Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  CCM ni chama cha siasa au kampuni ya biashara?
CCM ni chama cha siasa au kampuni ya biashara?
By Habari Tanzania | Published  06/12/2007 | Habari za Kitaifa | Rating:
NIMEPATA mshtuko baada ya jana kuona habari kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kina kampuni ya biashara iitwayo Tanzania Green Company Limited!

Ni kwenye gazeti la Tanzania Daima. Habari hiyo pia ilishawahi kuandikwa na gazeti la The East African ambalo lilifichua malalamiko kutoka kwa kampuni nyingine kuwa TGC-CCM ina masilahi kwenye tenda ya kandarasi ya kujenga mtambo wa kusafisha mafuta na bomba la kusafirisha mafuta hadi Kigoma, Mwanza na nchi jirani! Mradi wenyewe una thamani ya sh bilioni 2.6.

Hii ni baada ya kampuni tatu za ndani na za kigeni kutaka kwenda mahakamani kuzuia serikali kutekeleza mradi huu.

Mradi huu ambao CCM ina masilahi, umetolewa kwa kampuni za mafuta za Qatar-Noor Oil and Industrial Technology ambayo uhusisha pia Roneg AG ya Ujerumani na Stroytransgaz na Prometeus za Urusi.

Kilichonipa mshtuko na kutamani kuwashinikiza Watanzania kuandamana kuishinikiza CCM ikae kando tuwe na serikali ya mpito ni kugundua kuwa kumbe CCM haina uadilifu tena, hadhi wala stahiki ya kuendelea kuwa madarakani.

Na sababu kubwa ni kwamba imepungukiwa imani na heshima iliyokuwa navyo.

Je, CCM ni chama cha siasa au kampuni ya biashara? Kuwa na vitega uchumi kama haviathiri masilahi ya taifa na uadilifu si tatizo.

Hebu tujiulize mantiki ya serikali ya CCM kutangaza rasmi kuwa ilijitoa kwenye biashara ili kusimamia uwekezaji.

Je, kunapokuwa na serikali yenye kuendeshwa na kumilikiwa na chama, kisha chama hicho hicho kinatoa tenda na kujigawia chenyewe, hapa kweli kuna haki?

Hapa sina shaka ni mwanya wa kukwepa kodi na kupewa upendeleo kwa kampuni husika.

Hapa ndipo ulipo uchochoro wa misamaha yenye kutia walakini ambayo tumekuwa tukiishuhudia.

Je, hiyo kampuni ingekuwa ya CHADEMA, CUF au TLP, ingepewa hiyo tenda? Je, huku si CCM kutumia bendera yetu kujinufaisha kwa kujipendelea na kuchota pesa ya miradi yetu bila kustahili?

Hivi pesa ya mradi huu itasimamiwa na nani iwapo mwenye mradi ni chama na serikali yenyewe?

Hii mie naona ni janja na sababu ya kuiibia hazina yetu. Ni aina mpya ya ujambazi na ubadhirifu.

Kuonyesha kuwa huu ni ujambazi wa kitaasisi, hata Mkurugenzi wa TGC-CCM, John Chaggama, alipoulizwa kutaja CCM ina hisa ngapi na za thamani gani kwenye mradi, alikubali kuwa CCM ina masilahi lakini hakutaka kutaja idadi na thamani ya hisa!

Je, sasa CCM imeanzisha sera mpya ya kufanya biashara badala ya siasa? Je, ina kampuni ngapi ambazo bado ni siri na zimeishanufaika na miradi mingapi?

Yaani CCM sasa inaanza kuwa chama cha ajabu!

Pamoja na kuwa na nafasi ya kuchota pesa kutoka hazina yetu kitakavyo kwa miaka zaidi ya arobaini, bado hakijaridhika kiasi cha kujiingiza kwenye kimradi cha shilingi bilioni mbili na ushei?

Hawa Watanzania wa kawaida wenye kampuni zao ndogo watafanya nini na wapi?

