WAZIRI Mkuu, Edward Lowassa, amesema katika mwaka ujao wa fedha, serikali inakusudia kuanzisha halmashauri mpya 11 katika mikoa mbalimbali nchini.
Lowassa aliyasema hayo jana wakati akiwasilisha bungeni Mapitio na Mwelekeo wa Kazi za Serikali na Makadirio ya Matumizi ya Fedha ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Mfuko wa Bunge kwa mwaka ujao wa 2007/08.
Alizitaja halmashauri hizo mpya zitakazoanzishwa kuwa ni Arusha, Meru, Bahi, Chamwino, Rorya, Chato, Longido, Mkinga, Nanyumbu, Siha na Misenyi.
Mbali ya hilo, Lowassa aliliambia Bunge kuwa, serikali imekubali kupandisha kwa asilimia 100, posho za madiwani kutoka kiwango cha sh 30,000 za sasa hadi sh 60,000 kwa mwezi kuanzia mwaka ujao wa fedha.
Pamoja na maamuzi hayo mazito ambayo kwa kiwango kikubwa yataathiri mwenendo wa mambo, Lowassa alikiri kuwa, kasi ya sasa ya ukuaji wa uchumi wa taifa haiwezi kuiondoa nchi katika tatizo la umaskini.
“Tuna changamoto kubwa ya kukuza uchumi wetu kwa kasi kubwa zaidi,” alisema Lowassa baada ya kueleza kuwa kwa mujibu wa wataalamu wa uchumi, ili nchi iweze kujiondoa katika lindi la umaskini, ni lazima ukuaji wa pato la taifa usipungue asilimia saba hadi 10 katika kipindi cha miaka mitano mfululizo.
“Ukweli huu unatukumbusha falsafa ya hayati Mwalimu Nyerere inayosema, nanukuu: “Lazima tukimbie wakati wenzetu wanatembea.” Kimsingi kasi ya sasa ya ukuaji wa uchumi haiwezi kutuondoa kwenye umaskini,” alisema.
Lowassa alisema kila mwananchi mahali alipo, anatakiwa kuwa na dhamira na kuamua kuukataa umaskini kwa nguvu zake zote na kutafuta maendeleo kwa kila fursa inayojitokeza.
Alibainisha kuwa, imebakia miaka takriban saba, kufikia malengo ya milenia na miaka 18 ya kufikia malengo ya Dira ya Maendeleo ya Taifa (2025).
Alisema miaka hiyo si mingi na muda unakwenda kwa kasi kubwa, hivyo nchi inakabiliwa na changamoto kubwa ya kukuza uchumi kwa kasi kubwa zaidi.
Alisema viongozi wanawajibika kuhakikisha kuwa kila mtu mwenye uwezo wa kufanya kazi anafanya hivyo kwa bidii na ili kuonyesha msisitizo wa suala hilo, Lowassa alinukuu maneno yaliyopata kutumiwa na Yesu Kristo katika Biblia yasemayo: ‘Asiyefanya kazi na asile.’
“Kwa kweli tunahitaji kuwa wabunifu zaidi, ili tusibaki kutamani tu maendeleo ya wengine, bali kila mwananchi ajitume kutafuta maendeleo pale alipo,” alisisitiza.
Aidha, Lowassa alisema changamoto nyingine inayolikabili taifa hivi sasa ni nidhamu katika matumizi ya fedha za umma na kubainisha kuwa fedha zote ambazo serikali inazikusanya kwa njia ya kodi na misaada ni mali ya Watanzania na ni lazima zitumike kwa kuzingatia kanuni na taratibu.
Ili kuhakikisha hilo linatimizwa, aliziagiza halmashauri na mikoa kukamilisha taratibu za kuunda kamati za ukaguzi kama ilivyo katika ngazi ya wizara.
“Katika mwaka ujao wa fedha, kila afisa masuuli ahakikishe kuwa anafuata miongozo bora ya uhasibu na utunzaji wa fedha. Vile vile, awasiliane na wakaguzi kutatua matatizo na siyo kutafuta sababu za kushindwa kutimiza wajibu wake,” alisema.
Alibainisha kuwa pamoja na changamoto zilizopo na mahitaji makubwa ya rasilimali ili kufikia malengo yaliyowekwa, nchi ina uwezo na rasilimali za kutosha.
“Uwezo tunao na rasilimali tunazo. Kinachotakiwa ni kujenga mshikamano na umoja katika kuwatumikia wananchi,” alisema.
Lowassa aliliomba Bunge liidhinishe matumizi ya zaidi ya jumla ya sh trilioni 1.465 kwa ajili ya Ofisi ya Waziri Mkuu na zaidi ya sh bilioni 42.718 kwa ajili ya Mfuko wa Bunge, ikiwa ni mishahara, matumizi mengine na fedha za maendeleo za ndani na nje.
Akichanganua matumizi hayo, Lowassa alisema fedha zinazoombwa kwa ajili ya Ofisi ya Waziri Mkuu ni sh 122,773,366,500, ambapo za matumizi ya kawaida ni sh 48,808,296,000 na matumizi ya maendeleo ni sh 73,865,070,500.
Aidha, aliomba sh 117,265,770,000 kwa ajili ya TAMISEMI na sh 141,511,054,500 kwa ajili ya ofisi za wakuu wa mikoa na pia sh 1,084,080,766,000 kama ruzuku kwa halmashauri.
Lowassa alitumia fursa hiyo pia kuwaonya viongozi wa mikoa na wilaya kwa kushindwa kwao kuwajibika, hali inayosababisha wananchi wenye shida walazimike kuwatafuta viongozi wa kitaifa, ili kutatuliwa matatizo yao.
Katika hotuba yake, Lowassa aliwakumbusha viongozi hao kuwa changamoto ya kutatua kero za wananchi inahitaji kila mtumishi wa umma kuwajibika ipasavyo katika majukumu aliyopewa.
“Katika hali ya kawaida, sitarajii mwananchi yeyote kwa mfano, mwenye tatizo la mpaka wa shamba katika Kijiji cha Kasharu katika Mkoa wa Kagera, aende Dar es Salaam kutatuliwa matatizo yake na kumwacha mkurugenzi wa halmashauri husika, mkuu wa wilaya, mkuu wa mkoa na viongozi wengine katika ngazi mbalimbali. Akifanya hivyo, maana yake ni kwamba, alikotoka uongozi hauwajibiki ipasavyo,” alisema.
Lowassa alisema ana imani kuwa, asilimia 95 ya kero zinazofikishwa kwa viongozi wa kitaifa na wananchi, zinaweza kushughulikiwa na kutatuliwa katika ngazi ya wilaya, mkoa na wizara.
Alisema sheria za Serikali za Mitaa na sheria ya Tawala za Mikoa zilifanyiwa marekebisho mwezi Februari mwaka huu, ili kuwezesha kuanzishwa kwa kamati za ushauri za mikoa.