Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Uwezo wakwamisha MKUKUTA
Uwezo wakwamisha MKUKUTA
By Habari Tanzania | Published  06/15/2007 | Habari za Kitaifa | Unrated
na Mwandishi Wetu


SERIKALI imekiri jana bungeni kuwa, haina uwezo wa kukidhi mahitaji ya rasilimali zinazohitajika kwa ajili ya utekelezaji wa Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini (MKUKUTA).

Akiwasilisha bajeti ya 2007/08 bungeni jana, Waziri wa Fedha, Zakia Meghji, alisema kuwa, ingawa kimsingi bajeti hiyo inazingatia umuhimu wa kuongeza rasilimali kwa ajili ya kukuza uchumi, kama msingi wa mkakati endelevu wa kupiga vita umaskini, uwezo wa kupata rasilimali ni mdogo.

Alisema kuwa zoezi la kukokotoa mahitaji ya rasilimali (fedha na watu) zinazohitajika kutekeleza MKUKUTA, bado linaendelea. 

 “Hata hivyo, viko viashiria muhimu vinavyoonyesha kwamba fedha na rasilimali nyingine zinazohitajika ili kutekeleza MKUKUTA ni nyingi, na kwa vyovyote vile, serikali haiwezi kupata uwezo wa kutosha kukidhi mahitaji hayo kwa njia ya mapato ya ndani pekee. 

“Kwa hali hii, utekelezaji wa MKUKUTA unahitaji ushirikiano wa karibu kati ya sekta ya umma, sekta binafsi, jumuiya za wananchi, nchi wahisani, na mashirika ya maendeleo ya kimataifa,” alisema Meghji.

Hata hivyo, aliliambia Bunge kuwa, katika mwaka wa fedha wa 2007/08, maeneo yote matatu ya MKUKUTA yamezingatiwa kulingana na uwezo wa bajeti. 

Aliyataja maeneo hayo kuwa ni kukuza uchumi na kuondoa umaskini wa kipato, kuboresha hali za maisha ya watu na huduma ya jamii pamoja na kuimarisha utawala bora na uwajibikaji. 

Alisema kuwa, viashiria vinavyoonyesha gharama za kutekeleza MKUKUTA ni pamoja na mpango wa uwekezaji wa sekta ya usafirishaji, inayojumuisha barabara, reli, bandari, viwanja vya ndege, n.k. ambao unaonyesha mahitaji ya zaidi ya dola za Kimarekani bilioni 5 sawa na sh trilioni 6.4 katika kipindi cha miaka 10 – au sh bilioni 640 kwa mwaka.

Aidha, mpango wa ukarabati wa njia za kusambaza umeme na kuimarisha hali ya fedha ya Tanesco, unahitaji dola za Kimarekani bilioni 1.3 au sh trilioni 1.6, katika kipindi cha miaka mitano au sh bilioni 320.0 kwa mwaka.

Mpango wa afya ya msingi kwa ajili ya kufikia malengo ya milenia, unahitaji dola za Kimarekani bilioni 15, au sh trilioni 19.5 katika muda wa miaka mitano au sh trilioni 3.9 kwa mwaka.

Alisema pia kuwa, mpango wa kuimarisha huduma za ugani, unahitaji sh bilioni 193 kwa miaka mitatu, au sh bilioni 64 kwa mwaka.

“Mahitaji yaliyowasilishwa na wizara, idara zinazojitegemea, mikoa, na halmashauri kwa ajili ya bajeti ya 2007/08, ni zaidi ya sh trilioni 12. Hiki pia ni kigezo cha kukadiria mahitaji ya fedha kwa ajili ya kutekeleza MKUKUTA. 

 “Kiasi hiki ni mara mbili ya uwezo ulioko wa mapato ya ndani na misaada ya nje kwa pamoja. Kwa hali hii, hatuwezi kukwepa kupanga vipaumbele kwa makini sana, na hatuwezi kujidanganya kwamba mapato ya ndani pekee yanaweza kutosha kutekeleza MKUKUTA, bila misaada ya nje, na bila ushiriki wa dhati wa sekta binafsi,” alibainisha Meghji na kuongeza:

“Ni vizuri ieleweke pia kwamba, mashirika ya maendeleo kama Benki ya Dunia na Benki ya Maendeleo ya Afrika, yalianzishwa kwa madhumuni ya kutoa mikopo kwa ajili ya miradi ya maendeleo. Hivyo, kukopa kutoka kwenye mashirika haya si utegemezi.  Hakuna nchi au kampuni kokote duniani iliyoendelea kihalali bila kukopa.” 

Akitoa mfano wa hilo, Meghji alisema kuwa, sehemu kubwa ya fedha za nje katika bajeti aliyokuwa anaiwasilisha, ni mikopo ya masharti nafuu kutoka Benki ya Dunia na Benki ya Maendeleo ya Afrika. 

Aliwaambia wabunge kuwa, kupata misaada kutoka nchi marafiki, pia si jambo baya, ilimradi misaada hiyo ielekezwe kwenye maeneo yatakayoongeza uwezo wa nchi kujitegemea.

Hata hivyo, Meghji alisisitiza kuwa, bajeti ya mwaka 2007/08 itaendeleza juhudi za serikali za kuwaongezea uwezo wananchi wa kujiletea maendeleo yao wenyewe. 

Ili kufanikisha azma hii, Meghji aliainisha baadhi ya mambo ambayo yamezingatiwa. Alisema kwanza, msisitizo utawekwa katika kuharakisha utekelezaji wa awamu ya pili ya mageuzi ya sekta ya fedha ambayo itawezesha wananchi wengi zaidi kupata mikopo ya uzalishaji, biashara, na pia mikopo ya nyumba, mikopo ya mali za kukodi na kuboresha mifuko ya pensheni na hifadhi ya jamii.

Aidha, serikali itaendelea kuweka mazingira mazuri ya kujenga tabia ya kujiwekea akiba miongoni mwa wananchi kwa kuwahamasisha na kuwasaidia kuunda SACCOS za makundi mbalimbali ya wajasiriamali, ambazo zitawezesha mtu mmoja mmoja au makundi ya watu kupata mikopo kutoka katika mabenki mikoani kote nchini.

Hatua ya tatu inayochukuliwa na serikali ni kuendelea kuimarisha mifuko ya dhamana za mikopo, inayosimamiwa na Benki Kuu, ili itoe dhamana kwa wajasiriamali wengi zaidi.

Aliianisha hatua nyingine kuwa ni Benki ya Rasilimali (TIB) kuimarishwa kwa kuongezewa mtaji ili iweze kutekeleza majukumu yake ya sasa kama benki ya maendeleo, hatua kwa hatua.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.