AMINA Chifupa Mpakanjia (26), amefariki dunia juzi katika Hospitali ya Jeshi ya Lugalo alikokuwa amelazwa kwa takriban wiki moja akiugua homa kali na kisukari.
Mengi yamesemwa kuhusu mbunge huyu kijana aliyejijengea jina kubwa katika kipindi kifupi kabisa kutokana na namna alivyojitoa mhanga akitetea maisha ya vijana wenzake wengi.
Amina anaondoka akikumbukwa kama mmoja wa watangazaji bora wa redio, mbunifu mzuri wa vipindi, mwanasiasa chipukizi asiyekata tamaa, msema kweli na mwanamke jasiri.
Mengi yamesemwa kuhusu Amina Chifupa ambaye aliingia bungeni kwa mara ya kwanza Desemba mwaka 2005 akipitia katika kundi la Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Baadhi ya watu wanaomfahamu mbunge huyo aliyejitoa mhanga kupambana na biashara haramu ya dawa za kulevya hata kufikia hatua ya kuwa tayari kupoteza maisha yake, wamesema maneno mengi yanayohuzunisha kuhusu msiba huo mkubwa.
Rais Jakaya Kikwete katika salamu zake, amewataka vijana wa Tanzania kuyaendeleza mema yote aliyoyasimamia mwanasiasa huyo, hususan mapambano yake dhidi ya dawa za kulevya.
Waziri Mkuu, Edward Lowassa, yeye alimsifu Amina kwa namna alivyojitoa kupigania masilahi ya vijana wenzake na akatoleo mfano wa harakati zake za kupambana na biashara hiyo haramu ya dawa za kulevya.
Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema, Freeman Mbowe, naye pia alimwelezea Amina kuwa mwanasiasa mkweli, hodari, ambaye alikataa sifa ya unafiki ambayo wanasiasa wengi wanayo.
Emmanuel Nchimbi, Mwenyekiti wa Taifa wa Umoja wa Vijana amewataka Watanzania, ndugu, marafiki, wazazi na aliyekuwa mume wa Amina kuyakubali matokeo, akisema hiyo ni kazi ya Mungu, isiyo na makosa.
Kabwe Zitto, mmoja wa wabunge vijana, yeye amekwenda mbali zaidi na kumfananisha mwanasiasa huyo chipukizi na gwiji la siasa za kudai uhuru, Bibi Titi Mohammed.
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Samuel Sitta, wakati akitangaza kuhusu msiba huo bungeni jana alieleza bayana kuguswa na tukio hilo, akimwelezea Amina kama mfano wa wanasiasa hodari.
Maneno hayo yote ni sehemu tu ya mengi yaliyosemwa na watu mbalimbali hapa nchini, ambao kwa namna moja au nyingine wameguswa sana na msiba huu mkubwa na wa aina yake.
Pamoja na yote hayo, tunatambua kuwa Amina ametangulia kwa Mola na ametutoka tukiwa bado tunamhitaji sana kama taifa kutokana na namna alivyojitoa mhanga kulipigania.
Katika kipindi kifupi cha miezi takriban 18 aliyokaa bungeni, Amina alithibitisha pasipo shaka kwamba, alikuwa mwanasiasa makini na mwenye upeo mkubwa tofauti na ilivyokuwa wakati alipata nafasi hiyo.
Ni jambo la kusikitisha sana kwamba, taifa hili limempoteza mwanasiasa kijana ambaye kazi aliyokuwa ameianza ya kuwapigania vijana wenzake na ya kuhakikisha anawalinda dhidi ya ujinga, umaskini na dhidi ya athari za kutumia dawa za kulevya hajaimaliza bado.
Tunapenda kuwaasa wabunge wengine vijana ambao wamebaki bungeni na wale walio nje ya Bunge, kusimama na kuanzia pale alipoishia mpiganaji huyo hodari kama njia bora kabisa ya kumuenzi jemedari kijana aliyethubutu kutenda kile kilichowashinda wengi.
Watanzania tuna kila sababu ya kukiri kwamba, kwa kipindi kifupi cha ubunge wake, tuliweza kubaini kuwa taifa lilikuwa limepata aina ya wanasiasa wapambanaji, waliokuwa wamejitoa mhanga kupambana na kila aina ya dhuluma katika jamii. Si rahisi kusema kila jambo kwa ufasaha ingawa kila mtu makini anatambua kuwa taifa limepoteza