Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Mabadiliko ya Katiba Tanzania hayaepukiki (6)
Mabadiliko ya Katiba Tanzania hayaepukiki (6)
By Habari Tanzania | Published  06/19/2007 | Habari za Kitaifa | Rating:

KATIKA makala yangu ya mwisho ya mfululizo huu kuhusu Katiba, nilimalizia kwa kuahidi kwamba makala ifuatayo ningeandika kuhusu Tume ya Uchaguzi.

Kutokana na tuhuma au kudhihirika hivi karibuni kwamba haki, fadhila na madaraka ya rais yametumiwa vibaya kujinufaisha binafsi, nimeamua kuchambua vipengele vya Katiba vinavyohusu kinga dhidi ya mashitaka, maadili na miiko ya viongozi wakuu wa nchi yetu. Nitashughulikia Tume ya Uchaguzi baadaye.

Kwanza, nishughulikie suala la benki kukopesha ‘bila dhamana’, ambalo linaonekana kuwakera wachambuzi kadhaa. Nielewavyo ni jambo la kawaida kwa benki yoyote ya biashara kufuatilia kwa makini sana tabia na mienendo ya wateja wanavyoendesha akauti zao, hasa pale wanapotaka kukopa kuendeleza biashara zao.

Ni lazima benki iweze kujiridhisha kwamba mteja ataweza kurejesha mkopo pamoja na riba iliyoainishwa katika mkataba wa mkopo.

Benki huwa endelevu kutokana na riba ya mikopo. Kwa hiyo ikijiridhisha kuwa riba italipwa na mkopo kurejeshwa na mteja, basi biashara ni nzuri.

Benki yoyote nchini ambayo ingekuwa na shaka kwamba mkopo kwa rais haungerejeshwa pamoja na riba iliyohusika, ingekuwa ina mushkeri katika menejimenti yake. Kwa hiyo, mimi sina matatizo na hizo benki zilizomkopesha rais.

Kuna utata kwamba rais mstaafu alitumia nyumba aliyonunua akiwa madarakani kwa mkopo kama ndiyo ‘dhamana’ ya mkopo wenyewe.

Kwa mtu wa kawaida hilo linawezekana kabisa, endapo mkopo wenyewe ulikuwa ni sehemu tu ya thamani ya nyumba aliyokuwa anauziwa rais. Huenda mmiliki wa nyumba hiyo alikubaliana na rais kwamba nyumba ithaminiwe na thamani yake ikafikia, kwa mfano, dola 800,000.

Rais akalipa dola 300,000 kutoka katika akiba yake binafsi, na kuomba benki imkopeshe, alibaki ya dola 500,000. Kama baadaye benki imepokea hatimiliki ya nyumba halali kabisa na benki ina dhamana tosha kwa mkopo wa dola 500,000, iliyotolewa na Benki ya Nyumba, ambayo dhamana zake zilikuwa ni nyumba zile zile zilizohusika.

Jambo ambalo linakerea na ambalo linahitaji uchambuzi na tathmini ya kina, ili ikiwa ni lazima, Katiba ibadilishwe au sheria mpya maalumu itungwe kulishughulikia, ni kwa rais aliyeko madarakani pamoja na mkewe kuamua kuanzisha kampuni kama ‘wajasiriamali’ na kuendelea kufanya biashara papo hapo.

Itakumbukwa kwamba kutokana na utekelezaji wa Azimio la Arusha, sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma ilikuwa inatamka bayana kwamba kiongozi wa umma yeyote hatakuwa na hisa katika kampuni.

Katika Toleo la Katiba la 1995, inatamka katika Ibara ya 46A(2) kwamba rais hatashitakiwa ili kuondolewa madarakani, “isipokuwa tu kama inadaiwa kwamba rais, ametenda vitendo ambavyo……. vinaivunja Katiba au Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma, ametenda vitendo …… vinavyokiuka uandikishaji wa vyama vya siasa, au amekuwa na mwenendo unaodhalilisha kiti cha Rais……”.

Toleo la Katiba la 2000 linaloorodhesha hadi wakati huo linaendelea na vipengele nilivyonukuu hapo juu. Kwa hiyo wakati Rais Mkapa akianzisha kampuni mwaka 1999, alitakiwa azingatie matakwa ya Katiba na Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma.

Najua kwamba Ibara ya 24 (1) ya Katiba inatamka kwamba: “……….. kila mtu anayo haki ya kumiliki mali, na haki ya hifadhi ya mali yake aliyonayo, haki ya sheria.”

Kwa hiyo huenda kwamba baada ya Azimio la Zanzibar lililofuta kipengele kilichokuwa kinapinga marufuku viongozi wa umma kumiliki hisa za kampuni, rais kama raia aliona ni halali kwake kuanzisha na kumiliki Kampuni ya ANNBEM Ltd.

