WAKATI wananchi wakianza kusahau kero za ujambazi, watu wanaodhaniwa kuwa ni majambazi, wamepora kiasi kikubwa cha fedha baada ya kuvunja mashine ya kuchukulia fedha (ATM) ya Benki ya NBC katika kituo cha mafuta cha Magomeni Mapipa, kilicho katika makutano ya barabara za Kawawa na Morogoro, Dar es Salaam.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Jamal Rwambow, alithibitisha jana kutokea kwa wizi huo, ingawa hakuweza kutoa maelezo zaidi kuhusu kiasi cha fedha kilichoibwa.
“Ni kweli nimepata hizo taarifa, kuna wizi umetokea, lakini maelezo zaidi nitayatoa baada ya kuwapata wahusika wa benki,” alisema.
Hata hivyo, alieleza kwamba, watu hao walijipenyeza hadi katika mashine hiyo kwa kupitia mlango wa nyuma kati ya hoteli ya Travertine na kituo hicho cha mafuta, kisha wakaingia chumba cha ATM na kuilipua kwa kitu kinachodhaniwa kuwa ni baruti.
“Kesho nitatoa taarifa kamili, nipe muda,” alisema Kamanda Rwambow aliyetoa ushirikiano mkubwa baada ya kutakiwa kuthibitisha wizi huo.
Ingawa hakuwa na maelezo ya kutosha, habari zilizotufikia kabla ya kuthibitishwa na Kamanda Rwambow zilisema kwamba, majambazi hao wameiba kiasi cha kati ya sh milioni 40 na 50.
Wimbi la ujambazi lililokuwa linatishia usalama wa raia na mali zao nchini, lilionekana kupunguza kasi kuanzia mwanzoni mwa mwaka huu, kutokana na mikakati thabiti ya Jeshi la Polisi.
Hata hivyo, ili kujaribu kumaliza kabisa tatizo hilo, Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP), Said Mwema, ameanzisha kitengo kipya cha Operesheni Maalum, ambacho mkuu wake ni Kamishna Msaidizi Mwandamizi, Venance Tossi. Kabla ya uteuzi huo, Tossi alikuwa Kamanda wa Mkoa wa Kagera, alikokaa kwa muda mfupi, lakini akifanya mambo makubwa katika kupambana na uhalifu mkoani humo.