UMOJA wa Vijana wa Chama cha Wananchi (CUF), umemtaka Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad, kuachana na mazungumzo yanayoendelea, ya kutafuta muafaka wa kisiasa wa Zanzibar kati ya CUF na Chama Cha Mapinduzi hadi hapo Rais Jakaya Kikwete atakapoonyesha mwelekeo mwema.
Taarifa ambazo Tanzania Daima imezipata kutoka ndani ya vikao viwili vya juu vya siri vya chama hicho, vilivyokutana jana katika ofisi za Makao Makuu ya CUF, Buguruni, jijini Dar es Salaam, zinaeleza kuwa, msimamo mkali wa vijana hao, maarufu kwa jina la Blue Guards, uliungwa mkono na wajumbe wengi.
Mkutano wa kwanza kujadili hali ya kisiasa Zanzibar, ulikuwa ni ule wa Kamati ya Taifa ya Ulinzi na Usalama, ulioongozwa na Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba na baadaye kikaanza kikao cha Kamati ya Utendaji Taifa kilichokaa chini ya Maalim Seif.
Habari kutoka ndani ya vikao hivyo viwili zinaeleza kuwa, hali ya mambo ilikuwa ni ya mashaka makubwa baada ya Blue Guards kuwasilisha ushahidi wa mikanda ya video katika Kamati ya Utendaji iliyokuwa ikionyesha hotuba za Katibu Mkuu wa CCM, Yussuf Makamba alizotoa wakati akiwa Pemba, hivi karibuni.
Umoja huo unaoongozwa na mwanaharakati maarufu wa chama hicho, Said Miraji, katika taarifa yake kwa Kamati ya Utendaji, ulisema bayana kusikitishwa na matamshi makali na yenye mwelekeo mbaya yaliyotolewa na Makamba wakati wa ziara yake hiyo.
“Vijana walitubana kweli leo (jana). Waliingia katika kikao wakiwa na mikanda ya video na wakaonyesha hotuba za Makamba Pemba, hata kufikia hatua ya kuungwa mkono na takriban wajumbe wote wa Kamati ya Utendaji Taifa,” alisema mjumbe mmoja wa vikao hivyo ambaye pia ni kiongozi wa juu wa CUF.
Kiongozi mwingine wa juu wa CUF, aliyezungumza na Tanzania Daima jana jioni, alikiri kutokea kwa hali hiyo katika vikao hivyo.
Kwa mujibu wa kiongozi huyo, vijana hao walielezwa kushtushwa na hoja kuu nne za Makamba wakati wa ziara zake hizo, hata kufikia hatua ya kuzielezea kuwa ndiyo msimamo wa Rais Kikwete.
Kauli ya Makamba kuwataka Wazanzibari kutulia kwa kuwa hakutakuwa na uchaguzi mwingine kabla ya mwaka 2010, hata kufikia hatua ya kutoa mfano kuwa ushindi wa Yanga hauwezi kwenda Simba, ndiyo iliyokuwa ya kwanza kutolewa kama kielelezo.
Aidha, madai ya Katibu Mkuu huyo dhidi ya CUF kuwa imekuwa ikiwatisha Wapemba wanaotaka kujiunga na CCM, ilitolewa kama ushahidi wa pili na wa namna chama hicho tawala kinavyoyacheza shere mazungumzo kati yake na chama hicho kikuu cha upinzani Zanzibar.
Kama hiyo haitoshi, kauli ya Makamba kusema chama hicho kilikuwa kikiyapuuza madai ya viongozi wa CUF, kwamba Wapemba wamekuwa ni watu waliosahaulika na kunyanyaswa, nayo ilielezwa kuzusha hoja nyingi ndani ya kikao cha Kamati ya Utendaji.
Suala la mwisho lililohitimisha hoja za vijana hao wa Blue Guards kuhusu kauli hizo za Makamba, hata kufikia hatua ya wana CUF kuwashawishi wajumbe wa Kamati ya Utendaji kutaka majibu kutoka kwa Kikwete, ni ile aliyosema kuwa, kulikuwa hakuna kitu kama serikali ya mseto au ya umoja wa kitaifa visiwani humo.
Taarifa kutoka ndani ya kikao hicho ambacho kilikuwa kikiendelea hadi wakati tukienda mitamboni zinaeleza kuwa, wajumbe wengi wa mkutano huo waliafiki mapendekezo ya Blue Guards na mapendekezo ya maamuzi yao, yanatarajiwa kuwasilishwa mbele ya Baraza Kuu la Uongozi la chama hicho linalotarajia kukutana kuanzia kesho.
Kwa muda mrefu sasa, na hususan tangu Makamba aende Zanzibar, hali ya hewa visiwani humo imechafuka, hasa baada ya wabunge na wawakilishi wa CUF na baadaye Blue Guards kuwataka viongozi wao kuachana na mazungumzo hayo.
Hata hivyo, hatua ya makundi hayo ya CUF imeshindwa kutekelezwa baada ya viongozi wa juu wa vyama vyote viwili kuanza kukutana kwa ajili ya kupanga tarehe mpya za kukutana, hususan huko Dodoma wakati huu Bunge la bajeti linapoendelea.