Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Benki Kuu yamshinda Meghji
Benki Kuu yamshinda Meghji
By Habari Tanzania | Published  06/24/2007 | Habari za Kitaifa | Rating:
na Charles Mullinda


MLOLONGO wa kashfa zinazoiandama Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ambayo ni taasisi iliyo chini ya Wizara ya Fedha, unaelekea kumuelemea Waziri wa Fedha, Zakia Meghji.

Kashfa kubwa ambayo imedumu kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa, ya gharama kubwa kuliko hali halisi ya ujenzi wa minara pacha miwili ya benki hiyo, imeshindwa kupatiwa ufumbuzi, licha ya wabunge kuipigia kelele serikali kwa kipindi kirefu kuwa kuna kila dalili za ubadhirifu wa fedha za mali ya umma katika gharama za ujenzi huo.

Ingawa Meghji katika hotuba yake ya kuhitimisha mjadala wa bajeti ya mwaka wa fedha 2007/2008 aliyoitoa bungeni ijumaa iliyopita alieleza kuwa serikali imekwishatoa maelezo kuhusu gharama za ujenzi wa minara hiyo, kauli hiyo imeshindwa kuisafisha BoT dhidi ya tuhuma zinazoiandama za kutumia mabilioni ya fedha za Watanzania kinyume cha taratibu kwa kisingizio cha ujenzi huo.

Katika tamko lake la Ijumaa, Meghji aliwakumbusha wabunge kuwa serikali imekwishatoa maelezo kuhusu gharama za ujenzi wa BoT, Mwananchi Gold Meremeta, na kampuni ya Alex Stewart Assayers hapo hapo bungeni na katika kamati ya bunge ya fedha na uchumi.

“Napenda kulikumbusha Bunge lako tukufu kwamba maelezo ya kina kuhusu masuala ya gharama za ujenzi wa Benki Kuu, Mwananchi Gold, Meremeta, na Kampuni ya Alex Stewart Assayers niliyatoa hapa bungeni wakati Bunge hili likijadili muswada wa sheria ya Benki Kuu ya Tanzania mwezi Aprili 2006.

“Na pia wakati wa majumuisho yangu ya bajeti ya mwaka 2006/07, mwezi kama huu mwaka jana. Licha ya kutoa maelezo hayo bungeni, ufafanuzi kuhusu masuala haya pia ulikwishatolewa mara nyingi kwa Kamati ya Bunge ya Fedha na Uchumi. Kwa kuwa maelezo yaliyokwishatolewa yanajitosheleza, nisingependa kuyarudia tena kwa kuwa hakuna maelezo ya ziada.

“…Kuhusu habari zinazosambazwa katika mtandao wa internet zinazomshutumu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania. Serikali inazo taarifa hizo zinazotoa shutuma mbalimbali dhidi ya Gavana wa Benki Kuu na baadhi ya wafanyabiashara hapa nchini.

“Hata hivyo, serikali haiwezi kutoa tamko lolote kwa kuwa chanzo cha habari hizo hakijathibitishwa, na mara nyingi habari za internet hazina uhakika kama ni za kweli au za uongo. Aidha, serikali ina vyombo vyake vya kufuatilia mambo haya.”

Kauli hiyo ya Meghji haikidhi madai ya baadhi ya hoja za wabunge za kuwepo kwa kashfa ya ufujaji wa mabilioni ya fedha unaodaiwa kufanywa na maofisa wa BoT kwa kushirikiana na baadhi ya wafanyabisahara katika mradi huo.

Wabunge kwa kipindi kirefu wameonyesha wasiwasi wa wazi kuhusu suala hilo baada ya kupatikana kwa taarifa kwamba, ujenzi wa kila meta za eneo katika majengo hayo, ni kubwa kuliko hata zile za ujenzi wa kila meta moja ya eneo katika miji mikubwa ya New York, Marekani au Tokyo, Japan.

Wasiwasi huo wa wabunge unaongezewa nguvu na taarifa ambazo zinasambazwa katika mtandao wa intaneti zikieleza kuwa, wakati ujenzi wa jengo jipya la Benki Kuu ya Tanzania unaojumuisha minara pacha miwili unafikia dola 8,625 za Marekani (sh milioni 11.2) kwa kila meta za eneo, gharama za ujenzi wa kila meta moja ya eneo katika miji ya New York na Tokyo za jengo lililokwishanakshiwa hazifikii dola 2,000 (sh milioni 2.6).

Habari hizo zinaeleza kuwa, gharama hizo za ujenzi wa BoT kwa kila meta za eneo ambazo ni kubwa mara nne zaidi ya zile zinazotumika katika nchi za Marekani na Japan, hazijawahi kutumika katika nchi yoyote ya Afrika.

Kwamba ingawa gharama halisi ya ujenzi wa kila meta moja ya eneo ya jengo hilo zilizopaswa kutumika ni dola 700 (sh laki tisa), baadhi ya viongozi wa BoT waliukataa ushauri wa wataalamu wa ujenzi wa Bodi ya Wahandisi Tanzania, Bodi ya Usanifu wa Majengo na Bodi ya Ukarandasi uliokuwa ukipinga gharama zilizotumika kujenga kila meta ya eneo ya jengo hilo.

Kwa gharama zilizotumika sasa za dola 8,625 kwa kila meta moja ya eneo, kwa meta 40,000 za eneo za jengo hilo la BoT, ujenzi wake tayari ulikuwa umeshagharimu dola milioni 80 (sh bilioni 104), kabla ya kumalizika kwa mradi.

Kukataliwa kwa ushauri wa kitaalamu wa Bodi ya Wahandisi wa Tanzania, Bodi ya Usanifu wa Majengo na Bodi ya Ukandarasi za kupinga gharama kubwa zilizoteketea katika minara pacha ya BoT kumeelezwa kuwa kulifanywa kwa makusudi na baadhi ya viongozi wa BoT.

Habari zaidi zinaeleza kuwa, mmoja wa viongozi wakuu wa BoT alifanikiwa kushinikiza matumizi ya dola milioni 345 (sh bilioni 448.5) ili kuendelea na ujenzi wa minara hiyo, kwa gharama ile ile ya dola 8,625 kwa kila meta moja ya eneo.

Wakati kukiibuka habari za matumizi makubwa kupita kiasi ya ujenzi wa minara hiyo, kumekuwepo na tuhuma nyingine za kuwapo kwa rushwa katika mradi huo zilizoibuka mwaka 1998 na kuifanya kampuni ya Sweden ya Skanska inyang’anywe mradi huo baada ya kutuhumiwa kumhonga gavana wa BoT, dola milioni tano (sh bilioni 6.5).

Kwamba ingawa kampuni hiyo ilinyang’anywa mradi huo, bado iliendelea kupewa tenda mbalimbali zinazohusu mradi huo kupitia Kampuni ya Group 5, kampuni tanzu ya Skanska ya Afrika Kusini.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.