KIKIWA kinapata ruzuku ya karibu sh bilioni moja kila mwezi, Chama Cha Mapinduzi (CCM), sasa kimeamua kujiingiza rasmi katika biashara, baada ya kubainika kwa mpango wake wa kunyemelea mradi wenye thamani ya mabilioni ya dola za kimarekani.
Habari zilizoifikia Tanzania Daima kwa miezi kadhaa sasa, zilieleza kuwa, CCM kupitia kampuni yake ya Tanzania Green Ltd, ina hisa katika mradi wa ujenzi wa bomba la kusafirisha mafuta pamoja na bidhaa zinazotokana na mafuta kutoka Dar es Salaam kwenda mikoa ya Mwanza na Kigoma pamoja na nchi jirani zinazopakana na mikoa hiyo.
Mradi huo una thamani ya dola za Marekani bilioni 2.6 ambazo ni zaidi ya sh trilioni 2.8 na CCM imekwishakiri hadharani kuwa na hisa katika mradi huo, ambao utekelezaji wake ulitarajiwa kusainiwa Machi, mwaka huu.
Kuibuka kwa Kampuni ya Tanzania Green Ltd ya CCM na kueleza wazi kuwa na mkono wake katika mradi huo, kumezua utata baada ya kampuni tatu za ndani na nje ya nchi zilizoshindwa katika zabuni hiyo, kupanga kufungua kesi mahakamani kuizuia serikali kuanza utekelezaji wa mradi huo.
Taarifa zinaeleza kuwa, mradi huu wa usafirishaji mafuta na ujenzi wa bomba la mafuta, ambao ulianzishwa miaka 10 iliyopita, sasa umetolewa rasmi kwa kampuni ya ndani yenye ubia na wawekezaji wa nje wa Qatar Oil, Noor Oil na Industrial Technology Ltd ambayo pia ina ubia na Roneg AG ya Ujerumani na Stroytransgaz na Promoteurs ya Urusi.
Inadaiwa kuwa, kampuni zilizoshindwa katika tenda hiyo, hazikuridhishwa na mchakato wa utolewaji wa mradi huo mkubwa kwa kampuni inayomilikiwa na chama kilichoko madarakani.
Mwenyekiti wa Kampuni ya Africommerce International, Elisante Muro, amekaririwa na baadhi ya vyombo vya habari akieleza kuwa, kampuni yake ndiyo iliyoasisi mradi huo, ambao sasa unadaiwa kuzawadiwa kwa CCM.
Muro alisema kampuni yake haikuridhishwa na jinsi tenda hiyo ilivyotolewa na kueleza zaidi kwamba, Bunge la Jamhuri ya Muungano liliithibitisha kampuni yake kuendesha mradi huo kupitia barua yenye kumbukumbu namba BC. 50/155/05 ya mwaka 2005.
Alisema kwamba, Bunge liliridhia mradi huo utekelezwe na Kampuni ya Africommerce International kwa kushirikiana na kampuni ya gesi na mabomba ya Marekani, EL Paso ya Houston, Texas na kampuni mshauri wa kifedha, Fieldstone Capital Group ya New York.
Kinyume chake, serikali iliutoa mradi huo kwa Kampuni ya Qatar’s Noor Oil na Industrial Technology Ltd ya Qatar ambayo inaongoza ubia wa kampuni tatu kutoka Urusi, Ujerumani na Tanzania kujenga na kusimamia mradi huo, ambao unahusisha pia ujenzi wa mtambo wa kisasa wa usafishaji mafuta na bomba la kusafirisha mafuta.
Habari zaidi zinaeleza kuwa, hatua hiyo ya serikali iliifanya Africommerce International Ltd na washirika wake; Fieldstone Capital Group na El Paso Corporation ya Marekani, kuungana kutishia kufungua kesi kudai fidia kwa hasara iliyopatikana kutokana na gharama za uasisi na promosheni za mradi huo zinazofikia dola milioni 12.8.
Zinaeleza taarifa kuwa, wawekezaji hao kupitia wenzao wa Tanzania Africommerce International Ltd, wamekwishaieleza serikali nia yao ya kufungua kesi mahakamani, kuzuia utekelezani wa mpango huo iwapo haitatimiza masharti ya waasisi wa mradi huo.
Kampuni ya Tanzania Green inadaiwa kuhusika katika miradi mikubwa ya aina hii kwa mara ya pili, awali ilikuwa miongoni mwa wawezekaji na wabia saba waliorodheshwa katika mauzo ya asilimia 49 za hisa za Benki ya NMB.
Taarifa zaidi zinaeleza kuwa, Tanzania Green ilikuwa mjumbe katika ubia wa mkakati wa maendeleo Tanzania, ambao harakati zake ziligonga mwamba.
Kwa mujibu wa habari zilizowahi kuchapishwa na gazeti la The East-African, mapema mwaka huu, kampuni hiyo inayomilikiwa na CCM, ilikaribisha ujumbe mzito kutoka Bunge la Urusi, Duma kuja nchini kukutana na maofisa waandamizi wa CCM na serikali mjini Shinyanga wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu mwaka 2005.
CCM ilishinda uchaguzi huo kwa kishindo.
Mmoja wa maofisa hao wa Urusi waliokuwa katika msafara huo, ni mshauri wa masuala ya mafuta na uchumi wa Rais Vladimir Putin.
Haifahamiki kama ziara ya ujumbe huo ilihusiana na shughuli za uchaguzi mkuu wa mwaka 2005 au ilikuwa na lengo la kuanzisha ushirika wa kibiashara kati ya CCM na chama kinachotawala nchini Urusi.