MAJIRA kama haya, miaka miwili tu iliyopita, taifa hili lilikuwa katika mchakato wa kumtafuta rais wa nne wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania.
Ingawa mchakato ulikuwa umeanza, machoni mwa wachambuzi wa mambo wa ndani ya nchi na hata wale wa nje, Kikwete ndiye aliyekuwa akionekana dhahiri kuwa; ‘President in the Waiting.’ (yaani rais mtarajiwa).
Ingawa katika uchaguzi huo, wagombea wengine wawili wa urais, Profesa Ibrahim Lipumba (CUF) na Freeman Mbowe (Chadema) walionekana kuamsha hisia mpya za kuungwa mkono na makundi kadha wa kadha, bado ukweli ulikuwa ukionekana kuwa walikuwa washindani wa kutoa changamoto na si wa kuchukua jahazi la uongozi, japo kwa wakati ule.
Zama hizo, vyombo mbalimbali vya habari, hususan magazeti takriban yote ya kila siku, yalikuwa yakiimba wimbo mmoja zaidi katika kampeni; Kikwete, Kikwete, Kikwete.
Vichwa vya habari kama vile vilivyokuwa vikiandika; Kikwete shujaa!, Hakuna kama Kikwete! Kikwete we acha tu! Kikwete aiteka… na vingine vingi ambavyo kimantiki vilikuwa vikifanana na hivyo, vilipamba kurasa za habari na makala katika magazeti mbalimbali.
Waandishi na wahariri waliokuwa na jeuri ya kuandika kwa kina habari na makala za wagombea wengine wa urais na kufikia hatua ya kuwapamba kwa namna ile ya Kikwete, walikuwa wakihesabika na idadi yao ilikuwa ikipungua kadri siku za uchaguzi zilivyokuwa zikikaribia.
Kile ambacho Kikwete mwenyewe hivi karibuni alipata kukiita maandalizi yake ya miaka 10 ya kuwa Rais wa Tanzania yalijipambanua kwa uwazi kabisa.
Kati ya mwezi Machi na Mei mwaka 2005 wakati CCM ikiwa katika mchakato wa kutafuta mgombea urais, wakiwa wamejitokeza wanasiasa 10 kusaka kiti hicho, niliandika safu za makala za kuwachambua wagombea hao wote, nikieleza nguvu na udhaifu wa kila mmojawapo.
Kwa sababu ya mwelekeo wa makala yangu ya leo, nitanukuu moja ya sehemu muhimu inayoendana nayo, inayomuelezea Kikwete niliyemuweka katika mizania ya wagombea wengine washindani wake. Niliandika hivi:
Ni jambo la wazi kwamba, watu ambao wamekuwa wakimuunga mkono Kikwete, tangu mwaka 1995, wamekuwa wakimuona kama mgombea anayewakilisha mawazo ya kizazi kipya cha Watanzania, na mtu anayeweza akawa daraja la mahusiano kati ya wazee wastaafu na vijana wenye uchu wa kutaka kupewa nafasi ya kuongoza.
Pamoja na ukweli kwamba, Kikwete anapogombea hivi sasa ana umri wa miaka 55, vijana na wana CCM wanaoungana na falsafa ya Baba wa Taifa ya kuwataka wazee wang'atuke madarakani wanamuona kuwa ndiye chaguo lao sahihi kabisa la 'wakati huu' pamoja na ukweli kwamba, watu wa rika lake kama vile Frederick Sumaye (55) na Mark Mwandosya (57) wanaonekana kuwa ni wa kizazi kingine na tena waliochomoza kwa bahati mbaya tu.
…Swali moja hadi hivi sasa linaonekana kutojibiwa sawasawa: Ni kwa nini basi miaka 10 baada ya kugombea urais kwa mara ya kwanza mwaka 1995, Kikwete bado anaonekana ndiye mwakilishi wa Watanzania wa kizazi hiki na mtu anayeonekana kufaa zaidi kuongoza taifa katika karne ya 21 zaidi kuliko ilivyo kwa wengine kama hao akina Sumaye, Mwandosya kwa upande mmoja na hata akina Malecela, Salim, Iddi Simba kwa upande mwingine?