Nahisi ni kutokana na kwamba Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma baada ya Azimio la Zanzibar iko kimya kuhusu viongozi kutomiliki hisa, ndiyo sababu hata Rais Mkapa amepata kutamka kwamba wale wanasiasa waliokuwa wanapinga waziri mkuu wa wakati huo kumiliki mashamba ya Kibaigwa, au baadaye ya Dakawa, kwamba walikuwa “wana wivu wa kike” na wakati mwingine “ni wavivu wa kufikiri”.

Aliweza kutamba hivyo kutokana na kwamba walikuwa hawajatambua ukweli wa mabadiliko yaliyoletwa kimya kimya na Azimio la Zanzibar. Yeye mwenyewe alikuwa ameshajiingiza kikamilifu katika ujasiriamali, kwa hiyo hangeweza kumpinga waziri mkuu wake kwa ‘kufuata nyayo.’

Kwa hiyo, la msingi la kufanya sasa ni kutafakari kama rais anapokuwa madarakani ajiingize upya katika biashara au hata aendelee na biashara aliyokuwa anafanya hapo awali.

Mimi naamini kwamba kazi ya kuwa rais ni kazi nzito kuliko zote katika nchi. Ni lazima rais awekewe mazingira yanayomwezesha kufanikisha majukumu yake, la sivyo masilahi ya umma yataathirika vibaya.

Ndiyo sababu, hata hapa Tanzania, Katiba na sheria zimeweka utaratibu wa kumpatia wasaidizi waliothibitika ni waadilifu, wazalendo, wenye utaalamu uliotukuka, walio jasiri, wenye kupenda na kuzingatia haki na wapenda watu.

Ndiyo sababu hata Bunge linaloidhinisha sheria zilizopendekezwa na serikali ikiwa chini ya rais, linakuwa na wapinzani na utaratibu wa uchambuzi wa kina wa kila pendekezo ili rais apatiwe tu ile sheria ambayo italeta manufaa ya hakika.

Baada ya kuhakikisha haya yote, itakuwa tunapingana endapo tutaruhusu kuwa na mfumo utakaomfanya rais asumbuliwe na masuala binafsi ya kibiashara wakati akiongoza nchi. Kwa hiyo napendekeza kwa dhati kabisa Katiba na Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma vitamke bayana miiko hii.

Ni jambo la kawaida katika nchi nyingi kuwataka viongozi wakuu wake kuachana na uendeshaji na menejimenti ya biashara zao wakati wanapokuwa madarakani.

Yumkini hata viongozi wenyewe wakisha kupata madaraka ya juu serikalini, hujivua majukuu ya uendeshaji wa kampuni zao ili waweze kutekeleza mambo mazito ya kitaifa yanayowakabili.

Sheria yetu iliyokuwa inasimamia Zabuni za Serikali (Central Tender Board), ambayo sasa imebadilishwa kuwa Public Procurement Act, ilikuwa inatamka bayana kwamba ofisa yeyote anayehusika na uchambuzi wa zabuni, ni lazima ajitoe kama ana uhusiano kibiashara au kifamilia na mzabuni yeyote.

Sasa kama rais atakuwa mfanya biashara na huku ndiye ‘msimamizi’ wa zabuni zote za serikali, kwa maana kuwa anaweza kufuata au kuagiza mabadiliko katika maamuzi ya serikali, atawezaje kusimamia shughuli ya umma?

Ni kutokana na dhana kwamba rais ni lazima asijihusishe na juhudi za kuongeza kipato wakati akiwa madarakani, nchi nyingi zinahakikisha rais anapata masilahi na marupurupu ya juu.

Kwa hiyo napendekeza kwa dhati kabisa kwamba ama Katiba yetu itamke rasmi kwamba rais hatajihusisha kwa namna yoyote ile na biashara akiwa madarakani au Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma itamke hivyo.

Niongezee kwamba kama tutaendelea kuruhusu rais afanye biashara wakati akiwa madarakani kama inavyoonekana, tutaingiza vishawishi kwake kutumia fursa na madaraka aliyonayo kujilimbikizia mali binafsi visivyo.

Huenda hata akashawishika kupokea hongo ambayo itamvusha katika mpango wake wa kibiashara, licha ya kwamba kwa kawaida hana muda wa kutekeleza majukumu yake mazito pamoja na biashara.

Hata hivyo, hapa ningeweza kuongeza kwamba, rais ambaye anachaguliwa akiwa mfanyabiashara/mkulima, anaweza kuendelea na biashara/ukulima wake kama sehemu ya makazi, bora tu akabidhi uendeshaji kwa wakala atakayeendesha shughuli anapokuwa madarakani.

Kuhusu viongozi wakuu wengine, naona ni muhimu sana wakati wanapokabidhiwa madarakani waorodheshe kinaganaga shughuli zao za kibiashara, na rais kama mwajiri wao, aweze kuamuru kama mteule wake aendelee kusimamia hizo shughuli au la.

Edwin Mtei amewahi kuwa Waziri wa Fedha, Gavana wa Benki Kuu (BoT ), na mwasisi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) . Anapatikana kwa simu: 0754 387 177.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.