Ajabu CCM haitaki kujibu tuhuma hizi za kujipendelea, badala yake inaendelea na ‘dirty business as usual!’ Huu ni uchangudoa wa kiuchumi ambao huwa nausisitiza.

Kama chama chenye vitega uchumi zaidi ya mia, kuanzia maegesho ya magari kwenye viwanja kilivyonyakua, ruzuku ya zaidi ya sh bilioni moja, serikali, nchi na watu wake, hakiwezi kutosheka, basi huu ni ufisi wa hali ya juu.

Kama viongozi wa chama hiki hawatajisafisha haraka na kujitoa kwenye hali hii, tutashindwa kuona hata mantiki ya busara zao.

Watabakia kuwa kikundi hatari kwa mustakabali wa taifa letu. Je, tuendelee kuwaendekeza?

Tamaa ya kumiliki na kujipatia tenda ni ushahidi wa kimazingira (circumstancial evidence), kuwa CCM na serikali yake kwa kuzingatia walichofanya ilipoibuka kashfa ya Chavda, ni washirika wakubwa wa kudhoofisha uchumi wetu.

Kwani nani hajui kuwa kashfa ya Chavda ilikuwa ni dili la baadhi ya viongozi wa wakati ule?

CCM na serikali yake walimtumia Chavda kama mbuzi wa shughuli kufanikisha ujambazi wao.

Hivi ni akili kiasi gani kama Chavda hakuwa wakala wao, mtu anabainika na jinai ya kuhujumu uchumi (economic crime and sabotage), badala ya kumfunga unampa ndege kurudi kwao India! Hii maana yake nini?

Hivi ni nani anaweza kumfumania mtu akizini na mume au mkewe akampa ofa ya tripu kwenda Ngorongoro au Mikumi kuona wanyama? Mbona majambazi wengine walipokamatwa hawakurudishwa Moshi hata Kenya?

Kumbe uovu huu wa kuwatumia mawakala wa Kihindi kuvuruga na kunyonya uchumi wetu unaendelea!

Ndiyo maana hata mkoloni aliyewaleta alifanya hivyo kuwatumia kama mawakala wa kati ili kumfanya Mwafrika aendelee kuwa maskini, ili iwe rahisi kunyonywa na kutawalika.

Bahati mbaya sana na wakoloni wetu wanaendeleza dhambi na laana ile ile ili waweze kutuibia na kututawala watakavyo. Je, tutaendelea na ukondoo huu hadi lini?

Hebu tujiulize. Kama chama chenye kutawala nchi yenye rasilimali lukuki kinaweza kujitoa udhu kwa ajili ya kupata mgawo kutoka kwenye shilingi bilioni mbili, je, chama hiki kinaweza kusimamia madini yetu kwa uadilifu? Huu ndiyo uchochoro mwingine wa kuingia mikataba feki ya madini halafu wahusika wakiguswa, rais anakuwa mstari wa mbele kuwatetea.

Hii ndiyo siri ya nchi inayozalisha madini ya tani na tani kuwa maskini! Kumbe kikulacho ki nguoni mwako!

Kuna uwezekano kuwa hata hao tunaozugwa kuwa ni wawekezaji, wasiwe wawekezaji, bali mawakala au kampuni za CCM na serikali yake.

Nilikuwa nikishangaa kwa nchi kapuku kama yetu kutoa misamaha kwa wawekezaji ambao kimsingi ni watu na pesa zao! Kwanini misamaha hiyo isiwe na masilahi ya CCM?

Anayetilia shaka dhana hii arejee IPTL, Richmond, Net Group na mabalaa mengine. Kila balaa lina kigogo nyuma yake.

Kikwete na Makamba kama kweli chama chenu hakihusiki na uchafu huu na uhujumu wa uchumi wetu, jitokezeni mtupe maelezo.

Simu: 0713260071


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments
  • Comment #1 (Posted by mkojoaji)
    Rating
    Hapana inatia uchungu hakuna zaidi kwa Watanzania wote kuandama na kupinga suala hili kinagaubaga
     
Submit Comment


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.