Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Nani atamnyima kura mtoto wa rais NEC?
Nani atamnyima kura mtoto wa rais NEC?
By Habari Tanzania | Published  06/13/2007 | Habari za Kitaifa | Rating:

MWALIMU Nyerere wakati anaondoka madarakani, hakuacha hata mtoto wake mmoja kwenye siasa za Chama Cha Mapinduzi (CCM), zaidi ya kuacha mwanawe mkubwa, Makongoro, akiwa ameiasi CCM na kwenda alikokuwa anadhani panamfaa.

Mwalimu hakuona umuhimu wa damu yake kujiingiza katika siasa zaidi ya sifa safi za mtu. Nani wakati wa Mwalimu kwa mfano angeona Makabachori wakihonga na kuupata ubunge?

Nani atakuwa amesahau jinsi zoezi zima la kupata wagombea kipindi hicho lilivyokuwa chafu hasa kutokana na wafanyabiashara kulivamia na kutapakaza uchafu wao?

Hebu waulize sifa ya Ridhiwani, mtoto wa Rais Kikwete anayewania ujumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Taifa kupitia Wilaya ya Bagamoyo ni ipi zaidi ya kuwa mtoto wa rais.

Baba ni rais. Mama naye ana ki-NGO chake cha kutafutia riziki. Mtoto leo naye anataka ulaji kwenye chama.

Nenda kwa Makamba. Baba katibu mkuu wa chama. Mtoto mwandamizi Ikulu! Hii jamani ni ‘nepotism’ katika hali yoyote.

 Ukitaka kujua madhara ya watu kutumia sifa za wazazi wao kujiingiza kwenye siasa, angalia Zanzibar ilivyoteseka wakati CCM hiyo hiyo ikiwalazimisha Wazanzibari kutawaliwa na mtoto wa rais wa kwanza wa Zanzibar, yaani rais wa sasa.

Watu walipigwa hadi wengine kuuawa. Kisa mtoto wa rais wa zamani achukue kiti cha baba yake, utadhani cha urithi.

Waulize hadi leo sifa gani Karume alikuwa nazo kuliko watu kama Dk. Gharib. Hakuna, bali jina Karume.

Kuna mambo mawili yamenisukuma kuandika makala hii. Jambo la kwanza ni kuonyesha jinsi CCM inavyoanza kutapatapa na inavyoishi kwa kuanza kujichimbia kaburi lake huko tuendako.

 Jambo la pili ni kuonyesha jinsi CCM ilivyotekwa na vikundi viwili vya watu, yaani wafanyabiashara na wale wanaojiona wakongwe, ambao ndio wenye dola.

Hili linajidhihirisha kwenye sura zinazowania nafasi za Halmashauri Kuu ya Taifa ndani ya CCM.

Mtu kama  Kikwete hakupaswa kuruhusu mtoto wake kuwania nafasi hiyo na kama alishamshauri, basi haukuwa ushauri mzuri.

Ridhiwani amewahi kufanya nini kisiasa hadi akwee anakotaka kukwea? Je, hiyo ndiyo CCM ya wakati ule?

Kwenye chama ni mtoto wa rais. Akienda kwenye mabenki yetu kukopa mtoto wa rais. Akienda kupitisha mizigo bandarini, mtoto wa rais! Jamani hii nchi sasa imekuwa mali ya rais na wenzake, ambao kuwapo na kutokuwapo ukivipambanisha hata huoni tofauti. 

Ukiachana na  Ridhiwani,  watoto wengine wa vigogo waliojitokeza ni pamoja na Zainab Kawawa, mtoto wa waziri mkuu mstaafu, mzee Rashid Kawawa, na Nape Nnauye, mtoto wa naibu katibu mkuu wa zamani wa CCM.

 Wengine ni Tom Mwang’onda, ambaye pia ni mbunge wa kuteuliwa na rais. Kijana huyo pia ni mtoto wa mkuu wa usalama wa zamani. Pia yupo mtoto wa Mama Gertrude Mongella, John Mongella, ambaye kwa sasa ni mkuu wa wilaya ya Kigoma Mjini.

Turejee kwa watoto wa wakubwa. Kesho usishangae kusikia mtoto wa Mwinyi akiwa rais na wa Kikwete au Makamba akiwa makamu wa rais au waziri mkuu. Hii ni hatari.

