ZAIDI ya wanafunzi 100 wa kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari ya Bungulwa, iliyopo wilayani Kwimba, Mwanza, wamefukuzwa shule kutokana na kile kilichoelezwa kutofanya mtihani wa darasa la saba.
Imeelezwa wanafunzi hao walitimuliwa shuleni hapo Mei mwaka huu, baada ya Ofisi ya Ukaguzi Elimu Kanda ya Ziwa kubaini mchezo mchafu uliofanywa na baadhi ya walimu wa shule hiyo kwa kushirikiana na walimu wa shule za msingi walikotoka wanafunzi hao.
Habari hizo ambazo pia zimethibitishwa na Mkuu wa Wilaya hiyo, Danh Makanga, zimebainisha kwamba, wanafunzi hao wametimuliwa huku wengi wao wakifutiwa matokeo ya mitihani ya kidato cha pili, iliyofanyika kitaifa mwaka jana.
Kwa mujibu wa habari hizo, miongoni mwa wanafunzi hao inadaiwa hawakuwa na sifa za kuendelea na masomo kwa vile walijiunga na masomo ya kidato cha kwanza pasipo kufaulu mitihani ya darasa la saba, kama sera ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi inavyohimiza.
Vyanzo vya habari kutoka wilayani humo vimeeleza kuwa wanafunzi hao ‘walizolewa’ na mwalimu mkuu wa shule hiyo, Medard Dominic baada ya kupokea kitu kidogo kutoka kwa wazazi wa wanafunzi hao.
Kadhalika, habari hizo zimeongeza kwamba tume iliyoundwa na Ofisi ya Ukaguzi Elimu Kanda ya Ziwa kuchunguza madai hayo ilibaini kwamba mwalimu mkuu huyo, Dominic alikuwa hawasilishi ada za wanafunzi kwa muda mrefu, hali ambayo pia ilisababisha wanafunzi zaidi ya 60 wazuiliwe kufanya mitihani ya kidato cha pili.
Akizungumza na Tanzania Daima kwa njia ya simu, Mkuu huyo wa Wilaya, Makanga, alikiri kuwapo kwa tukio hilo na kusema tayari linashughulikiwa na Ofisi ya Elimu wilaya na mkoa.
Akielezea zaidi dhidi ya hali hiyo, Makanga alisema ofisi yake haina mamlaka ya kutoa uamuzi juu ya suala hilo na kwamba maamuzi yatakayotolewa na Ofisi ya Eilimu wilaya na mkoa ndiyo yatakayotekelezwa.
Ofisa mmoja kutoka Ofisi ya Ukaguzi Kanda ya Ziwa alisema suala hilo lipo mikononi mwao pamoja na Ofisi ya Elimu ya wilaya na mkoa kwa ujumla na kuongeza kuwa hatua kali za kinidhamu na kisheria zitachukuliwa kwa wahusika watakaobainika kufanya mchezo mchafu huo.
“Mimi si msemaji wa ofisi ya ukaguzi, lakini ninachofahamu ni kwamba ni kweli wanafunzi hao wametimuliwa, na taratibu za kumwajibisha mwalimu mkuu wa shule hiyo zinaendelea,” alisema ofisa huyo ambaye aliomba jina lake lisitajwe.
Jitihada za Tanzania Daima za kumpata mwalimu mkuu huyo ili aweze kuzungumzia tuhuma hizo hazikuzaa matunda kutokana na simu yake ya kiganjani kutopatikana mara kwa mara alipotafutwa.