MKURUGENZI wa Makosa ya Jinai (DPP), amewaachia huru watuhumiwa watatu, waliokuwa na tuhuma za kughushi na kutoa kibali bandia cha ujenzi wa maghorofa ya Masaki, jijini Dar es Salaam.
Walioachiwa chini ya kifungu cha 91(1) cha sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai, ni Robert Sinde Warioba (46), mkaguzi wa majengo Manispaa ya Kinondoni, Joyce Mwamlima (39) na Diana Peter (44), watunza kumbukumbu za halmashauri hiyo. Kesi hiyo ilikuwa inawakabili watuhumiwa watano.
Watu hao waliachiwa huru baada ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) kuiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, kuondoa mashitaka dhidi yao.
Mwendesha mashitaka, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Charles Kenyella, alitoa ombi hilo mbele ya Hakimu Mkazi, Saidi Msuya wa Mahakama ya Kisutu, hali iliyowafanya walioachiwa huru kusali kabla ya kutoka nje ya mahakama.
Katika kesi hiyo, Mhandisi wa Manispaa ya Kinondoni, Olimpia Kundi (38) na mfanyabishara anayemiliki majengo hayo, Ramzanali Hirji (42), walionekana kuwa wana kesi ya kujibu kuhusu kibali bandia cha ujenzi.
Baada ya ombi hilo kukubaliwa, Kenyella aliwasomea mashitaka watuhumiwa hao na kudai kuwa walikula njama na kughushi kibali cha ujenzi namba 00000600 kilichotolewa Agosti 20, 2004 na Manispaa ya Kinondoni, kuonyesha kuwa ni halali kwa ujenzi.
Aidha, Olimpia anakabiliwa na tuhuma nyingine za kuharibu ushahidi. Ilidaiwa na Kamishna Kenyella kuwa, kati ya Agosti 2004 na Mei 2006, kwenye ofisi za Manispaa ya Kinondoni, kwa makusudi, mtuhumiwa huyo aliharibu baadhi ya nyaraka zilizohitajika mahakamani na kuwezesha zisipatikane wakati wa ushahidi.
Kamishna Kenyella, alidai mahakamani hapo kuwa, Hirji alitoa ushahidi wa uongo katika kesi namba 66/2006 iliyopo Mahakamana Kuu Kitengo cha Ardhi, ambapo Kampuni ya ujenzi ya Empire ni mlalamikaji dhidi ya Manispaa ya Kinondoni.
Ilidaiwa mahakamani hapo kuwa, kati ya Mei 17, mwaka jana na Juni 6, mwaka huu, mtuhumiwa huyo akiwa kama shahidi, alitoa maelezo ya uongo, kwamba alipokea kibali namba 00000600 kutoka Manispaa ya Kinondoni kwa ajili ya ujenzi wa majengo mawili ya ghorofa nane kila moja na jingine la ghorofa tatu, eneo la Masaki Dar es Salaam.
Baada ya maelezo hayo, watuhumiwa wote walikana kosa. Upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na hakimu aliiahirisha hadi Julai 17 itakapoanza kusikilizwa.