Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Kikwete akabidhiwa jahazi kuongoza CCM na kutaka:
Kikwete akabidhiwa jahazi kuongoza CCM na kutaka:
By Habari Tanzania | Published  06/26/2006 | Habari za Kitaifa | Unrated
Kikwete akabidhiwa jahazi kuongoza CCM na kutaka:
 
Viongozi wabadilike kukipa Chama uhai
Asema Chama imara ni chenye viungo vinavyofanya kazi
Ataka watendaji kuwa mfano kwa vitendo, si maneno
Chama kijenge uwezo wa kifedha, rasilimali vinginevyo…
 
Na Noor Shija, Dodoma
 
MWENYEKITI mpya wa Chama Cha Mapinduzi Taifa, Rais Jakaya Kikwete amewataka viongozi, watendaji na Jumuia za Chama kubadilika ili kuleta uhai kwenye Chama.
 
Kikwete amesema Chama imara ni kile ambacho viungo vyake vimekamilika na vinafanya kazi vizuri.
 
Rais Kikwete alisema hayo mara baada ya mwenyekiti mstaafu na ambaye pia ni Rais mstaafu wa awamu ya tatu Benjamin Mkapa kutangaza kuwa Rais Kikwete ndiye mshindi wa kishindo wa nafasi ya mweyekiti wa CCM.
 
Mkapa alisema kuwa Rais Kikwete alishinda kwa kupata kura 1,812 kati ya kura halali 1,813 zilizopigwa na kwamba kura moja ndiyo ilisema hapana na hakuna kura iliyoharibika.
 
Rais Kikwete na mwenyekiti wa CCM alisema kuwa Chama imara ni kile chenye wanachama wengi, viongozi tena wanaofanya vikao watendaji imara, rasilimali na jumuia imara za Chama.
 
Alisema ili kuhakikisha Chama ni imara lazima kuhakikisha kiungo cha viongozi kiko imara, safu za viongozi ziwe zimekamilika ipasavyo na wako mstari wa mbele kutimiza wajibu wao wa uongozi.
 
Rais Kikwete alisema kuwa kiongozi ndiye mwonyeshaji njia, lazima viongozi wa Chama Cha Mapinduzi waifanye kazi yao kwa umahiri mkubwa na kwamba viongozi lazima waongoze kwa mifano na siyo kwa maneno.
 
“Kauli za fuata maneno yangu usijali matendo hazina nafasi katika uongozi wa Chama chetu. Tuseme tunayotenda ili tujenge moyo kwa watu kutuamini,” alifafanua Rais Kikwete ambaye pia ni mwenyekiti wa Chama.
 
Alisema kuwa ni ukweli usiofichika kwamba viongozi wa Chama Cha Mapinduzi hawafanyi vya kutosha kazi ya uongozi miongoni mwa umma.
 
“Wakati mwingine ukitulinganisha na viongozi wa vyama vya upinzani, viongozi wa Chama Cha Mapinduzi hatufanyi sana mikutano ya hadhara na umma. Mikutano ya hadhara ni nyenzo ya kuwavutia watu upande wetu,” alisema Mwenyekiti Kikwete.
 
Alisema kuwa mikutano ya hadhara ni nyenzo ya kuwavutia watu upande wa Chama Chama Mapinduzi. “Naomba wenzangu tubadilike ili tuzuie upotoshaji na kuhakikisha kuwa wananchi wanapata ukweli wa mambo kutoka midomoni mwetu,” alisema.
 
Kikwete alisema kuwa ufanyikaji wa vikao ndani ya Chama siyo nzuri na aliwataka viongozi kubadilika kwa kuwa udhaifu huo ni jambo lisilofurahisha hata kidogo.
 
Alisema ndani ya Chama maamuzi hufanywa kupitia vikao tofauti na serikali ambapo Rais, Waziri, Mkuu wa Mkoa na Mkuu wa Wilaya wanaweza kuamua wenyewe bila vikao.
 
Mwenyekiti Kikwete alisema kutofanyika vikao vya Chama vya ngazi husika kunadhoofisha sana mfumo mzima wa maamuzi ndani ya Chama, pia kunaua dhana nzima ya demokrasia ndani ya Chama na dhana ya uongozi wa pamoja.
 
Aliwataka wanachama na wajumbe wa vikao husika wawe wakali kudai kufanyika kwa vikao vya ngazi zao. “Naomba tubadilike ili kiungo hiki muhimu sana tukipe nafasi stahiki ya uhai wake,” alisisitiza.
 
