WANANCHI wametakiwa kuacha woga pindi wanapopigania haki zao sehemu za kazi.
Hayo yalielezwa na aliyekuwa mtumishi mstaafu wa Baraza la Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFC) Dk. Peter Temu katika uzinduzi wa kitabu alichokitunga kinachoitwa ‘Fighitng to Keep My Job’ uliofanyika juzi katika Hoteli ya Moven Pick, Dar es Salaam.
Alisema kitabu hicho amekitunga kutokana na tabu alizozipata kwa aliyekuwa katibu mkuu wake wa fedha 1976, katika kipindi cha utawala wa hayati Mwalimu Nyerere.
Alisema katika kipindi hicho bila ya juhudi zake na kutetewa na rais huyo kwa kipindi hicho angekuwa ameshafukuzwa kazi kutokana na hila alizokuwa anafanyiwa na katibu mkuu huyo.
Naye mgeni rasmi katika uzinduzi huo, Mwenyekiti wa IPP, Reginald Mengi, alisema kutokana na kitabu hicho kuwa na umuhimu na chenye historia ya kweli ni mfano wa kuigwa na kila mtu ili aweze kupigania haki katika sehemu yake ya kazi.
Alisema katika utunzi huo, Dk. Temu amepitia katika harakati nyingi za kudai haki katika kazi hadi ilivyofikia hatua ya kupandishwa kwa cheo na kuwa mwenyekiti wa NICO.