KAMBI ya Upinzani, imetoa hoja nzito, kiasi cha kumfanya Spika wa Bunge, Samuel Sitta, kumshauri Waziri Mkuu, ajiandae kuwajibu Watanzania wajue ukweli wa mambo. Hoja hizo zimesheheni katika Hotuba ya Msemaji Mkuu wa Kambi hiyo, Dk. Wilbroad Slaa, kuhusu Hotuba ya Bajeti ya Waziri Mkuu kwa mwaka wa fedha wa 2006/2007, aliyoiwasilisha bungeni jana mchana.
Wengi wakiwamo wabunge wa CCM, walionekana kukunwa na aliyozungumza Dk. Slaa, hasa aliposema wapinzani wanahoji hayo kwa masilahi ya nchi na ustawi wa Watanzania wote bila kujali tofauti ya itikadi zao.
Baada ya kumaliza hotuba yake Sitta, alisifu, na kumtaka Waziri Mkuu kuandaa majibu yatakayokata kiu ya Watanzania kuhusu masuala yaliyozungumzwa na mbunge huyo wa Karatu kupitia CHADEMA. Baadhi ya mambo aliyozungumza Dk. Slaa yalihusu ubadhirifu wa mali za umma, kulindwa kwa viongozi wanaokiuka maadili, matumizi makubwa ya uemdeshaji ndege ya Rais, uhamiaji Dodoma na uimarishaji demokrasia nchini.
Kuhusu demokrasia alisema: “Serikali badala ya kufanya hujuma ya kuidumaza demokrasia na kufanya kila mbinu kufuta upinzani katika maeneo hayo, ianzishe rasmi na kwa vigezo wazi mashindano ya maendeleo kati ya wilaya zinazoongozwa na upinzani na zile zinazoongozwa na chama tawala.“Huu ndio utakuwa ukomavu wa demokrasia katika nchi yetu na ishara ya wazi kuwa serikali na chama tawala kweli vimedhamiria kimatendo kuruhusu mfumo wa vyama vingi nchini.
“Hii ni bajeti ya kwanza tangu Uchaguzi Mkuu wa Rais, wabunge na madiwani uliofanyika Desemba 14, 2005. Hata kama wapo waliojaribu kuchezea umoja wetu, ni jambo jema sana kuwa tumebaki kuwa nchi mmoja, na kuendelea kupingana bila kupigana.“Tunamshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa neema ya kipekee aliyotujalia sisi Watanzania. Neema hiyo si nyingine ila kuwa na utamaduni wa uvumilivu na ustahimilivu,” alisema.Dk. Slaa alitaja mambo kadhaa ambayo alisema kwayo, yakitekelezwa, amani itaendelea kudumu.
“Mheshimiwa Rais wa Tatu wa nchi yetu katika hotuba yake bungeni alisema kuwa watendaji wa Kata na wa Vijiji wamekuwa ‘miungu watu’. “Serikali inafahamu fika jinsi wengi walio katika kada hii ni kero kubwa kwa wananchi.
Mfano hai ni Mtendaji wa Kata ya Kansay, Wilaya ya Karatu, anayetuhumiwa kumtorosha mtu aliyebaka. “Wanakijiji wakishirikiana na viongozi wao wanamkamata mbakaji wanampeleka ofisini kwake kama mlinzi wa amani, lakini yeye anamtorosha. Mtu wa namna hiyo bado yuko kazini?! Kuna kulindana sana.
“Ni vichekesho, tunajenga imani gani kwa wananchi! Maneno yetu matamu yanakuwa kitanzi kwa wananchi wanyonge hata kwa uhai na maisha yao,” alisema. Dk. Slaa, kwa niaba ya upinzani, alirejea msimamo wa kambi hiyo kupinga wabunge kuteuliwa kuwa wakuu wa mikoa. “Hatua ya serikali ya hivi sasa ya kuwateua wabunge wa majimbo kuwa wakuu wa mikoa au mkuu wa mkoa kuwa mbunge, inaelekea kupingana na dhana nzima ya Ibara ya 66(3), hasa ikisomwa pamoja na Ibara ya 67(2)(g).
