SHIRIKA la Nyumba la Taifa (NHC), limesema nyumba ya Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Nyerere, iliyopo Magomeni, Dar es Salaam, haivunjwi bali inafanyiwa ukarabati na kuwa sehemu ya biashara.
Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo, Antony Komba, alieleza hayo jana alipozungumza na waandishi wa habari katika makao makuu ya ofisi hizo zilizopo, Temeke, Dar es Salaam.
Alisema jengo hilo linatarajiwa kuanza kujengwa Oktoba mwakani kuwa ghorofa nane, ambalo litagharimu sh milioni 956.
Alitaja sababu za kuamua kujenga jengo hilo ni ili kuwa kivutio kwa watalii, kuwa kumbukumbu na sehemu ya biashara, ili kuondoa msongamano katika jiji na kuonyesha njia katika mwendelezo wa miji, ili kupunguza msongamano.
“Jengo hilo halitavunjwa bali litajengwa vizuri na tutalipa jina la ‘Mwalimu Art Gallery’ kama kumbukumbu ya taifa kwa kuwa ndiyo nyumba ambayo alikuwa anaishi wakati wa kupigania uhuru mwaka 1956,” alisema Komba.
Naye Mkurugenzi wa Ujenzi wa Shirika hilo, Nathaniel Malisa, alisema baada ya kukamilika kwa ujenzi huo, kitakachofuata ni kuweka vitu vya kitalii, ili kuvutia watu wa nje na wa ndani kuweza kwenda kuwekeza katika jengo hilo.
Hivi karibuni kumeibuka utata kuhusu uvunjwaji wa nyumba ya Mwalimu Nyerere, na vyombo mbalimbali vya habari vimekuwa vikinukuu maneno ya watu pamoja na wapangaji waliokuwa wakiishi ndani ya nyumba hiyo.