CHAMA cha Wananchi (CUF), kimesema kauli iliyotolewa hivi karibuni kisiwani Pemba na Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Luteni Yusuf Makamba, imeharibu na kuchafua hali ya hewa kisiasa Visiwani Zanzibar.
CUF pia imesema kufuatia kauli hiyo ya Makamba, itachukua muda mrefu zaidi kurejesha katika ya hali ya kawaida mazungumzo yanayoendelea baina yake na CCM.
Kauli hiyo ilitolewa na kiongozi wa CUF katika mazungumzo hayo, ambaye pia ni kiongozi wa kambi ya upinzani bungeni, Hamad Rashid, wakati alipozungumza na gazeti hili mwishoni mwa wiki.
Rashid alikuwa akizungumza na mwandishi wa habari hizi aliyetaka kujua mchakato wa kisiasa unaoendelea visiwani Zanzibar na hali ya mambo baada ya ziara ya Makamba kisiwani Pemba, hivi karibuni.
“Kwa kweli wanachama wetu wamesikitishwa na kauli ya Katibu Mkuu wa CCM, na wameleta maoni yao kuwa CUF ijitoe katika mazungumzo yanayoendelea,” alisema Rashid.
Rashid aliongeza kwamba, CUF imejitahidi kutuliza munkari wa wanachama wake kwa kuwataka wavute subira, na kuwaamini kwamba ni viongozi wao wanaostahili kusikilizwa.
Alisema kimsingi, ziara ya Makamba huko Pemba, mwezi uliopita haikuwa na maana kwani haikueleza kile ambacho wananchi walitarajia katika mazungumzo yanayoendelea, badala yake alitumia muda wake mrefu kuibeza CUF na kutengeneza fitina.
Kwa msingi huo, Rashidi alisema kwamba CUF bado inaamini umuhimu wa kuwapo kwa mchakato wa mazungumzo hayo, hivyo iliwasiliana na CCM kujua kinachoendelea na matamshi ya Makamba.
“Kama ni kujitoa katika mazungumzo ni maamuzi yanayopaswa kuamuliwa na Baraza Kuu la Uongozi la CUF, na lolote linaweza kutokea, ama kuendelea na mazungumzo ama kujitoa,” alisema Rashid.
Alisema yeye binafsi kama mbunge kutoka Pemba, kiongozi mwandamizi wa CUF na sehemu ya mazungumzo hayo, hakubaliani na kauli za Makamba, na kushindwa kuamini kama zinaweza kutolewa na kiongozi mkubwa kama yeye.
“Lakini tunadhani hiyo ndiyo rangi ya CCM, na sisi mara zote tupo makini kusikiliza wao wanasema nini, lakini kwa hili tunadhani (Makamba) amekurupuka kutoa kauli bila kufanya utafiti.
“Kauli zake hazionyeshi ukomavu na nia ya wazi ya CCM kama chama kinachotawala nchi, kushughulikia mgogoro wa kisiasa huko Zanzibar, lakini pia wanachama wetu wanaamini alifanya ziara ile kwa lengo la kubomoa,” alisema.
Hata hivyo, Rashid alisema kwamba CUF haijapata athari zozote baada ya ziara hiyo, kama ambavyo yeye mwenyewe Makamba alivyoueleza umma kuwa amefanikiwa kukisambaratisha chama cha CUF.
“Makamba baada ya kurejea katika ziara ya Zanzibar, alisema kwamba amekivuruga chama cha CUF Pemba na kuiteka nyara ngome yetu, sisi hatujaona hilo, lakini mashaka yetu ni matamshi, kama yana nia gani katika mazungumzo yanayoendelea.
“CUF ni chama imara, hatuna tatizo kabisa, tunajua kile tunachokifanya na wala maneno ya Makamba hayatutishi, shida yetu ni je, huo ndio msimamo wa CCM?” alihoji.