“Pamoja na kauli ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali bungeni ya Juni 22, 2006, Kambi ya Upinzani inaamini kuwa tafsiri ya Ibara hizi zinaenda kinyume na Katiba. Isitoshe, kauli hiyo ya Mwanasheria Mkuu, ikitafsiriwa kwa mujibu wa Ibara ya 61(l) inaleta utata zaidi wa kikatiba, hasa kwa kuwatafsiri wakuu wa mikoa kama viongozi wa kisiasa.“Kambi ya Upinzani inaitaka serikali itoe maelezo ya kina kuhusu tafsiri sahihi ya Ibara hizi. Si vema Serikali inayotakiwa kuilinda Katiba pia iwe mstari wa mbele katika kuivunja,” alisema.
Kuhusu ndege ya serikali ambayo ni mahususi kwa matumizi ya Rais, hasa anapotaka kusafiri nje ya nchi, alisema: “Tunapohoji kuhusu ndege ya Rais, siyo kwa sababu tunataka kujifurahisha, bali tunataka kufahamu, na tunataka Watanzania wafahamu na waelewe ni kwa nini ndege iliyonunuliwa kwa bei kubwa namna hiyo, haitumiki inavyotakiwa na kwa jinsi Bunge hili lilivyoelezwa wakati wa ununuzi wake? “Mheshimiwa Spika tunataka kufahamu, tuna haki ya kufahamu na Watanzania wanataka kujua kama taarifa zilizopo kuwa ndege hiyo inatumia sh milioni 6 kwa kila saa moja inapokuwa angani ni za kweli! Na kama kweli inatua tu viwanja vitano hapa nchini.
“Ni sababu zipi zinamfanya Rais wetu asitumie ndege iliyonunuliwa mahususi na kwa gharama kubwa na badala yake anapanda ndege za abiria kinyume cha makusudio ya kununua ndege inayokwenda kasi sana? Kama ni kweli, inawagharimu Watanzania sh milioni 6 kwa kila saa inayokuwa angani na mabilioni mengine mbali na gharama za ufundi ambao mafundi wake wanaagizwa kutoka Marekani kila wakati, Kambi ya Upinzani inashauri ili kuwapunguzia Watanzania gharama zisizo za lazima zinazoendelea kujilimbikiza na kuwa mzigo kwa Tanzania, ndege hiyo iuzwe mara moja. Bado tunaitaka serikali kutoa ufafanuzi wa kina.
“Tunapohoji hayo tuna nia moja tu, kusimamia matumizi ya fedha za kodi ya wavuja jasho wa nchi hii. Tunapotaka Bunge au Kamati zake zipitie mikataba ni kwa msingi huo huo. Mikataba iwe siri kwa mwenye mali? Hii ni mikataba mibovu. “Tulikoiga pia kuna mgawanyo wa kazi kati ya Serikali na Bunge. Lakini kwao mikataba si siri kwa Bunge, kwani Bunge kwa niaba ya wananchi ndio wenye mali. Mheshimiwa Spika, tutauliza hadi Watanzania wapate majibu ya kuridhisha, chochote kinachoonekana kuwa si matumizi mazuri, liko ndani ya mamlaka ya mbunge mmoja mmoja au wabunge kulihoji, na ni jukumu la serikali kutoa majibu sahihi wakati wote,” alisema.
Alisema Waziri wa Mipango katika hotuba yake ukurasa wa 58 Ibara ya 86 anazungumzia ‘Mpango Maalumu wa kuharakisha Maendeleo Tanzania au Tanzania Mini –Tiger Plan 2020. Mpango huu unasemekana umeanza kutekelezwa 2005 kwa kuzingatia uzoefu na mafanikio ya nchi za Kusini Mashariki mwa Asia. Kuna taarifa kuwa maandalizi ya mpango huo yametugharimu sh bilioni 7, je, kuna ukweli gani?” alihoji. Pia alihoji fedha zilizotengwa na Sweden kupeleka umeme Uyui mwaka 2002.
