Na Mussa Juma, Arusha
HATIMAYE Chama cha Mapinduzi (CCM), kimetoa waraka kwa viongozi wa chama hicho wa mikoa kuwazuia wabunge na madiwani kugombea nafasi za utendaji wa kila siku ndani
ya chama hicho.
Habari za uhakika toka ndani ya chama hicho, ambazo zimethibitishwa na Katibu wa CCM Mkoa wa Arusha, Mohamed Mbonde, zimeeleza kuwa CCM makao makuu imetuma waraka kwa makatibu wote wa mikoa kuwakumbushia suala hilo.
"Ni kweli kuna waraka huo, lakini sio wa kwanza, hili suala lipo wazi, madiwani na wabunge wanahesabika kuwa wana majukumu ya kazi ya kila siku hivyo kugombea na kupitishwa ni mpaka wapate kibali maalum," alisema Mbonde.
Katibu huyo alisema katika uchaguzi uliopita, kulikuwapo na viongozi kadhaa ambao
waliruhusiwa kugombea nafasi nyingine, hasa baada ya kutolewa mapendekezo katika
vikao vya CCM na baadaye kukubaliwa na Kamati Kuu ya chama.
Hata hivyo, baadhi ya wabunge wa chama hicho tayari wameomba nyadhifa mbalimbali ambazo ni za utendaji wa kila siku ikiwamo, katibu mwenezi, uenyekiti wa mkoa na wilaya , uweka hazina na kwamba kuna mapendekezo ya kuwazuia hata kugombea ujumbe wa NEC.
Tayari wagombea kadhaa wametishia kukata rufani iwapo wagombea wenzao wenye nyadhifa za ubunge na udiwani, wataachiwa kugombea nafasi za utendaji katika chama.
Haieleweki hasa waraka huo unalenga nafasi zipi hasa, kwani mtendaji mkuu katika Chama Cha Mapinduzi, ambaye ni Katibu Mkuu wa Chama, Yusuf Makamba ni Mbunge. Hata Katibu wa Idara ya Uenezi makao makuu, Aggrey Mwanri pia ni Mbunge. Wakati Mwanri ni Mbunge wa Jimbo la Siha lililopo Mkoa wa Kilimanjaro, Rostam Aziz ambaye ni Mweka Hazina wa CCM pia ni Mbunge wa Igunga na Makamba ni Mbunge wa Kuteuliwa na Rais.
"Kanuni hii ipo wazi, lakini tunaona kuna viongozi wetu wana nafasi kubwa na
wana majukumu ya kila siku lakini wamechukua fomu, hivyo tunaomba CCM kuwa makini na kurejesha majina yao," alisema mgombe mmoja wa Uenyekiti wa CCM Mkoa wa Arusha.
Baadhi ya wagombea hao (majina yanahifadhiwa) katika nafasi za uenyekiti wa mikoa
na wilaya, ujumbe wa halmashauri kuu (NEC) na nafasi ya katibu uenezi, wameeleza kuwa kama suala hilo lisipowekwa bayana, ni wazi watu wachache watakuwa na madaraka makubwa katika sehemu mbalimbali za maamuzi ya serikali na CCM.
Wanachama zaidi ya 500 wamejitokeza kuwania nafasi mbalimbali za CCM kutoka wilaya sita za Mkoa wa Arusha. Ukiacha mbalimbali malalamiko hayo mapya, wakati wagombea wakielekea katika uchaguzi, kumekuwa na madai ya baadhi yao kutumia rushwa ili kupata ushindi.
Hata hivyo, Makamba aliwataka waandishi wa habari, walioripoti matukio ya rushwa, kuwataja wana CCM wanaojihusisha na vitendo hivyo katika uchaguzi badala ya kuwahifadhi, akisema hatua hiyo itakisaidia chama na Taasisi ya Kuzuia Rushwa (PCB) kuwachukulia hatua zinazohusika.
“Chama hiki hakiongozwi na wala rushwa, utaratibu wa vyombo vya habari kusema majina (ya wala rushwa) tunayo, ni unafiki. Tupeni majina, tutachukua hatua. Usiandike jina tunalo, we lilete tu,” alisema Makamba alipozungumza na waandishi wa habari wiki iliyopita.
Alisema mwana CCM yeyote anayeendesha fitina katika uchaguzi, amepoteza sifa ya kuwa mwanachama wa chama hicho na pia mwanachama yeyote anayetoa rushwa, jina lake halitarudi kwa wajumbe kwa ajili ya kupigiwa kura.
Katibu Mkuu huyo wa CCM alisema hali katika chama hicho ni shwari na kwamba wanaodai kinyume chake, ni watu walioshindwa katika chaguzi za chama hicho zilizopita za mashina na matawi ambao aliwafananisha na mbaazi ambazo alisema “zinapokosa maua husingizia jua”.
Lakini wakati Makamba akisema hali ni shwari katika chama chake, habari za rushwa, fitna na majungu zimekuwa zikiripotiwa kutoka maeneo mbalimbali katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi
Mkoani Mwanza, wajumbe wanaowania chama hicho kuwateue kuuwakilisha katika Halmashauri Kuu, wamekuwa wakituhumiana kufanyiana fitina na majungu pamoja na kutembeza rushwa, huku mmoja wao akionya kuwa hali hiyo inaweza kukiacha chama katika makovu makubwa mara baada ya uchaguzi kumalizika.
Katibu wa CCM Mkoa, Mwangi Rajab Kundya, alikaririwa na gazeti hili wiki iliyopita akisema amepata malalamiko kutoka kwa wagombea na kwamba ameiomba Taasisi ya Kuzuia Rushwa (PCB) kuwafuatilia wagombea wanaotoa rushwa na kuwachukulia hatua za kisheria.