AHADI iliyotolewa na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Jakaya Kikwete, na aliyekuwa Katibu Mwenezi wa chama hicho, Ramadhani Mapuri, pamoja na Meya wa Kinondoni, Salum Londa, kusaidia ujenzi wa nyumba ya familia ya marehemu Mwajuma Nyanza, haijatekelezwa.
Nyanza ambaye alikuwa Katibu Mwenezi wa CCM Tawi la Midizini, alifariki dunia pamoja na watoto wengine watano baada ya nyumba yao kuchomwa moto kwa sababu za kisiasa Septemba 8, mwaka jana.
Katibu wa Kata ya Manzese, Abdallah Kidoga, alisema jana kuwa mpaka sasa hakuna ahadi yoyote zaidi ya ile ya mabati 20, ceiling board 15 na mifuko 15 ya saruji, waliyozawadiwa na Mkurugenzi wa African Stars Entertainment, Asha Baraka.
Kidoga alisema Baraka alitoa zawadi hizo katika bonanza lililofanyika miezi mitatu iliyopita katika Ukumbi wa Travertine Magomeni, Dar es Salaam na kugawa vifaa hivyo pamoja na fedha taslimu sh 100,000 kwa ajili ya marekebisho ya chumba cha marehemu huyo.
Nyanza alifariki dunia baada ya nyumba yake kuchomwa moto. Wengine waliofariki dunia katika tukio hilo la kisiasa ni watoto wake wawilii na wajukuu watatu.
Alisema matengenezo ya nyumba ya marehemu Nyanza yanatarajiwa kuanza siku chache zijazo baada ya viongozi wa kata kuanza mikakati ya kumtafuta fundi wa kufanya matengenezo ya nyumba hiyo.
Kidoga alisema kwa kuwa marehemu Nyanza aliacha kiwanja katika eneo la Mbezi, wataelekeza nguvu zao katika kiwanja hicho ili familia hiyo ipate mahala pa kuishi.
“Nimeshangaa kusikia Rais Kikwete ameshatoa mchango wake katika familia hiyo ambao ni sh milioni 4, taarifa hiyo si sahihi,” alisema. Alisema viongozi wa Kata ya Manzese wako karibu na familia hiyo na wanafanya kila wawezalo kuisaidia familia hiyo. Jaribu kufanya nao taratibu zinazotakiwa si kama jinsi baadhi ya watu wanavyovumisha vitu ambavyo si vya kweli