Kuhusu bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka wa fedha 2006/2007, alisema uchambuzi unaonyesha kuwa matumizi ya kawaida ya Ofisi ya Waziri Mkuu yameongezeka kutoka shbilioni 1.7 hadi sh bilioni 2; ongezeko la asilimia 17. “Fungu 25 ndilo lenye ongezeko kubwa, ambapo bajeti ya kawaida ya Waziri Mkuu imeongezeka kutoka 1,749,077,200 hadi kufikia 4,014, 623,000. Bajeti ya kununua samani na vifaa vya nyumbani (furniture) imeongezeka kutoka sh 95,000,000 hadi 237,000,000. Bajeti ya kununua magari nayo imeongezeka kutoka sh 170, 100, 000 hadi kufikia 600,000,000.
“Kwa kiwango chochote, nchi masikini ambayo inategemea ufadhili kwa bajeti yake kwa asilimia 39, nchi ambayo wengi wa wananchi wake hawana uhakika wa mlo mmoja, nchi ambayo wananchi wamehamasika na kujenga shule nyingi za sekondari, lakini hazina waalimu, madawati, vitabu na vifaa vya maabara au zahanati hazina manesi na waganga, kiwango hiki ni kikubwa mno.“Ofisi ya Waziri Mkuu ndiyo kiranja au msimamizi wa wizara nyingine zote. Itawezekana vipi, kwa wao kusimamia wizara nyingine katika zoezi la kubana matumizi wakati wao wameonyesha njia katika matumizi makubwa?
Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inapenda kujua nini kimetokea katika fenicha zilizonunuliwa mwaka 2004/2005 na 2005/2006. “Kwa taarifa ya Watanzania, Mheshimiwa Spika, mwaka 2004/2005 Ofisi ya Waziri Mkuu ilinunua vifaa na fenicha vya sh 19,999,280 na mwaka 2004/2005 ilitumia sh 95,000,000. Labda ni kweli vimechoka, lakini mbona havikuuzwana kuonekana kama maduhuli ya Serikali?
Ofisi ya Waziri Mkuu ni mfano tu, na katika mahesabu ya haraka haraka tumepata kwa wizara 10 jumla ya sh billioni 5 kwa ajili ya kifungu hiki cha 10300, yaani vifaa vya nyumbani na ‘Fenicha’. “Haya ni matumizi makubwa sana kwa nchi ambayo wananchi wake ni maskini wa kutupwa, si tu kwa umasikini wa mtu mmoja mmoja, lakini pia kwa huduma za jamii kama maji, vifo vya watoto chini ya miaka mitano, idadi kubwa ya watu wasiojua kusoma na kuandika, na mengine mengi kama yalivyoonyeshwa na Taarifa ya Hali ya Umasikini ya mwaka 2005,” alisema.
Kuhusu Dodoma, alisema Kambi ya Upinzani imeshtushwa na kasma mbili na inapenda kupata ufafanuzi wa kina. “Kasma ya kwanza ni Programu ya 10, kasma ndogo ya 1001 na kasma ndogo zaidi ya 10800 ambayo kwa Kiingereza inasomeka tu ‘Rehabilitation, Renovation, and Replacement of Equipment’ lakini maana halisi ya kasma hii iko kwenye Randama ya Wizara ambayo kwa bahati mbaya si wabunge wote wanayo. Kwenye Randama kasma hii iko kwenye kasma ya 310801 sh 3,510,000,000 ambayo inaombwa kwa ajili ya ukarabati majengo ya Ofisi ya Waziri Mkuu Dodoma na Dar es Salaam katika mwaka wa Fedha wa 2006/2007.
“Mheshimiwa Spika, ieleweke kuwa Kambi ya Upinzani haina tatizo la kukarabati Ofisi ya Waziri Mkuu wetu na kuiweka katika hali na hadhi nzuri, lakini tunasikitishwa kuona kuwa tunatenga fedha nyingi kiasi hicho kwa ajili ya ukarabati wa Ofisi ya Waziri Mkuu Dar es Salaam badala ya kuweka nguvu zetu kwenye kukarabati au kujenga Ofisi ya Waziri Mkuu Dodoma ili kuharakisha azima ya serikali ya kuhamia Dodoma. “Kwa nini Ofisi ya Waziri Mkuu ijengwe Dar es Salaam badala ya Dodoma wakati uamuzi wa kuhamia Dodoma umekwisha kufanywa zaidi ya miaka 30 sasa?” alihoji.