana mbele ya haki.
Mungu ailaze roho ya Amina Chifupa mahala pema peponi. Amin!