WATU wasiofahamika, wanaodhaniwa kuwa ni majambazi, wamelipua posta ya Mkoa wa Pwani kwa kutumia baruti kwa nia ya kuiba.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Henry Salewi, alisema tukio hilo limetokea juzi, saa 9 usiku katika eno la Shirika la Elimu Kibaha.
Alisema watu hao walifika posta wakiwa na bastola ambayo haikuweza kufahamika ni ya aina gani, kisha kuvunja ukuta kwa kutumia shoka.
“Wakati watu hao wakivunja, walinzi walikimbia na kujificha kutokana na kutokuwa na silaha na baada ya kusikia baruti ikilipuliwa… Walijificha kwa woga na kuwafanya watu hao kufanya walivyotaka wakiwa na dhumuni la kuvunja kifaa cha kuhifadhia fedha,” alisema Kamanda Salewi.
Kamanda huyo alisema polisi wa Kituo cha Wilaya ya Kibaha, walifika na kuwakurupusha watu hao ambao walitaka kulipua baruti ya pili.
Polisi walipofika eneo la tukio, walianza kurushiana risasi na watu hao ambao walifanikiwa kutokomea kusikojulikana.
Inakadiriwa kuwa, kwenye kifaa cha kuhifadhia fedha kulikuwa na zaidi ya sh milioni tatu ambapo posta hiyo ni wakala wa benki, hivyo watu hao walikuwa na lengo la kuiba fedha zilizokuwepo.
Polisi wanaendelea na uchunguzi juu ya tukio hilo.