Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Lowassa ageukia kilimo
Lowassa ageukia kilimo
By Manyerere Jackton | Published  06/27/2006 | Habari za Kitaifa | Rating:
Na Manyerere Jackton, Dodoma

WAZIRI Mkuu, Edward Lowassa, amesema ukuaji wa sekta ya kilimo nchini si wa kuridhisha, hivyo ameagiza kuanzia mwaka huu wa 2006/2007, halmashauri za wilaya zianze kuweka shughuli za kilimo cha umwagiliaji katika mipango ya maendeleo ya kilimo ya wilaya.

Waziri Mkuu alitoa agizo hilo jana wakati akiwasilisha bungeni hotuba ya mapitio na mwelekeo wa kazi za serikali na makadirio na matumizi ya fedha ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Bunge ya mwaka 2006/2007. Alisema uzoefu uliopatikana wakati wa kipindi cha ukame, unaonyesha kuwa kilimo cha umwagilia

ji ndiyo njia sahihi ya kukabiliana na athari za ukame. Alisema kwa kutambua hilo, katika mwaka wa fedha wa 2006/2007 serikali itaweka kipaumbe katika ujenzi na ukarabati wa skimu na mabwawa na ujenzi wa miradi mipya, hasa inayoweza kuendelezwa na wananchi wenyewe kwa gharama nafuu.

Pia alisema mkazo utawekwa kwenye teknolojia ya uvunaji maji ya mvua. Aliziagiza halmashauri zote nchini zihamasishe sekta binafsi ziwekeze katika usanifu na ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji.

“Serikali itatoa kipaumbele katika kuwajengea uwezo wataalamu na wakulima katika kilimo cha umwagiliaji, upatikanaji wa pembejeo na zana za kilimo,” alisema.

Katika hatua nyingine ya kuwakwamua wananchi, Lowassa, alisema kuanzia mwaka wa fedha wa 2006/2007, kila mkoa umetengewa sh milioni 500 ili zitumike kuwakopesha wananchi kwa mfumo wa kibenki ili waweze kujikwamua kiuchumi.

“Fedha hizo zitatolewa kwa mtu mmoja mmoja au vikundi kwa njia ya mikopo yenye masharti nafuu na kwa kutumia taratibu za kibenki kulingana na uwezo wa kibiashara wa mwombaji. “Serikali inakusudia kuunda bodi kusimamia mikopo hiyo, na waheshimiwa wabunge watashirikishwa kikamilifu,” alisema Lowassa.

Waziri Mkuu alizungumzia sekta ya madini na kusema bado inakabiliwa na migogoro kuhusu umiliki wa maeneo ya uchimbaji na uhusiano mbaya kati ya wachimbaji. Alisema migogoro mingi inatokana na matumizi ya teknolojia duni katika mfumo mzima wa utoaji leseni.

“Ili kuondokana na migogoro hiyo, serikali imeanza kuchukua hatua za kuhakikisha kuwa tunajenga mfumo bora wa utoaji na usimamizi wa leseni za madini.

“Kwa upande wa wachimbaji wadogo, serikali imeandaa mkakati mpya na programu ya kuwaendeleza, mkakati huo unaolenga kufanikisha upatikanaji wa maeneo, kuimarisha na kuunganisha nguvu katika utoaji wa mafunzo ya ufundi na ujasiriamali, kuhamasisha na kueneza matumizi ya teknolojia bora na salama,” alisema.

Waziri Mkuu alitaja vipaumbele vya serikali kwa mwaka 2006/2007 kuwa ni kuboresha kilimo, na kwamba nguvu zote zielekezwe kwenye sekta hiyo.

Kuboresha elimu kwa kuhakikisha watoto wenye sifa za kuanza darasa la kwanza wanapata nafasi, kuongeza ujenzi wa shule, kutoa elimu bora na kupata walimu wa kutosha.

Vingine ni wananchi washirikiane na dola katika kulinda usalama wa raia na mali zao, kupambana na ujambazi, uhalifu wa aina zote na kuwafichua wahamiaji haramu; wananchi washirikiane na serikali katika kutunza mazingira; na walio ndani ya serikali waongeze kasi ya utendaji na utoaji uamuzi wa kazi kwa kulenga kuondoa kero za wananchi.

“Naagiza viongozi wa wizara, idara za serikali, mikoa na halmashauri kuhakikisha kwamba watumishi wote wanafanya kazi kwa malengo, tija na ufanisi. Ni vema sasa utumishi wa umma uendeshwe kwa ari mpya, nguvu mpya na kasi mpya,” alisema.

Waziri Mkuu alihitimisha hotuba yake kwa kusema: “Nchi hii ni yetu sote, hatuna mjomba, wadau wetu wa maendeleo wanaunga mkono juhudi zetu tu, lakini hatima ya maendeleo yetu ipo mikononi mwetu.

Tufanye kazi kwa bidii kila mmoja kwa nafasi na kwa eneo alilopo, huo ndiyo msingi utakaotuwezesha kubadili maisha yetu.”

Ofisi ya Waziri Mkuu imeomba Bunge liidhinishe sh 1,148,784,807,000. Mchanganuo wa fedha hizo ni; Ofisi ya Waziri Mkuu sh 85,485,254,400; Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa sh 188,818,726,400; Ofisi ya Bunge sh 34,884,964,000; Ofisi za Wakuu wa Mikoa sh 99,233,985,200; Halmashauri za Wilaya sh 600,492,901,000; na Halmashauri za Miji sh 139,868,976,000.

Wabunge walianza kujadili hoja hiyo jana jioni. Kuhusu kupanda kwa bei ya mafuta ambako kumechangia kupanda kwa mfumuko wa bei nchini, Lowassa aliwataka wafanyabiashara wa mafuta wasitumie bei ya mafuta iliyopo katika soko la dunia “kujipatia utajiri wa haraka haraka.” Katika bajeti ya serikali ya mwaka 2006/2007 iliyosomwa na Waziri wa Fedha, Zakhia Meghji, Juni 15, serikali iliondoa Kodi ya VAT katika mafuta.

Serikali pia itaubadilisha Mfuko wa Akiba ya Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa (LAPF) na kuufanya uwe wa pensheni ili kuboresha masilahi ya wafanyakazi hao.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.