SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), imesema baadhi ya mahakimu wamekuwa wakila fedha za dhamana zilizowekwa na washitakiwa, wakishirikiana na makarani wa mahakama.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Nchi Afisi ya Rais Katiba na Utawala Bora, Ramadhan Abdallah Shaaban, alipofungua mkutano wa kutathmini ripoti ya miaka mitano tangu kuanzishwa Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka Zanzibar.
Alisema usimamizi wa mashitaka unahitaji uadilifu, lakini baadhi ya mahakimu na makarani Zanzibar wameanza kukosa uadilifu huo na kuathiri ngazi zote za utendaji katika vyombo vya kusimamia sheria.
“Baadhi ya makarani wa mahakama, wanadai fedha kwa jina ama la hakimu au jaji na ipo mifano hata nyaraka zilizopo chini ya dhamana ya mahakama kuibiwa na kuuziwa washitakiwa, ili wazitumie tena kupata dhamana,” alisema Waziri Shaaban.
Alieleza kwamba, baadhi ya mawakili Zanzibar wamekuwa wakifanya kazi kinyume na maadili yao, ikiwemo kushirikiana na washitakiwa kuchelewesha kesi kwa makusudi, ili kesi hizo zife.
Alieleza kwamba, rushwa inaendelea kuathiri vyombo vya kusimamia sheria na kuwataka wananchi kushirikiana na vyombo vya dola na vya habari kufichua wanaoendeleza rushwa, hasa watendaji katika dhamana za serikali.
Alisema zipo kesi zimekufa kutokana na wananchi kutojitokeza kwenda kutoa ushahidi mahakamani, vitendo ambavyo havisaidii kujenga misingi ya utawala bora.
Waziri huyo, alisema kwamba hivi sasa kuna malalamiko kutoka kwa wananchi kuwa, baadhi ya mahakimu Zanzibar wamekuwa wakitoa hukumu zinazokwenda kinyume cha sheria, hasa katika kesi za uharibifu wa mazingira, ikiwemo uvuvi haramu, uchimbaji mchanga na bidhaa za magendo.
Alisema baadhi ya washitakiwa wamekuwa wakitakiwa kutoa fedha taslimu za dhamana, lakini baada ya kesi zao kumalizika, hazirejeshwi na badala yake kuchukuliwa na makarani na mahakimu.
“Kuna malalamiko washitakiwa kutakiwa kutoa dhamana ya fedha taslimu, lakini baada ya kesi kumalizika, hawarejeshewi fedha hizo na hubaki kuwa mali ya makarani na mahakimu,” alisema.
Waziri Shaaban alisema analazimika kuyazungumzia hayo kwa vile yeye ndiye mwenye dhamana ya kusimamia vyombo vya sheria, ingawa vipo huru kufanya kazi kwa kujitegemea.
Awali, Mkurugenzi wa Upelelezi na Makosa ya Jinai Zanzibar, Ramadhan Kinyogo, alisema polisi linatarajia kuzirejesha kesi za ubadhirifu wa mali za serikali zilizokuwa zikiwakabili watendaji wakuu wa serikali, ambazo zimefutwa na mahakama, baada ya upande wa mashitaka kushindwa kuwasilisha ushahidi katika muda muafaka.
Alisema kwamba polisi hivi sasa inaendelea na upelelezi wa kesi hizo na baada ya kukamilika, itazirejesha mahakamani kwa vile sheria inawaruhusu kufanya hivyo.
Hivi karibuni, kesi tatu za ubadhirifu wa mali za serikali zilifutwa kisiwani Pemba na Unguja, ikiwemo kesi mbili za ulipaji mishahara wafanyakazi hewa katika Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali.
Kushitakiwa kwa watendaji hao kulitokana na ripoti ya kamati ya kuchunguza wizi huo iliyoongozwa na Katibu wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar, Ramadhan Muombwa Mwinyi, ambayo ilibaini SMZ ilikuwa ikipoteza sh bilioni moja kila mwaka kulipwa wafanyakazi hewa.
Kinyogo alisema kwamba, polisi inashindwa kukamilisha upelelezi kwa muda muafaka kutokana na kukabiliwa na matatizo mbalimbali, ikiwemo vitendea kazi na uhaba wa wataalamu katika kuchunguza kesi za kughushi.
Alisema kwa mujibu wa marekebisho ya sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai Zanzibar, kesi kama hizo hutakiwa ushahidi wake kukamilika katika kipindi cha miezi minne na zile za mauaji miezi tisa, na zaidi ya hapo mahakama inaweza kuzifuta.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi wa Mashitaka Zanzibar, Othman Masoud, alisema upelelezi wa makosa ya jinai bado una udhaifu mkubwa na unachangia kesi nyingi kufutwa.
Alisema udhaifu huo unatokana na sababu mbalimbali, ikiwemo uchache wa watendaji na ukosefu wa vitendea kazi hasa kwa Jeshi la Polisi.
Alieleza sababu nyingine ni ukosefu wa wataalamu wa kutosha katika masuala ya upelelezi, kukosekana maabara ya kisasa inayohusu uhalifu, polisi kubebeshwa majukumu mengi pamoja na mfumo dhaifu wa ulinzi wa ndani.