Huu ni ufashisti wa kizamani uliowahi kufanyika kwenye nchi kama Korea ya Kaskazini, ambako mwanzilishi wa taifa hilo Kim il Sung alimuachia madaraka mwanawe mlevi, ambaye licha ya kuwa mzigo amekuwa tishio kwa  ufanisi wa nchi hiyo. 

Hivyo kwa mchezo huu mchafu usishangae siku moja ukakuta nchi ikiongozwa na watoto wa viongozi wastaafu na wa wafanyabiashara, tena wenye mabaka.

Hapa ni kama kuna mashindano ya kuipora nchi hii. Leo unapomwangalia mtoto wa Kikwete kwa mfano, ambaye kwangu mimi kwa sasa hana sifa ya kutaka kuingia anakotaka kwenda, ujue ufalme wa aina mpya unaanza kuzuka.

 Jingine lililonishangaza ni kwamba, sikuamini niliposoma taarifa kuwa mmoja wa watu waliochukua fomu za kugombea ujumbe wa NEC ni Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Idd Pandu Hassan.

Ni ajabu kwa mwanasheria mkuu ambaye bado yumo ofisini kujiingiza kwenye siasa za vyama. Maana yeye ni mtumishi wa umma. Hafai huyu kuwa mwanasheria mkuu.

 Hivi, huyu mwanasheria mkuu wa Zanzibar ambaye ni mkereketwa wa CCM kweli anaweza kuwatendea wanachama wa vyama vingine haki? 

Sina nakala ya Katiba ya Zanzibar. Lakini katiba hiyo naamini iko chini ya Katiba ya Muungano. Je, huu si uhuni wa kisiasa kwa mambo ya chama kuvunja hata mantiki ya kawaida ambapo Tanzania tumetamka wazi baada ya kuanzisha mfumo wa vyama vingi kuwa watumishi waliomo kwenye ofisi za umma hawapaswi kuwa mashabiki au wanachama wa vyama vyovyote?

 Kwa wafanyakazi wadogo wadogo wa kawaida hili halina madhara makubwa. Lakini linapokuwa kwa nafasi nyeti kama jaji, polisi, wanajeshi na wengine ambao kwa mujibu wa kazi zao wako kwenye mkondo wa kusimamia haki, tukubali kuna tatizo, tena si dogo.

 Leo CCM inapwaya sana na ina sifa mbaya tofauti na ile iliyokuwa nayo wakati wa kupigania uhuru, ambao sasa inaanza kuufuja.

Katika kuadhimisha miaka 30 niliandika makala juu ya CCM ilivyojigeuza baunsa na mporaji wa haki za wananchi.

Niliongelea jinsi ilivyopora ardhi na kuigeuza  maegesho ya magari. Hii si sifa ya chama cha wananchi.

 Pia hata ukiangalia miradi michafu kama ule wa bomba la kupeleka mafuta Kigoma, unapata kujua kuwa CCM sasa inaanza kujikaanga kwa mafuta yake.

Chama hakiongozwi kama bendi ya muziki kwa kuangalia sauti za waimbaji na minenguo yao, bali sifa thabiti za uongozi ambao mara nyingi walio nazo ni wachache waliobahatika na kuandaliwa baada ya kuchomoza na kuonyesha vipawa vyao.

Kuna haja ya wapinzani kujiimarisha tayari kuchukua madaraka.

Maana kwa mwendo huu wa chama kuwa mali ya koo fulani, CCM imo ICU ikingojewa kuzikwa.

mpayukaji@yahoo.com


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments
  • Comment #1 (Posted by Loota Mungaya Lotisia)
    Rating
    Makala haya ni mazuri sana ukisinatia kweli kurithiana kiti sio kitu kizuri. Lakini ni vema tukaangalia kuwa Ridhwani ni Mtanzania na ni mtu mwenye utashi kama baba yake. Haitakuwa jambo la busara kwa Kikwete kumnyima mwanaye afuate nyayo zake. Hata hivyo kuwa mwanasiasa ni swala la utashi na sio lazima na pia sio ushauri wa kushauriwa. Chukua mfano Kabila. Baada ya baba yake kufa na yeye kuingia madarakani mambo sasa ni shwari kabisa. Hivyo akili ya Kikwete na ya Ridhwani ni tofauti Kabisa. Na nafikiri hata malengo yao ni tafauti kabisa. Hivyo sio vyema kumlaumu Kikwete kwa hilo.
     
Submit Comment


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.