SERIKALI imekiri kushuka kwa kasi ya uchumi na kubainisha kuwa, kushuka huko kulisababishwa na hali ya ukame iliyojitokeza kwenye maeneo mengi katika msimu wa mvua wa mwaka 2005/2006.
Akiwasilisha taarifa ya hali ya uchumi wa taifa kwa mwaka 2006 na mwelekeo wa mpango wa maendeleo mwaka 2007/2008 bungeni jana, Waziri wa Mipango, Uchumi na Uwezeshaji, Dk. Juma Ngasongwa, alisema katika mwaka 2006 uchumi ulikuwa kwa asilimia 5.9 ukilinganisha na ukuaji wa asilimia 6.7 mwaka 2005.
Aliainisha matatizo kadhaa yaliyochangia hali hiyo kuwa ni pamoja na ukosefu wa umeme yaliyosababishwa na ukame na kufanya kuwepo kwa mfumuko wa bei kwani bidhaa nyingi huzalishwa kwa kutegemea umeme.
Alisema tatizo jingine ni kupanda kwa bei ya mafuta katika soko la dunia na kusababisha gharama za maisha kupanda.
Ngasongwa alisema, sekta zilizoathirika zaidi na hali hiyo ni pamoja na kilimo, bidhaa za viwandani, umeme na maji, ambavyo ni muhimu kwa matumizi ya kila siku.
Alisema viwango vya ukuaji viliongezeka kwa sekta za uuzaji wa jumla, rejareja, mahoteli, utalii, uchukuzi na mawasiliano, madini, bima pamoja na huduma za kibiashara.
Alisema katika kiwango cha ukuaji kwa sekta ya uendeshaji wa serikali na huduma nyingine, haikubadilika na kwa kiasi kikubwa imebaki kama kiwango cha mwaka 2005.
Alisema pamoja na kupungua kwa kiwango cha ukuaji, sekta ya kilimo iliendelea kutoa mchango mkubwa katika pato la taifa ikilinganishwa na sekta nyingine, ambapo mwaka 2006 mchango wa sekta hiyo ulikuwa asilimia 44.7.
Kuhusu mfumuko wa bei, Waziri Ngasongwa alisema katika mwaka 2006 ulikuwa asilimia 7.3 ikilinganishwa na asilimia 5.0 mwaka 2005.
Alisema kuongezeka kwa mfumuko wa bei mwaka jana kulitokana na kupanda kwa bei za bidhaa, hususani chakula na mafuta ya petroli ambayo pia yalichangia kuongezeka kwa gharama za usafirishaji na uzalishaji umeme uliokuwa unatumia mafuta.
“Hadi Aprili 2007 kasi ya upandaji wa mfumuko wa bei ulikuwa asilimia 6.1 baada ya kushuka kutoka asilimia 7.2 katika mwezi Machi, kiwango hicho kinatarajia kushuka kutokana na ongezeko la upatikanaji wa chakula baada ya kipindi cha mavuno kuanza sehemu mbalimbali za nchi,” alisema Waziri Ngasongwa.
Alibainisha kuwa, katika nusu ya kwanza ya mwaka 2006/2007 mapato ya ndani yalifikia sh bilioni 1,311.7 sawa na asilimia 8.0 juu ya makisio yaliyotarajiwa ambapo fedha hizo zilitokana na kodi na mapato ya kawaida.
Alisema kuongezeka kwa mapato kulitokana na kuimarika kwa ukusanyaji kodi hususan kodi ya mapato, Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwa bidhaa za ndani na nje ya nchi na ushuru wa forodha.
Kwa upande wa matumizi katika nusu ya kwanza ya mwaka wa fedha 2006/2007, Dk. Ngasongwa alisema yalifikia sh bilioni 2,104.5 sawa na asilimia 81.0 ya matumizi yaliyopangwa kwa kipindi hicho.
Alibainisha kuwa, deni la taifa lilipungua kutoka dola za Marekani milioni 9,383.9 Desemba 2005 hadi dola za Marekani milioni 7,188.4 Desemba 2006 sawa na punguzo la asilimia 23.3.
Kati ya deni hilo, dola za Marekani milioni 5,749.0 ni deni la nje sawa na asilimia 80.0 ya deni lote na dola za Marekani milioni 1,439.4 ni deni la ndani.
Alisema kupungua kwa deni la taifa kulitokana na msamaha wa madeni uliotolewa na mashirika ya fedha ya kimataifa, nchi wananchama wa Paris Club pamoja na juhudi za serikali katika kulipa madeni ya ndani.