SERIKALI jana ilitangaza mabadiliko makubwa katika mfumo na viwango vya kodi kwenye bidhaa mbalimbali yakiwamo mafuta ya taa, petroli na dizeli, hatua ambayo mbali ya kuiongezea mapato, inaweza kusababisha kupanda kwa gharama za maisha katika mwaka ujao wa fedha unaoanza Julai mosi.
Chini ya mabadiliko hayo, bei ya bidhaa kadhaa zitapanda kutokana na hatua hiyo ya serikali kurekebisha ushuru wa bidhaa hizo na kuupandisha hadi kufikia asilimia saba.
Bidhaa nyingine zilizoingia katika orodha ya ama ushuru wake au kodi kupanda ni mafuta ya viwandani, vinywaji baridi (soda), bia, mvinyo, pombe kali pamoja na bidhaa za tumabaku.
Akiwasilisha bajeti ya serikali kwa mwaka wa fedha 2007/08 bungeni jana, Waziri wa Fedha, Zakia Meghji, alisema kuwa, mabadiliko hayo yanalenga kuiwezesha serikali kuboresha maisha ya wananchi wake.
Chini ya mabadiliko hayo, ushuru wa vinywaji baridi umeongezwa kutoka sh 45 hadi kufikia sh 48 kwa lita, bia inayotengenezwa na nafaka ya hapa nchini ambayo haijaoteshwa, itapanda kutoka sh 161 hadi sh 173 kwa lita, aina nyingine ya bia kutoka sh 274 hadi sh 294 kwa lita.
Meghji aliliambia Bunge kuwa, ushuru wa mvinyo unaotengenezwa kwa zaidi ya asilimia 25 ya zabibu zinazoagizwa kutoka nje ya nchi nao utapanda kutoka sh 878 hadi sh 940 kwa lita na pombe kali kutoka sh 1,302 hadi sh 1,394 kwa lita.
Kuhusiana na bidhaa za mafuta, Meghji alibainisha kuwa ushuru wa petroli utapanda kwa sh 22 kutoka sh 315 kwa lita za sasa na kufikia sh 337 kwa lita. Aidha, ushuru wa dizeli utapanda kutoka sh 292 hadi sh 312 kwa lita.
Ushuru wa mafuta ya taa nao utapanda kutoka sh 52 kwa lita hadi sh 56 kwa lita; mafuta mazito ya mitambo (HFO) kutoka sh 109 kwa lita hadi sh 117 kwa lita na dizeli nzito ya kuendeshea mitambo viwandani (IDO) kutoka sh 366 kwa lita hadi sh 392 kwa lita.
Meghji alisema kuwa pamoja na hatua zitakazochukuliwa ni kurekebisha viwango vya ushuru wa bidhaa kwenye sigara, ambapo sasa sigara zisizo na kichungi na zinazotengenezwa kutokana na tumbaku inayozalishwa hapa nchini kwa kiwango cha angalau asilimia 75, ushuru wake utapandishwa kutoka sh 4,462 hadi sh 4,775 kwa sigara elfu moja.
Aidha, ushuru wa sigara zenye kichungi na zinazotengenezwa kutokana na tumbaku inayozalishwa hapa nchini kwa kiwango cha angalau asilimia 75, utapanda kutoka sh 10,529 hadi sh 11,266 kwa sigara elfu moja.
Meghji alisema pia kuwa sigara nyingine zenye sifa tofauti na zilizoainishwa hapo juu, ushuru wake utapanda kutoka sh 19,195 hadi sh 20,460 kwa sigara elfu moja.
Alibainisha pia kuwa tumbaku ambayo iko tayari kutengeneza sigara (cut filler), ushuru wake utapanda kutoka sh 9,657 hadi sh 10,333 kwa kilo, na ushuru wa bidhaa kwa ‘Cigar’ utaendelea kubaki kuwa asilimia 30.
“Kwa pamoja, hatua hizi katika Sheria ya Ushuru wa Bidhaa zinakadiriwa kuongeza mapato ya serikali kwa kiasi cha sh bilioni 34.446,” Meghji aliliambia Bunge.
Mabadiliko hayo yanakwenda mbali zaidi na kuigusa sekta nyeti ya Sheria ya Ushuru wa Barabara kwenye Mafuta ya Petroli, Meghji alisema.
“Ili kuongeza uwezo wa Mfuko wa Barabara kumudu ongezeko la gharama za matengenezo ya barabara, serikali inapendekeza kuongeza ushuru wa mafuta ya petroli kutoka sh 100 za sasa kwa lita hadi sh 200 kwa lita,” alisema Waziri wa Fedha.
Aidha, serikali inapendekeza kubadili mfumo wa kutoza ada ya mwaka ya leseni za magari kutoka kiwango kimoja cha sh 20,000 kwa gari na kuwa na viwango vitatu kulingana na ujazo wa injini.