Je, ni hulka yake ya kujichanganya na watu wa rika tofauti? Ni haiba yake ya ujana aliyodumu nayo kwa miaka yote 10 tangu mwaka 1995? Ni upofu wa mashabiki zake? Ni upeo wake mkubwa wa kuona mambo? Ni hoja zake za kisasa? Ni uzalendo wake? Ni mapungufu waliyonayo washindani wake? Ni kitu gani hasa? Watanzania wanapaswa kuliangalia hilo na kulitafutia majibu.
Hicho nilichokiandika Aprili mwaka 2005 ndicho ambacho kweli kilitokea ndani ya CCM. Benjamin Mkapa, akiwa Mwenyekiti wa Taifa wa CCM huku akiungwa mkono kwa siri siri na majemedari kama Kingunge Ngombale Mwiru, Ali Hassan Mwinyi na Rashid Kawawa (kwa kuwataja wachache) walitumia ajenda za namna hiyo hiyo kumpa ushindi Kikwete.
Siku ilipotoka makala yangu hiyo, rafiki mkubwa wa Kikwete, Rostam Aziz, ambaye sasa ni Mweka Hazina wa CCM Taifa, alinipigia simu na akaeleza kushangazwa kwake na hoja zangu hususan katika aya hiyo ya mwisho.
Kwa maneno yake mwenyewe; Rostam aliniuliza; “Hivi mdogo wangu Kibanda, unaishi katika dunia gani? Kweli hujui ni kwa nini Kikwete ni mgombea maarufu na anayekubalika kuliko mwingine yeyote?
Kwa bahati mbaya kwangu, hata Rostam mwenyewe hakunieleza ni kitu gani hasa kilichokuwa kikimfanya Kikwete atokee kuwa kipenzi cha Watanzania, hata kufikia hatua ya baadhi ya wadadisi wa mambo kama akina Prince Bagenda kumuita ‘Tumaini Lililorejea’.
Hata hivyo, mwitikio mkubwa na wa kipekee wa wapiga kura na matokeo ya ushindi wa asilimia 80, yaliyopewa majina anuai, ushindi wa kishindo, kimbunga, el-nino na mengi mengine yaliendelea kumpamba, Kikwete aliyeonekana kuwa mtu wa watu.
Mmoja wa wasaidizi wakubwa wakati wa kampeni za urais wa CCM, niliyezungumza naye wakati akiwa katika msafara wa Kikwete mkoani Ruvuma, aliniambia kwamba, wengi wanaomuunga mkono Kikwete katika harakati zake, wanamuona kuwa ndiye kiongozi pekee atakayeleta mabadiliko makubwa ndani ya CCM na katika mfumo wa kiutawala.
Msaidizi huyo wa Kikwete huku akiwa amezingirwa na wapambe na watu wengine kadhaa waliokuwa ndani ya timu ya ushindi wa mwanasiasa huyo alinieleza, nitamnukuu, ili nisipotoshe maana; “Kikwete ni mpinzani ndani ya CCM, wenzake wengi wanalijua hilo na ndiyo maana baadhi ya watu wanamuogopa wakijua akiingia madarakani atafanya mabadiliko makubwa.”
Leo hii ninaweza nikawaeleza Watanzania wenzangu kuwa, kwa kiwango fulani, nilianza kushawishika kuwa JK alikuwa mtu wa mabadiliko na kiongozi ambaye angeweza kuleta mapinduzi makubwa kabisa ya kifikra katika mfumo wa kiutawala.
Ni bahati mbaya sana kwamba, miezi 18 sasa tangu aingie madarakani, matarajio makubwa waliyokuwa nayo watu wengi juu yake, yanaonekana ama kutoweka au kutokwenda kama ilivyodhaniwa awali.
