WAZIRI Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, alirejea nchini jana kutoka Marekani alikokuwa kwa mwaka mmoja masomoni, na kusema wazi kuwa hakwenda kusoma ili kujiandaa kuwa rais.
Sumaye aliyasema hayo jana katika Uwanja wa Mwalimu Julius Nyerere, muda mfupi baada ya kuwasili saa 12:30 asubuhi kwa ndege ya Shirika la Ndege la Uingereza (BA).
Sumaye alirejea akiwa ameambatana na mkewe, Esther, ambaye alikwenda Marekani kuhudhuria sherehe za mahafali yake.
Hata hivyo, alisema kuwa kutogombea kwake urais hakutokani na hofu dhidi ya kikundi kilichojijengea nguvu ndani ya CCM kijulikanacho kama ‘mtandao’, bali ni kujali taratibu za chama hicho kikongwe nchini.
Akijibu maswali ya waandishi wa habari waliojitokeza uwanjani hapo, Sumaye alisema kuwa, njaa yake ya kujitafutia elimu, haina uhusiano wa moja kwa moja na yeye kuwania urais kama inavyodhaniwa na watu wengi.
Kwa muda wa mwaka mmoja uliopita, Sumaye alikuwa akisoma katika Chuo Kikuu cha Havard nchini Marekani, akichukua shahada ya uzamili ya uongozi.
“Nchi hivi sasa inaye rais (Jakaya Kikwete) ambaye anatoka chama ambacho mimi ni mwanachama wake, bado ana muda wa miaka takriban tisa ya kuwepo madarakani. Kwa hiyo masuala ya mimi kusoma hivi sasa ni vigumu kuhusishwa na masuala ya kuwania urais,” alisema.
Alisema hisia kuwa yeye ana nia ya kuwania urais zitaendelea kuwa hisia tu na hivi sasa yupo tayari kukitumikia chama chake chini ya Rais Kikwete, ambaye ni mwenyekiti wake wa taifa.
Kwa kuthibitisha kuwa bado ana nia ya kufanya kazi CCM, Sumaye alisisitiza kuwa ndiyo maana ameamua kutetea ujumbe wake katika Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya chama hicho katika uchaguzi utakaofanyika baadaye mwaka huu.
Alisema kuwa kwa hivi sasa mpango wake ni kuwania nafasi hiyo kwa sababu ndiyo nafasi ambayo wanachama wa chama hicho wanaweza kuigombea katika uchaguzi utakaofanyika baadaye mwaka huu.
Akizungumzia nafasi za juu ndani ya chama hicho, Sumaye alisema kuwa hawezi kugombea nafasi hizo kwa sababu chama kinao utaratibu wa kuwapata watu wa kujaza nafasi hizo.
Sumaye amerejea wakati hali ya kisiasa ndani ya chama hicho tawala ikiwa katika fukuto kutokana na vigogo kushindana kuwania nafasi mbalimbali za uongozi.
Msuguano mkubwa upo katika nafasi za wajumbe wa NEC na kila mwanachama anayejiona kuwa ‘ana jina’ ndani ya chama hicho amekuwa akiwania nafasi hizo kwa udi na uvumba.
Aidha, Sumaye amerejea wakati ambapo kuna fununu za kuibuka kwa kundi jingine ndani ya CCM ambalo linapanga mikakati ya kusimamisha mgombea urais mwaka 2010 pale Kikwete atakapokamilisha ngwe yake ya kwanza ya miaka mitano, hivyo kupingana na utaratibu wa miaka mingi wa chama hicho wa kumuachia rais amalize ngwe zote mbili za uongozi.
Wapo baadhi ya watu ambao wanamhusisha Sumaye na nafasi ya Makamu wa Mwenyekiti wa CCM upande wa Tanzania Bara, ambayo kwa sasa inashikiliwa na John Malecela, Mbunge wa Mtera mkoani Dodoma.
Akizungumzia kundi la ‘mtandao’, Sumaye, ambaye ni mmoja wa watu waliowania kuteuliwa na CCM kuwania urais katika uchaguzi mkuu uliopita, alisema kuwa anaamini kuwa makundi yote ya wagombea urais wakati huo yalishavunjwa kwa mujibu wa taratibu za chama hicho.
“Binafsi ninaamini kuwa baada ya Kikwete kuteuliwa na chama kuwa mgombea wake, makundi yote yalivunjwa,” alisema.
Hata hivyo, alibainisha kuwa hata kama kuna kundi ndani ya chama hicho halitaathiri uamuzi wake wa kukitumikia chama.
Waandishi walimuuliza pia kuhusiana na tuhuma mbalimbali ambazo alihusishwa nazo wakati wa kinyang’anyiro cha urais kuelekea uchaguzi mkuu wa 2005, lakini Sumaye alisema kuwa hizo zilikuwa ni kampeni za kisiasa tu.
Hata hivyo, alisema tuhuma iliyotolewa na moja ya magazeti ikimhusisha yeye kuweka mabilioni ya fedha nje ya nchi wakati akiwa waziri mkuu, ndiyo iliyomgusa.
Na ndiyo maana alisema bado ataendelea kuifuatilia kesi aliyoifungua dhidi ya gazeti hilo.