SERIKALI imeagiza kuanza kufanyika kwa uchunguzi wa tuhuma za ubadhirifu wa fedha katika akaunti ya madeni ya biashara ya nje zinazoikabili Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Uamuzi huo wa serikali ulitangazwa bungeni jana na Waziri wa Fedha, Zakia Meghji, wakati akifanya majumuisho ya bajeti aliyoisoma Alhamisi ya wiki iliyopita.
Meghji katika kauli yake hiyo alikiri serikali kupata taarifa za kuwapo kwa vitendo vya rushwa na nyingine za matumizi mabaya ya fedha katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Waziri Meghji alisema, tayari alikuwa ameshamwagiza Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Fedha za Serikali, kuanza uchunguzi kuhusu tuhuma hizo ambazo kwa wiki nzima iliyopita ziliguswa na baadhi ya wabunge wakati wa mjadala wa bajeti.
Meghji alisema, serikali ilikuwa ikitarajia kukamilisha kazi hiyo na taarifa kamili ya uchunguzi huo kutangazwa ifikapo mwishoni mwa mwaka huu.
“Kambi ya Upinzani ilitaka pia maelezo kuhusu tuhuma za ubadhirifu wa fedha katika akaunti ya madeni ya biashara ya nje katika Benki Kuu.
“Ningependa kutoa maelezo kwamba serikali ilimuagiza Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali kusimamia uchunguzi huu. Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali amekwishaalika kampuni za kimataifa za ukaguzi wa hesabu zilete zabuni zao kwa kazi hiyo.
“Zoezi hilo linategemewa kukamilika kabla ya mwisho wa mwaka huu. Nawashauri waheshimiwa wabunge wavute subira, tupate uhakika,” alisema Meghji.
Mbali ya BoT kutuhumiwa kutumia fedha nyingi kuliko inavyostahili katika ujenzi wa majengo yake mapya ya ‘minara miwili pacha’ (Twin Towers), kiasi cha dola za Marekani milioni 30.8, sawa na sh bilioni 40 kinatuhumiwa kufujwa katika akaunti ya madeni ya biashara ya nje.
Taarifa zinaonyesha kuwa, wakopeshaji wa kimataifa kutoka nchi 12 waliingia mkataba wa kusimamia akaunti hiyo na kampuni ya Kitanzania ijulikanayo kwa jina la Kagoda Agriculture Ltd kati ya Septemba na Novermba mwaka jana.
Uchunguzi wa awali wa wakaguzi wa nje wa mahesabu ya akaunti hiyo unaonyesha kuwapo kwa mazingira yenye utata mkubwa unaozingira makubaliano kati ya wakopeshaji na kampuni hiyo iliyolipwa dola milioni 30.8.
Taarifa za awali za uchunguzi huo zinaonyesha kuwa, BoT ilifikia hatua ya kuipa kampuni hiyo fedha zote hizo ikidai kuingia mkataba na wakopeshaji hao katika mazingira ambayo nyaraka zilizopatikana zinaonyesha kuwa na hitilafu nyingi.
Miongoni mwa hitilafu zilizobainishwa katika uchunguzi wa awali ni kukosekana kwa karatasi rasmi zenye majina ya makampuni hayo ya kimataifa.
Akizungumza na waandishi wa habari nje ya viwanja vya Bunge muda mfupi baada ya Meghji kuwasilisha majumuisho na bejti kupitishwa, Mbunge wa Karatu, Wilbroad Slaa, alisema alikuwa akikusudia kuwasilisha majina ya wabunge ambao kwa namna moja walinufaika na kashfa hiyo inayohusu akaunti ya mikopo ya biashara ya nje.
Dk. Slaa ambaye wakati akichangia mjadala wa bejti alizungumzia sana kashfa hiyo alisema muda wa kufanyika kwa uchunguzi alioutoa Meghji ni mrefu, hasa ikizingatiwa kuwa wabadhirifu hao ni watu wanaojulikana.
Alisema yeye anayo majina mawili ya wabunge waliohusika na ubadhirifu huo wa mabillioni kupitia kampuni zao ambazo wanazimiliki.
Alisema wabunge wengi wamekuwa wakitoa hoja ya kutetea ubadhirifu BoT kwa masilahi yao kutokana na wao kuwa na manufaa ndani yake.
Alisema sh bilioni 40 zinazodaiwa kupotea ni fedha nyingi sana ambazo zingeweza kumsaidia mwananchi wa kawaida katika kupunguziwa mzigo wa kodi mbalimbali.
Alisema mwananchi wa kawaida akiiba sh 5,000, atachukuliwa hatua kali ambapo anaweza hata akafungwa, lakini wahusika wameamua kunyamaza kimywa wakati mabilioni ya shilingi yameliwa BoT.
Wiki hii wakati wa mjadala wa bajeti, Mbunge wa Kwela, Dk. Chrisant Mzindakaya (CCM), alitumia muda mwingi bungeni kuitetea BoT hata kufikia hatua ya kupinga hoja za wapinzani na hususan za Mbunge wa Karatu, Dk. Wilbroad Slaa (Chadema), aliyeelekeza mashambulizi yake dhidi ya Gavana wa Benki Kuu, Daudi Balali, wafanyabiashara na maofisa kadhaa serikalini.
Mzindakaya alisema kuna wafanyabiashara ambao wamekuwa wakiwatumia wabunge kuwasemea bungeni masuala yao kwa manufaa yao binafsi.