Alisema watendaji ni kiungo cha msingi katika uhai na maendeleo ya Chama, hivyo ni vema watendaji wa Chama wawe ni watu wenye ujuzi, maarifa na uwezo wa hali ya juu wa kazi zao za kiutendaji.
 
Mwenyekiti huyo mpya wa CCM alisema ni wajibu wa Chama kuwawezesha watendaji kutimiza ipasavyo majukumu yao kwa maana ya mafunzo, zana na vifaa vya kazi. Alisema pamoja na hayo ni wajibu wao kuwatengenezea mazingira mazuri ya kufanyia kazi maofisini na katika hali ya maisha yao.
 
Kikwete alisema pia ni muhimu kukaa chini na kuzungumzia uwezo wa kifedha na rasilimali za Chama. “Hili ni jambo la msingi sana,” alisisitiza.
 
Alisema japo hakuna jawabu rahisi kuhusu nini na vipi kifanyike, lakini lazima kufanya kwani hakuna badala yake, na ifanyike hivyo katika kila ngazi ya Chama.
 
“Nawaomba wenzangu kila kiongozi na kila mwanachama katika ngazi yake alipe suala hilo uzito unaostahili. Tuchune bongo zetu, tubuni mikakati, mbinu na mipango ambayo itakiingizia Chama chetu fedha na kukipa rasilimali za kufanyia kazi kwa uhakika,” alisema.
 
Alisema wakati umefika ndani ya CCM wa kuondokana na maisha ya kutafuta fedha na rasilimali za kufanyia shughuli zake kwa taratibu za zimamoto, aliongeza kuwa kwa kufanya hivyo kuna hatari ya siku moja kujikuta moto umekuwa mkubwa mno na hauzimiki kwa urahisi, lakini jambo baya zaidi ni hatari ya kuhusishwa na watu tusiokuwa na uhakika nao na kupata hatari kuishia kupata fedheha.
 
Mwenyekiti Kikwete aliwaomba viongozi na wanachama wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), Vijana na Wazazi watambue umuhimu wao kwamba ni viungo muhimu ndani ya Chama.
 
“Naomba watambue kuwa jumuia kuwa imara ni kwa maslahi mapana ya Chama chetu. Hatuna budi tufanye kila tuwezalo kuhakikisha kuwa jumuia zetu zinaimarishwa ipasavyo kwa ngazi zote,” alisema.
 
Aliwahakikishia wana CCM na wanachama na viongozi wa jumuia za Chama ushirikiano wake wa hali ya juu katika jitihada za kujenga na kuimarisha jumuia hizo.
 
Awali, alimshukuru mwenyekiti mstaafu Benjamin Mkapa kwamba ndiye mwalimu wake kwa kuwa ndiye aliyemlea na kumlimda mpaka alipofika hapo. Kwanza alikuwa mwalimu wake wa masuala ya kidiplomasia kwa kipindi chote cha miaka 10 alichokuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.
 
Alisema pili anamshukuru kwa imani yake na mapenzi yake kwake wakati wa mchakato, baada ya uteuzi, wakati wa uchaguzi na baada ya uchaguzi. Na sasa akiwa Rais, amekuwa mshauri wake na msaada kwa jambo lolote anapoona anaweza kumsaidia.
 
Kikwete alisema kuwa ushahidi mwingine mkubwa wa upendo na imani yake kwake ni uamuzi wake wa kuacha uenyekiti kabla ya wakati wake na kumpendekeza awe mgombea pekee wa nafasi hiyo ya uenyekiti.
 
“Ni imani iliyoje kwangu mtu anayoweza kuionyesha zaidi ya hii. Aliponiambia Februari 2006 kuwa ameamua kuacha uenyekiti na kuniachia, nilimwambia kuwa naona ilikuwa mapema mno, mimi ningependa kwanza nipate nafasi ya kujiimarisha katika serikali kabla ya kuchukua uongozi wa chama,” alisema.
 
Alisema anakumbuka kumwambia Mkapa kuwa: “Unajua Mzee nina miezi miwili tu, sina haraka… endelea mpaka 2007”. Mzee Mkapa akajibu kuwa na yeye alipokea hivyo hivyo kutoka kwa Mzee Mwinyi.
 
Kikwete alisema, Mkapa alisisitiza kuwa huu ni utaratibu mzuri, ni bora kuudumisha. Akanisihi kuwa nikubali maombi yake. Nikamjibu sawa ila siyo sasa. Akaniambia haitakuwa ghafla na hata Mzee Mwinyi alimkabidhi zaidi ya miezi sita baada ya kuchaguliwa, hivyo alidhani Juni, mwaka huu ungekuwa wakati muafaka, nikamwambia “Ndiyo Mzee”.

How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.