Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Mwalilia kipi kwenye bajeti hii ?
Mwalilia kipi kwenye bajeti hii ?
By Habari Tanzania | Published  06/23/2007 | Habari za Kitaifa | Rating:
NAANZA kwa kuwaambia komeni tena komeni hadi mkomae. Ninyi watu wa majungu tu mnaochungulia kwenye jungu.

Ebo!

Kwani cha mno ni kipi hadi muanze kupayuka na kulia eti bajeti ya mwaka huu ni mbaya tena mbovu? Nasema acheni za kuleta wanakwetu. Hiyo ni bajeti ya kuleta maisha bora kwa kila mwanakaya nawaapia.

Eti ghafla kila mmoja wenu keshajipachika utaalamu wa uchumi siyo? Kila kona mwapiga kelele eti hii bajeti ni mzigo mkubwa!

Kumbe mlitaka iweje? Kwani serikali ndiyo iliyowaleta huku ulimwenguni hadi mtake iwalee? Nawaambia nyie mlitarajia bajeti kama ya kuombea kura ili wapate kula? Hapa sina mzaha hata kidogo, mikanda mtaikaza hadi viuno vikatike. Nasema humo simo wala simo kabisaa.

Kwani ni mara ya kwanza kusikia bidhaa kama bia na sigara zikiongezewa ushuru? Mbona kila mwaka ndiyo staili hiyo mwanakwetu?

Ninyi kwa akili zenu finyu mlitaka watu wasumbue vichwa vyao kufikiria vyanzo vingine vya mapato siyo? Hamjui msemalo nawaapia. Usumbue kichwa kufikiri kusudi iweje? Mbona unachukua tu ya mwaka jana unabadili tarakimu kwa kwenda mbele?

Ya nini kugundua vyanzo vya mapato wakati kila mmoja anafahamu wazi kwamba sigara, bia na soda ndio mradi wa kuongezea makusanyo? Endeleeni kulia tu hadi mliwe. Nshakimbia katika hilo mtoto wa mama.

Hamkawii kuniuliza mbona wapinzani wameweza kuainisha vyanzo vingine vya mapato katika bajeti kivuli yao. Wao si wanapigania madaraka bwana? Wacha watumie mbongo kufika kwenye hatamu. Waliofika watumie nguvu za nini? Au kwa upungufu wenu wa akili mlitaka watu kama wa madini watozwe kodi kubwa zaidi siyo?

Ninyi mwafanya mzaha. Hamjui wamewekeza ili wavune? Kinachowauma ninyi ni kipi zaidi kama wanavuna tulipowaruhusu kupanda? Mbona mnakuwa hamnazo? Nawaambia huko siko kabisa miye.

Watu mnaofikiria kuwa na akili timamu mwajidai kulia machozi eti kodi ya mafuta imeongezwa. Ebo! Kwani mwataka nani agharamie matumizi ya serikali? Si ni jukumu lenu ninyi mlioiweka madarakani? Mwataka hayo mashangingi yakae juu ya mawe siyo? Nakuapia hilo halitokei. Lazima mashangingi yatembee hata kama kwa kufanya hivyo mtashindwa kumudu kununua mafuta ya taa. Lazima nijitoe.

Inawahusu nini ninyi linapokuja suala la kupanda bei mafuta? Kwani mnachotakiwa si kujifunga mkanda tu? Kama matobo yamekwisha nawashauri mtoboe mengine ili viuno vienee. Ninyamaze kabla sijawatusi! Ninyi mlitaka tupandishe kodi kwenye kitu gani hasa kama si mafuta? Mwataka kwa akili yenu tuwafutie wawekezaji likizo ya kodi? Nasema acheni hizo za kuleta. Huko uswahilini kwenu si mnasema kufa hamfi lakini cha moto mtakiona? Hayo si yangu, ni mtaani mwanakwetu.

Mwalialia nini wakati hakuna cha ajabu katika hii bajeti? Mbona hii ina unafuu kuliko wale waliosema eti ni afadhali kula nyasi kuliko tushindwe kujinunulia dude la kurukia angani?

Mwajidai softisofti sana kiasi kwamba hamtayamudu maisha ya kupikia kwa mkaa? Si nawasikia mkilalama eti hiyo kodi ya mafuta kupanda sasa ndio mwanzo wa kutumia kuni na mikaa kama vile hamna akili nzuri?

Mnalalamika nishati ya kupikia inakuwa ghali? Kwani hicho cha kupikwa tayari mnacho ghalani?

