KAULI zilizotolewa na Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wakati wa ziara yake kisiwani Pemba, hivi karibuni, zinaelekea kuhatarisha mazungumzo baina ya chama hicho na Chama cha Wananchi (CUF).
Tangu Makamba atoe matamshi hayo, makundi kadhaa ya wana CUF, wakiwemo wanachama wa kawaida, vijana na wabunge, wameongeza shinikizo kwa uongozi wa chama hicho kujitoa katika mazungumzo hayo iwapo CCM haitatoa kauli kupinga matamshi ya Makamba.
Hali hiyo ilisababisha chama hicho kuitisha vikao vyake vya ngazi mbalimbali, kujadili hali ya mambo kabla ya kutoa kauli kuhusu suala hilo.
Katika muendelezo wa shinikizo hilo, jana, kundi la wanachama wa CUF wapatao 400 kutoka wilaya za Temeke na Kinondoni, jijini Dar es Salaam, walivamia ofisi za makao makuu ya chama hicho, Buguruni, wakishinikiza viongozi watangaze kujiondoa kwenye mazungumzo hayo ambayo yamefanywa kuwa siri kubwa.
Ili kuhakikisha kuwa ujumbe wao unawafikia viongozi na wanachama wengine, makundi hayo yalikuwa yamebeba mabango yenye ujumbe unaoutaka uongozi kujitoa katika mazungumzo haraka.
Walipowasili katika ofisi hizo na kuomba kuonana na viongozi wa juu wa chama, walizuiwa mlangoni na walinzi na kutakiwa kuondoka kwa sababu viongozi hao walikuwa katika kikao.
Hata hivyo, wanachama hao waliendelea kushinikiza waruhusiwe kuwaona viongozi wao, huku wakitoa maneno makali kwa walinzi, ambao waliamua kuwaruhusu.
Walipoingia katika uwanja wa ofisi hizo, walikutana ana kwa ana na Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba, pamoja na Katibu Mkuu, Maalim Seif Shariff Hamad, na kuwazuia kuingia katika chumba cha mikutano.
Huku wakianikiza mabango waliyokuja nayo, wanachama hao waliwashinikiza viongozi hao wawaeleze kinagaubaga, kile kilichozungumzwa katika mazungumzo na CCM hadi kufikia sasa.
Wanachama hao, waliwataka viongozi hao wajiondoe kwenye mazungumzo hayo na kurudi kuendelea na kazi ya kukijenga chama hicho, kwani imejidhihirisha kuwa CCM haina nia ya kutekeleza yatakayoafikiwa.
“Mheshimiwa, kuna haja ya kukaa meza moja na hawa? Tutawaambiaje Watanzania?” alihoji Mwenyekiti wa CUF wa Serikali ya Mtaa wa Mbagala, Salum Abdallah.
Jitihada za Profesa Lipumba na Maalim Seif kuwatuliza wanachama hao, hazikufanikiwa hadi mwenyekiti huyo alipowaelezea aliyoyazungumza Rais Jakaya Kikwete katika hotuba yake ya uzinduzi wa Bunge ya Desemba 30, 2005 na kuelezea nia yake ya kumaliza matatizo ya kisiasa Zanzibar.
“Rais Kikwete amekuwa akiyarudiarudia maneno haya, na hiyo inatufanya tuamini kuwa ana nia ya dhati ya kile anachokizungumza,” alisema Profesa Lipumba.
Baada ya kusomewa sehemu ya hotuba hiyo, wanachama hao walionekana kutulia kidogo na kuanza kuwasikiliza viongozi wao.
Walichukuliwa hadi kwenye chumba cha mikutano na kuelezwa kuwa, viongozi wa chama hicho walikuwa katika mlolongo wa vikao, kwa muda wa wiki moja sasa, na ajenda kubwa katika vikao hivyo, ni mustakabali wa mazungumzo hayo.
Profesa Lipumba aliwafahamisha wanachama hao kuwa kwa siku ya jana, Baraza Kuu la Uongozi la CUF, lilipanga kukutana jana, katika mlolongo wa vikao vya kujadili suala hilo.
Profesa Lipumba aliwaeleza kuwa, kikao hicho ndicho kitakachokuja na uamuzi kuhusu mazungumzo hayo.
Baada ya kusikia hivyo, wanachama hao walikubali kuondoka, lakini licha ya kuambiwa wakasubirie matokeo ya kikao hicho majumbani kwao, baadhi yao waliamua kukaa nje ya ofisi hizo wakisema hawataondoka mpaka wajue hatma ya kikao hicho.
Hata hivyo, majira ya saa 7.30 mchana, Profesa Lipumba, akiwa ameambatana na ujumbe wa watu watatu, akiwemo kiongozi mwingine maarufu wa chama hicho, Juma Duni Haji, waliondoka na ilielezwa kuwa walikuwa wamekwenda kuonana na baadhi ya mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao Tanzania.
Ujumbe huo ulirejea majira ya saa 11 jioni na kuendelea na kikao hicho cha baraza la uongozi.
Hata hivyo, baadaye mchana, Mbaralah Maharagande, Kaimu Mkurugenzi wa Haki za Binadamu na Mahusiano ya Umma wa chama hicho, alitoa taarifa akisema kuwa tamko la Baraza Kuu la Uongozi Taifa kuhusu hatma ya mazungumzo ya CUF na CCM itatolewa leo saa 4 asubuhi ofisini hapo.
“Tamko hilo litatolewa na Mwenyekiti wa Chama Taifa Prof. Ibrahim Haruna Lipumba,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.
Wanachama hao wanataka chama kijitoe katika mazungumzo kwa sababu matamshi ya Makamba huko Pemba yanaonyesha kuwa chama chao kinachezwa shere.
Msimamo mkali hadi hivi sasa umeonyeshwa na kundi la vijana, ambalo lilifikia hatua ya kuwasilisha ushahidi wa picha za video, zikionyesha baadh ya kauli za Makamba katika mikutano yake Pemba.