RAIS mstaafu wa Zanzibar, Dk. Salmin Amour, amesema hajawahi hata mara moja kuwa na mpango wa kubadilisha katiba ili aweze kutawala kipindi cha tatu.
Dk. Salmin alitoa kauli hiyo jana wakati alipozungumza na wanahabari nyumbani kwake mjini Zanzibar, siku moja tu baada ya kurejea kutoka China alikokuwa akipatiwa matibabu ya macho.
Kiongozi huyo mstaafu aliondoka madarakani mwaka 2000 katika mazingira ambayo yalielezwa kuwa ni ya kushurutishwa na viongozi wenzake wa CCM, ambao walisimama kidete kupinga kile kilichokuwa kikionekana kuwa mpango wake wa kubadili katiba ili aongoze kwa kipindi kingine cha tatu.
“Siwezi kulisemea hilo sana. Mimi sikuwahi hata mara moja kusema ninataka kubadilisha katiba. Nilichokuwa nikitaka kukifanya kilikuwa ni kubadilisha vifungu fulani kwa maslahi ya wananchi wa Zanzibar,” alisema Dk. Salmin ambaye wakati akiwa Rais wa Zanzibar kati ya mwaka 1990 hadi 2000, alikuwa akijulikana kwa jina la Komandoo.
Alitoa kauli hiyo jana baada ya wanahabari kumtaka atoe ufafanuzi wa sababu ambazo zilimfanya hata afikie hatua ya kutaka kubadilisha katiba.
Ingawa Dk. Salmin amekuwa akikataa kuwa na mpango wa kubadili katiba, taarifa za kuwapo kwa mpango wa namna hiyo zilianza kusikika mwaka 1998, ikiwa ni miaka miwili tu kabla hajamaliza muhula wake wa pili wa uongozi.
Wakati fulani, wakati aliyekuwa Rais wa Afrika Kusini, Nelson Mandela alipofanya ziara yake ya kwanza hapa nchini mwaka 1998, Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, alitoa hotuba kali akiwalaani viongozi wa Kiafrika waliokuwa wakitaka kubadili katiba ili waendelee kubaki madarakani.
Siku iliyofuata, takriban magazeti yote yaliielekeza kauli hiyo ya Baba wa Taifa kuwa iliyokuwa ikiwalenga Dk. Salmin na aliyekuwa Rais wa Namibia wakati huo, Sam Nujoma, ambaye naye alikuwa na mpango kama huo.
Dk. Salmin katika mazungumzo yake ya jana, alisema kuwa kilichokuwa kinataka kufanyika wakati huo yalikuwa ni marekebisho ya sheria katika Katiba ya Zanzibar, ambayo yalilenga kuwanufaisha wananchi na si kumuongezea muda yeye.
Jana ilikuwa ni mara ya kwanza kwa Dk. Salmin ambaye hupenda kusema kwa mafumbo, kueleza waziwazi kuwa hakuwahi kuwa na mpango huo.
Akielezea uhusiano wake na wanahabari wakati akiwa madarakani, Dk. Salmin alisema, alivipenda sana vyombo vya habari na anaendelea kuvipenda, kwani alipokuwa rais hakuna hata mwandishi mmoja aliyetiwa ndani, aliyetishiwa zaidi ya yeye kushambuliwa mara kwa mara.
Katika hatua nyingine, alisema kuwa katika utawala wake vyombo vya habari na waandishi kwa ujumla walikuwa na uhuru mpana wa kukosoa na kuandika taarifa yoyote visiwani hapa na alilalamika kuwa wengine walivuka mipaka hata kumuingilia mambo yake binafsi ya ndani ya nyumba, lakini aliwavumilia.
Katika utawala wa Dk. Salmin, magazeti kadhaa yalifungiwa kuingia visiwani hapa kwa madai ya kuandika taarifa zilizoelezwa kuwa za uchochezi.
Kiongozi huyo pia alitetea utawala wake kuwa haukuwahi kukiuka haki za binadamu na misingi ya kidemokrasia, kwani yeye ndiye aliyemtoa kizuizini Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad.
Aidha, kiongozi huyo alifafanua kuwa, hakuhusika kwa namna yoyote na kukamatwa na wanachama wa CUF 18 waliodaiwa kutaka kuiangusha serikali ya awamu ya tano, aliyokuwa akiiongoza, mara baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 1995.
“Sijamtia mtu ndani. Kama kuna watu waliokamatwa waliwekwa ndani kwa mujibu wa sheria za nchi… mimi binafsi sikuwahi kutoa amri ya mtu kukamatwa,” alisisitiza.
Akizungumzia mwelekeo wa sasa wa CCM, alisema ni muhimu kwa wanachama wa chama hicho kutumia fursa ya uchaguzi kwa kuwachagua viongozi wenye uwezo na dhamira ya kukiendeleza na kukitetea chama hicho.
Alipoulizwa na waandishi wa habari kuhusu makundi ya kisiasa ya watu wanaotaka kugombea urais wa Zanzibar mwaka 2010 kupitia CCM, Rais huyo mstaafu alisema: “Mimi nina kambi moja tu ya CCM kuanzia shina hadi taifa… Kambi yangu kubwa ni CCM niliofanyia kazi kwa muda mrefu.”
Katika hatua nyingine, Dk. Salmin alipinga uharakishwaji wa uundwaji wa Shirikisho la Kisiasa la Afrika Mashariki kwa kusema kuwa, ni mapema mno Tanzania kujiunga katika shirikisho hilo ingawa hakueleza kwa undani.
“Tangu jana nimeanza kuona kidogo kidogo nuru imeanza kurudi. Nimeanza kusoma magazeti, navishuruku sana vyombo vya habari vya hapa nyumbani kwa kazi nzuri ya kuwapasha wananchi juu ya afya yangu kwa muda wote nilipokuwa China,” alisema.
Akitoa shukrani zake kwa wananchi, Dk. Salmin alisema anatoa shukurani za pekee na za dhati kwa Rais Jakaya Kikwete, kwa kusimamia kwa moyo mmoja na kufuatilia hali yake ya kiafya nchini China.
“Namshukuru sana, tena sana Rais Kikwete kwa huruma yake binafsi, kwa kushughulikia afya yangu, kwa kufuatilia kwa karibu sana, mbali ya kutuma mjumbe wake kuja kunitazama nilipokuwa China, lakini alikuwa akinipigia simu kila wakati,” alisema.
Pia aliwashukuru viongozi mbalimbali, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, na Katibu Mkuu wa zamani Jumuiya ya Madola, Chifu Ameka Anyaoku, Rais mstaafu, Benjamin Mkapa, ambao walikwenda kumuona alipokuwa kwenye matibabu.