Nawaambia miye simo katika yote haya. Mtaimba sana mwaka huu ninyi na wapinzani wetu lakini ndio hivyo tena. Machozi ya samaki shuruti yachukuliwe na maji. Nikimbie mbio katika hili mwanangu! Simo.

Zaidi ya hayo ninyi mwajidai wazalendo sana sio? Kwani si mlipopiga kura zenu mliwachagua wa kutusemelea kwenye hilo jumba huko Dodoma? Mwandishi mmoja uchwara anapaita Dodoma ni makao makuu yasiyokuwa maskani makuu. Sipo kwenye huo utani. Nirudi kwenye hoja. Si tuna wasemaji wetu huko Dodoma?

Sasa hivi vijibunge vya kujiundia vilabuni vimetokea wapi Yarabi? Kila kilabu unachopita unasikia watu wakijidai eti wanaichambua bajeti. Mwatka tuamini ninyi sio mbumbumbu sio? Mnajidai mna kajiuelewa fulani hivi eti eh? Mngekuwa na ubavu ninyi si ndio mngepewa hiyo kazi ya kuandaa bajeti? Nawaambia komeni tena mkomae.

Wakubwa si mnawasikia wakiiikosoa kwa bidii halafu mwisho wanaiunga mkono mia kwa mia?

Cha ajabu ni kipi kusikia mtu akitaja mapungufu milioni kidogo halafu akaamua potelea mbali ngoja niunge mkono hoja? Kwani hamjui cha muhimu ni haja sio hoja? Mtashangaa sana mwaka huu. Kama mlidhani anayetaka kushangaa lazima aende feri basi ujue mmeliwa tena mkiwa wimawima. Kila siku si nawaambia vya kushangaza viko vingi? Miye simo huko.

Kwani mlitaka watukufu wapingane na watukufu wenzao?

Ninyi ni kabila gani ambalo bado kujifunza kwamba au tunasimama pamoja au tunaangamia pamoja? Kwani hamjui kwamba hata mitambo hulainishwa na mafuta ikalainika?

Mmesahahu wenyewe kwamba pesa ni sabuni ya roho sio? Na kale kamsemo kanakosema nipe-nikupe nako ni kageni kwenye masikio yenu? Msinipe tafsiri mnazotaka kunipa miye ila nasema mambo bado mabichi, kama kulia mtalia hadi machozi yakauke? Nikae kimya kabla sijaitwa mchochezi. Simo tena nasema kwa sauti kubwa kwamba simo.

Kwa hiyo ninyi kwenye hiyo bajeti mlivyo na akili nyepesi kuliko mbu mlitegemea tutenge mapesa kibao kwa ajili ya kilimo sio? Mwa’nchekesha mtoto wa mama. Tupeleke mapesa kwenye kilimo ili iweje? Tuache mambo muhimu kwa watu muhimu ndio maoni yenu sio? Kilimo si ndio uti wa mgongo wa uchumi wetu? Mwaonaje tukianza sasa kuwekeza zaidi kwenye miguu na mikono halafu huo uti tutaushughulikia katika siku za usoni? Nani aliwadanganya umuhimu ni sawa na ulazima? Kwani hata mkishindwa kulima hapa kwenu si tuna hayo maduka mnayaita supamaketi yanauza bidhaa za kilimo kuanzia kwa mayahudi hadi kwa wale mliokuwa mkiwaita makaburu. Huko nasema tena simo.

Inawezekana wapo waliokuwa wakiota ndoto kusikia kwamba sasa mikopo ya chuo kikuu ni asilimia mia moja. Thubutu! Nani kawadanganya ninyi nanyi mnahitaji bahati kama ya wakubwa?

Kwa kuwa wao walisoma bure mwataka nanyi msome bure eti eh? Kwani nani kawaambia Nyerere amerudi kuongoza kaya yetu? Miye nasema lazima nijitoe kabisa katika haya yote tena bila khofu. Simo tena simo kabisaaa!

kevinmakyao@hotmail.com
0784 265072


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments
  • Comment #1 (Posted by saronge)
    Rating
    Ndugu yangu article yako safi sana, wantanzania ndio zao wacha wakome na bado, walipokuwa wakipewa doti moja ya kanga na kutoa kura za ndio mzee, walitegemea nini? hata mimi simo kabisaa!!! tena katika vilio vyao sauti yangu haimo kabisaa.


     
Submit Comment


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.