Chini ya mapendekezo hayo, Meghji alisema, kwa magari yenye ujazo wa injini usiozidi 1,500cc kiwango cha ada kitakuwa sh 80,000 kwa mwaka; kwa magari yenye ujazo wa injini unaozidi 1,500cc lakini hauzidi 5,000cc, kiwango cha ada kitakuwa sh 230,000 kwa mwaka, na kwa magari yenye ujazo wa injini unaozidi 5,000cc kiwango cha ada kitakuwa sh 100,000 kwa mwaka. Haya ni magari ya mizigo na mabasi ya abiria.
Meghji aliliambia Bunge kuwa hatua hizi kwa pamoja zinakadiriwa kuongeza mapato ya serikali kwa kiasi cha sh bilioni 169.737.
Meghji, aliliambia Bunge pia kuwa katika kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) inaendelea kuimarisha usimamizi wa kodi na mapato mengine yanayokusanywa na Mamlaka hiyo.
“Serikali inapendekeza kufanya marekebisho ya mfumo na viwango vya baadhi ya kodi katika maeneo kadhaa ili kurahisisha ukusanyaji na kuhamasisha wananchi kulipa kodi kwa hiari, na pia kuongeza mapato kwa ajili ya matengenezo ya barabara, na kwa ajili ya mfuko wa umeme vijijini,” alisema.
Kupitia bajeti hiyo, serikali imependekeza kurekebisha baadhi ya viwango vya kodi na tozo nyingine zisizo za kodi chini ya sheria mbali mbali za kodi.
Pamoja na mambo mengine, serikali imependekeza kusamehe Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwenye mitungi ya kuzimia moto ili kupunguza gharama na kuhamasisha matumizi ya vifaa hivyo katika kupambana na majanga ya moto.
Pia imependekeza kuondoa msamaha wa VAT kwenye nyuzi ghafi zinazotengenezwa nchini ili kuwawezesha wazalishaji kurejeshewa VAT wanayolipa kwenye malighafi na huduma kama umeme, dawa n.k. na hivyo kuwaongezea uwezo wa ushindani.
Aidha, mapendekezo mengine yanahusu kufanya marekebisho katika aya ya Nne ya Jedwali la Tatu la Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani ili unafuu unaotolewa kwa shughuli za utafutaji na uchimbaji wa madini uhusishe pia shughuli za utafutaji wa gesi na mafuta ya petroli.
Kwa mujibu wa Meghji: Hatua hizi katika Kodi ya Ongezeko la Thamani kwa pamoja zinakadiriwa kuongeza mapato ya serikali kwa kiasi cha sh milioni 400.
Aidha, Meghji alisema serikali inapendekeza kupunguzwa kwa kiwango cha chini cha kukokotoa kodi ya mapato ya ajira kutoka asilimia 18.5 hadi asilimia 15 ili kupunguza mzigo wa kodi kwa wafanyakazi wa kipato cha chini.
“Hatua hii ambayo itaongeza kipato halisi cha wafanyakazi, itapunguza mapato ya serikali kwa kiasi cha sh bilioni 1.809,” alibainisha.
Hata hivyo, nafuu hii kwa wafanyakazi inaweza ikawa isiwe na afueni kwao kutokana na kupanda kwa ushuru wa bidhaa muhimu kama mafuta ya taa na petroli, ambayo kwa namna yoyote ile yatasababisha kupanda kwa bei ya bidhaa nyingine kama chakula na nauli za mabasi.
Kuhusu mabadiliko ya ushuru wa bidhaa, Meghji alipendekeza yafuatayo; kuondoa sharti la kuweka alama ya “FOR EXPORT ONLY” katika bidhaa zinazouzwa nje ya nchi. Alisema sharti hilo limeonekana kukwamisha juhudi za kuongeza mauzo nje badala ya kuhamasisha.
Aidha, imependekezwa kurasimisha ndani ya Sheria ya Ushuru wa Bidhaa, utaratibu wa kuirejeshea Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), makusanyo ya ushuru kwa bidhaa zinazozalishwa Bara na kuuzwa au kutumika Zanzibar.
Wakati huo huo, ile kiu ya wafanyakazi wengi wa umma kujua viwango vya ongezeko la mishahara, imetumbukia nyongo, baada ya Meghji kutobainisha kinagaubaga ongezeko hilo.
Hata hivyo, Meghji aliliambia Bunge kuwa serikali imepokea mapendekezo ya Tume ya Rais kuhusu kuboresha masilahi ya watumishi wa umma.
“Uchambuzi wa mapendekezo hayo unaendelea. Serikali itatekeleza mapendekezo ya tume kwa awamu, kuanzia bajeti ya 2007/08. Aidha, serikali imezingatia mahitaji ya kuongeza ajira hasa katika sekta za elimu na afya. Maelezo zaidi yatatolewa na Waziri wa Utumishi pamoja na mawaziri wa sekta hizo mbili,” alisema.