WAKATI kikao cha Bunge la Muungano kinaanza leo mjini Dodoma, bajeti ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa ajili ya mwaka wa fedha wa 2007/08 inatarajiwa kusomwa Juni 20, mwaka huu.
Kwa mujibu wa taarifa iliyopatikana bungeni kupitia kwa ofisa habari mkuu wa Bunge, Ernest Zulu, baada ya ufunguzi wa shughuli za Bunge hilo la bajeti, siku mbili za mwanzo zitatawaliwa na maswali na majibu.
Zulu alisema kuwa, hotuba ya bajeti ya serikali kwa mwaka ujao wa fedha, itawasilishwa na kusomwa bungeni Alhamisi wiki hii na Waziri wa Fedha, Zakia Meghji.
Zulu alibainisha kuwa, kabla ya kusomwa kwa bajeti hiyo, Waziri wa Mipango, Uchumi na Uwezeshaji, Dk. Juma Ngasongwa, atatoa hotuba kuhusu hali ya uchumi wa nchi bungeni hapo.
Baada ya kutolewa kwa taarifa hiyo ya Uchumi wa nchi siku ya Ijumaa itatumika kutafakari taarifa hiyo pamoja na hotuba ya bajeti ya serikali kwa ajili ya kuzijadili.
Hotuba ya Waziri wa Fedha na taarifa hiyo ya uchumi wa nchi, zitajadiliwa kwa muda wa siku tano kuanzia Jumatatu ijayo kabla ya wizara mbalimbali kuanza kuwasilisha makadirio ya bajeti zao kwa mwaka wa fedha 2007/2008.
Juni 25 hadi 29, kutakuwa na mjadala wa siku tano wa hotuba ya Waziri Mkuu, Edward Lowassa, juu ya utekelezaji wa shughuli za serikali katika mwaka wa fedha unaomalizika na matarajio ya serikali kwa mwaka wa fedha unaofuata pamoja na Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa.
Kwa mujibu wa ratiba, baada ya mjadala huo, bunge litaanza kujadili utekelezaji wa wizara moja moja na kupitisha makadirio ya kila wizara.
Kikao hicho cha Bunge kitadumu kwa muda wa miezi miwili hadi Agosti 10, mwaka huu ambapo kila siku wastani wa maswali 10 yataulizwa na kupatiwa majibu.
Kutoka Zanzibar, habari zinapasha kuwa, kikao cha bajeti kitaanza Juni 20, siku ambayo bajeti ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibr (SMZ) itasomwa katika Baraza hilo.
Katibu wa Baraza hilo, Ibrahim Mzee, alisema jana kuwa, maandalizi ya kikao hicho yamekamilika, ikiwemo wajumbe wote kutaarifiwa.
“Tunatarajia kusoma bajeti Juni 20 na wajumbe wote wamekwisha taarifiwa kuhusu kikao hicho,” alisema Katibu wa Barazal hilo.
Wajumbe wa CCM na wale wa CUF kutoka kisiwani Pemba, tayari wameanza kuonekana katika maeneo mbalimbali ya Zanzibar, kwa ajili ya maandalizi ya kikao hicho.
Akitoa muhtasari wa bajeti hiyo, Waziri wa Nchi Afisi ya Rais anayeshughulikia Fedha na Uchumi, Dk. Mwinyihaji Makame Mwadini, alisema serikali inatarajia kutumia sh bilioni 279 katika mpango wa maendeleo na kazi za kawaida.
Alisema wananchi wa Zanzibar watarajie kushuka kwa mfumko wa bei kutokana na mipango ya serikali iliyoandaliwa, kuhakikisha wananchi wanapata unafuu. Alisema matarajio ni kuwa mfumuko wa bei utashuka kutoka asilimia 11 hadi chini ya asilimia 10.
Hata hivyo, alisema katika mwaka ujao wa fedha, serikali inatarajia kuzibana taasisi za ukusanyaji mapato ili kuona zinakusanya kodi ipasavyo.
Alieleza kwamba, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) itatakiwa kuongeza uwezo wa ukusanyaji mapato kwa asilimia 63, ikilinganishwa na mwaka uliopita, ambapo Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB) ilitakiwa kuongeza uwezo wa kukusanya mapato kwa asilimia 28.
Waziri huyo alisema, serikali imeamua kuwajengea uwezo watendaji, ikiwemo kuwapatia mafunzo yatakayowasaidia kupambana na vitendo vya ukwepaji kodi.
Hata hivyo, aliwataka wananchi wa Zanzibar kurudisha utamaduni wa kupanda minazi kwa wingi kwa vile zao hilo bado lina nafasi kubwa katika kuinua uchumi wa visiwani.