Ahadi zake kwamba ari, kasi na nguvu mpya vitakuwa chachu dhidi ya rushwa, uwajibikaji serikalini na hata katika mahusiano ya kisiasa na kijamii na vyama vingine vya siasa na nchi jirani, ni mambo yanayoonekana kutokuwapo.
Tunapowauliza vijana wasio na ajira waliojitoa mhanga kumuunga mkono kwa kishindo, wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu waliofikia hatua hata ya kumuona mtu aliyekuwa akifuata nyayo za Baba wa Taifa, wadadisi huru wa mambo na wasomi wa kada mbalimbali, jibu utakalopata ni rahisi kabisa; ‘tumeanza kukata tamaa’, ndivyo wanavyosema.
Si rahisi hivi sasa kusema kwa uhakika kabisa iwapo kasi, ari na nguvu inaonekana katika utendaji wa wizara moja moja au hata idara zake, hata baada ya kufanyika kwa milolongo ya semina elekezi na JK mwenyewe kutembelea wizara hizo na idara kadhaa nyeti.
Kile ambacho Waziri Mkuu, Edward Lowassa alipata kukielezea kuwa mwisho wa ‘business as usual’ serikalini, ndicho kinachoonekana kuendelea kubakia kikistawi.
Ukiacha tu kwamba, hivi sasa Rais ni Jakaya Kikwete na Waziri Mkuu ni Edward Lowassa, kasi ya mambo serikalini inabakia ile ile ya zama za Benjamin Mkapa na Frederick Sumaye.
Jambo baya zaidi ni kwamba, kabla Mkapa hajaanza kusukwasukwa na jinamizi la maamuzi yake ya kibiashara akihusishwa na mikopo ya benki na kampuni ya ANBEM, midomo ya Watanzania ilishaanza kusema mara kwa mara; ‘ni afadhali serikali iliyopita.’
Ingawa ni kweli kwamba, Kikwete anaweza akatembea kifua mbele, akijivunia mafanikio yake na Lowassa katika kuchochea ujenzi wa shule nyingi za msingi na ongezeko la wanafunzi wanaojiunga na elimu ya sekondari katika kipindi chao kifupi madarakani, bado sekta nyingine muhimu kama afya, miundombinu, maji, kilimo hazina mifano hai ya kuisemea.
Hivi sasa Watanzania hawawajui mawaziri na naibu mawaziri wa Kikwete kwa majina na kwa kazi za wazi za uwajibikaji wanazozifanya kwa namna tuliyopata kuiona zama za akina John Magufuli, Augustine Mrema, Lowassa mwenyewe, Meghji (wa zama zile).
Hali hii ya mambo imetufanya baadhi yetu tuanze kujiuliza je, huyu ndiye Kikwete yule yule aliyeungwa mkono kwa kishindo kwa hoja za ushawishi kwamba ataanzia pale alipoishia Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere?
Baadhi yetu ambao tuliaminishwa tukubali kuwa Kikwete ni mpinzani wa kweli ndani ya CCM na ‘nabii’ aliyekuja kurejesha heshima iliyopotea ya chama hicho tawala na kuirejeshea msingi wake wa ‘mapinduzi’, leo hii tumeanza kuona ndivyo sivyo.
Wakati tukiona namna Kikwete anavyolemewa na mambo, tumeanza kujiuliza ni kitu gani hasa kinamzuia Kikwete kuchukua hatua dhidi ya mawaziri wake wengi wasindikizaji, wakuu wa mikoa wavivu na wakuu wa wilaya waliolala?
Hivi ni jambo gani hasa linalomfanya ashindwe kuwawajibisha makatibu wakuu na wakurugenzi wa taasisi na idara za serikali aliowateua, walioshindwa kusimamia vyema maeneo yao ya kazi.
Ingawa mashahidi na manabii wa uongo wamekuwa wakijaribu kujenga hoja za kumlinda Kikwete na serikali yake kwa sababu wanazozijua wao, ukweli unabaki pale pale kwamba, matarajio makubwa waliyotujengea, yameanza kufifia na tuombe Mungu yasije yakatoweka kabisa.
absakib@yahoo.com
07 54 00 10 10