Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Meghji amejaribu lakini ametuonea…
Meghji amejaribu lakini ametuonea…
By Habari Tanzania | Published  06/23/2007 | Habari za Kitaifa | Unrated
BUNGE la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jana lilipitisha bajeti ya serikali ya mwaka 2007/2008 baada ya serikali kuifanyia marekebisho kadhaa.

Miongoni mwa mambo yaliyorekebishwa katika bajeti hiyo ni uamuzi wa serikali kuondosha ushuru wa mafuta ya taa na marekebisho ya leseni za magari.

Akihitimisha mjadala wa bajeti hiyo jana, Waziri wa Fedha, Zakia Meghji, alisema hatua ya kuondoa ushuru huo kwenye mafuta ya taa na leseni za magari, imetokana na kilio na maombi ya wabunge na wananchi waliokitoa tangu alipowasilisha bajeti hiyo wiki iliyopita.

Waziri Meghji alisema kiasi cha shilingi nne zilizokuwa kwenye mafuta ya taa zitahamishiwa kwenye mafuta ya petroli na dizeli.

Alisema pia kwamba, mbali ya kufuta ushuru huo kwenye mafuta ya taa pia serikali ilisikiliza kilio cha wananchi juu ya gharama za leseni za magari ambazo zilikuwa zimepandishwa wakati wa kuwasilisha bajeti yake wiki iliyopita.

Kutokana na hatua ya kuondoa ushuru kwenye mafuta ya taa, Waziri Meghji alisema serikali itakuwa kali kwa wafanyabiashara watakaojaribu kujichukulia hatua mkononi kupandisha bei ya mafuta kiholela.

Katika bajeti yake aliyowasilisha Alhamisi iliyopita, Waziri Meghji, alisema ushuru wa petroli ungepanda kwa sh 22 zaidi kutoka sh 315 kwa lita za sasa na kufikia sh 337 kwa lita. Aidha, ushuru wa dizeli ungepanda kutoka sh 292 hadi sh 312 kwa lita.

Kabla ya mabadiliko ya jana, ushuru wa mafuta ya taa nao ungepanda kutoka sh 52 kwa lita hadi sh 56 kwa lita, kiwango ambacho sasa kimeondolewa.

Alisema kutokana na hali hiyo, serikali imekubali kufanya mabadiliko ambayo wamiliki wa magari yenye ukubwa wa injini zinazoanzia CC 0 hadi 500, zikiwemo pikipiki na bajaji, watalipa sh 50, 000 badala ya sh 80,000 zilizopangwa awali.

Magari yenye injini za ukubwa wa CC zinazoanzia 501 hadi 1500 yatalipiwa sh 80,000 wakati magari ya CC 1501 hadi 2,500 yatalipwa sh 150,000.

Alisema magari yenye injini za ukubwa wa CC 2,501 hadi 5,000 yatalipiwa sh 330,000 na yale ya ukubwa wa zaidi ya CC 500 yatalipiwa sh 175,000.

Kabla ya mabadiliko ya jana, wiki iliyopita, Meghji alitangaza kwamba, magari yenye ujazo wa injini usiozidi 1,500cc kiwango cha ada kitakuwa sh 80,000 kwa mwaka; kwa magari yenye ujazo wa injini unaozidi 1,500cc lakini hauzidi 5,000cc kiwango cha ada kitakuwa sh 230,000 ambacho sasa kimegawanywa katika makundi mawili zaidi badala ya moja.

Aidha, wiki iliyopita Meghji alisema kuwa magari yenye ujazo wa injini unaozidi 5,000cc kiwango cha ada kitakuwa sh 100,000 kwa mwaka.

Kwanza tunapenda kuipongeza serikali na Waziri Meghji kwa kusikia kwa sehemu kubwa kilio cha wananchi kuhusu ushuru huo katika mafuta ya taa na kwenye leseni za magari.

Lakini tunaipongeza serikali pia kwa kuonyesha namna ilivyo na nia njema ya kukabiliana na tatizo la utegemezi katika bajeti yetu.

Pamoja na pongezi hizo, tunapenda kueleza bayana masikitiko yetu makubwa kwa Waziri Meghji kwa namna alivyowashambulia wanahabari na wabunge wa kambi ya upinzani waliokuwa na mtazamo tofauti katika bajeti.

Tukiwa wanahabari tunaamini Meghji hakututendea haki alipouelezea mtazamo wetu kuwa ni wa kukosa uzalendo kwa sababu tu ya kuiangalia bajeti kwa mtazamo tofauti na ule wa serikali.

Tunaamini kwamba, ukosoaji wetu uliogusia kodi katika mafuta ya taa na kupanda kwa leseni za magari ni moja ya sababu zilizoifanya serikali ifanye mabadiliko katika bajeti yake. Hivi serikali ilitaka uzalendo wa namna gani hasa?

Akizungumza jana, Waziri Meghji alisema si kweli kwamba bajeti ya mwaka huu ni ya kufunga mkanda kama ilivyosemwa na watu mbalimbali wakiwamo wabunge na wananchi.

Meghji alisema mbali ya serikali kuchukua hatua kali, pia Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati Tanzania (EWURA) inatakiwa kuwa kali na macho kusimamia vizuri na kuwa kali kwa wauuzaji wa mafuta.

Huku akionekana kuzungumza kwa hamaki na kwa kujiamini, waziri huyo aliiagiza Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA) kuwa kali kwa wamiliki wa magari yakiwamo daladala kuacha mara moja kupandisha nauli kwa kisingizio cha mafuta.

“Umefika wakati wa SUMATRA kuonyesha makali kwa wamiliki wa magari, ili wasipate mwanya wa kupandisha nauli na usafirishaji wa mizigo kwa madai ya ongezeko la sh 100 tu,” alisema Meghji.

Akitangaza matokeo ya kupitishwa kwa bajeti hiyo, Spika wa Bunge, Samuel Sitta, alisema jumla ya wabunge 271 walipiga kura ambapo kati ya hao 234 walikubali kupitishwa kwa bajeti hiyo huku 36 wakipinga.

Alisema wabunge 49 hawakupiga kura za kupitisha bajeti kutokana na kutokuwapo bungeni.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.