FITINA, majungu na uongo, vyenye lengo la kumchafua Rais Jakaya Kikwete, vimeanza kusambazwa mkoani hapa na kundi la watu wanaodaiwa kuwa wanamtandao waliosahauliwa.
Kundi hilo linadaiwa kuundwa na watu wanaodhaniwa kuwa ‘wanamtandao’ waliosahaulika, wengi kutoka Dar es Salaam na visiwani Zanzibar. Inadaiwa baadhi kuwa ni watu mashuhuri nchini.
Baadhi ya wanachama wa kundi hilo, hivi sasa wako mkoani hapa wakiwa wamepiga kambi kwa zaidi ya wiki moja, wakizunguka sehemu mbalimbali zenye mikusanyiko ya watu, wakieleza jinsi Rais Kikwete asivyowapenda wananchi wa Mbeya.
Uvumi unaoenezwa sasa na kundi hilo kwa wakazi wa mjini Mbeya ni kwamba, hasira za Rais Kikwete dhidi ya Wanambeya zinatokana na kuendelea kumuunga mkono Profesa Mark Mwandosya, ambaye alikuwa mmoja wa washindani wake wakubwa katika kinyang’anyiro cha kutafuta mgombea urais wa CCM mwaka 2005.
Kwamba kwa sababu ya hasira alizonazo, aliamua kuahirisha ziara yake ya Mkoa wa Mbeya, iliyokuwa ifanyike mapema mwezi huu baada ya kuelezwa na wasaidizi wake kuwa, wanachana wa CCM wa hapa, sasa wameungana kulipinga kundi la wanamtandao, ambalo limeweka mgombea wake katika nafasi ya Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa, ambayo inawaniwa pia na Prof. Mwandosya.
Fitina na majungu zaidi yanayosambazwa na kundi hilo, vinamgusa pia Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, John Mwakipesile anayeelezwa kuwa swahiba wa Rais Kikwete, ambaye licha ya kushindwa katika kura za maoni za ubunge mwaka 2005, aliinuliwa na Rais kikwete na kupewa wadhifa wa Mkuu wa Mkoa.
Zinawaonya wapinzani wa Mwakipesile kuacha kumuandama kwa maneno na kumshitaki kwa viongozi wa juu serikalini, kwa sababu jambo hilo linazidisha hasira za rais dhidi ya watu wa Mbeya, ambao wanaonekana kutofautiana na swahiba wake.
Kundi hilo limekuwa likionya kuwa, kitendo chochote cha kutofautiana na Mwakipesile kitazidi kuwasogeza mbali na serikali, ambayo iko katika mikakati ya kuhakikisha Prof. Mwandosya anaangushwa na mgombea kijana, Tom Mwang’onda, anayedaiwa kuungwa mkono na kundi la wanamtandao, katika kuwania ujumbe wa NEC.
Mwang’onda, mtoto wa mkurugenzi wa zamani wa Usalama wa Taifa, Apson Mwang’onda, anaelezwa kuwa mmoja wa wanamtandao walioshindwa kuteuliwa kuwania ubunge katika uchaguzi wa 2005, lakini Rais Kikwete alimteua haraka kuwa mbunge kwa sababu ni mmoja wa wapambanaji maarufu ndani ya mtandao wanaotumainiwa na rais katika kuwashughulikia wapinzani wake, Prof. Mwandosya akiwa mmoja wao.
Hata hivyo, Mwang’onda juzi alizungumza na Tanzania Daima na kueleza kuwa, madai yanayoelekezwa kwake kuwa amechukua fomu za kuomba kuteuliwa kuwa mjumbe wa NEC kupitia Mkoa wa Mbeya, nafasi inayoshikiliwa na Prof. Mwandosya, ikiwa ni katika hatua za kumshughukia, si ya kweli.
Mwang’onda alisema aliamua kuchukua fomu akiamini kuwa kwa ngazi aliyonayo Prof. Mwandosya ambaye alifikia hatua ya kuwa mgombea urais ndani ya chama na kuwa mmoja wa wagombea bora, hawezi kujitosa kuwania ujumbe wa NEC kupitia mkoani, bali kupitia taifa.
Alisema uvumi unaosambazwa kuwa kugombea kwake kunaungwa mkono na wanamtandao, ni majungu na fitina za kisiasa zenye lengo la kuharibu nia yake na kuwachanganya wananchi wa Mbeya ili washindwe kumchagua mwakilishi wanayemtaka na atakayewafaa katika kipindi hiki.
Fitina zaidi zinazosambazwa na kundi hilo, zinaeleza kuwa, uamuzi wa Rais Kikwete kuahirisha ziara yake Mbeya, ulilenga kuepuka kudhoofisha operesheni ya wanamtandao ya kumng’oa Prof. Mwandosya katika ujumbe wa NEC ili kummaliza kisiasa.
Zinaeleza kuwa wanusaji wa Rais Kikwete waligundua mapema kuwa kulikuwa na mpango wa kumtaka awe msuluhishi katika mgogoro wa kisiasa uliopo sasa mkoani Mbeya, ambao umeanza kuigawa CCM katika makundi yenye mwelekeo wa kikabila na kiukoo.
Fitina hizo zinaendelea kudai kuwa, Prof. Mwandosya ‘hanogi’ kwa Rais Kikwete, ingawa ameteuliwa katika Baraza la Mawaziri, akiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira).
Habari hizo za uzushi zinaeleza kuwa, tofauti na Rais mstaafu Benjamin Mkapa, ambaye alimshinda Rais Kikwete katika uchaguzi wa ndani ya chama wa kuwania kuteuliwa kuwa mgombea urais mwaka 1995, lakini alipoingia madarakani, alimteua kuwa Waziri wa Mambo ya Nje, Kikwete ameamua kumpa Prof. Mwandosya kazi ya kushughulikia mazingira ambayo haimpi nafasi ya kusikika kwa urahisi.
Prof. Mwandosya anadaiwa pia kuwa, sasa anafikiria kujitoa katika kinyang’anyiro cha ujumbe wa NEC kupitia Mkoa wa Mbeya baada ya kubaini kuwa rais hamuungi mkono na amemuwekea mtu maalumu kutoka ndani ya mtandao kupambana naye.
Hata hivyo, uvumi huo ambao umesambaa sehemu mbalimbali za mjini Mbeya, umekanushwa na watu wa karibu na Prof. Mwandosya, kuwa una lengo la kuwakatisha tamaa wanaomuunga mkono na pia kukwamisha jitihada zake za kukitetea kiti hicho na pia kutoa nafasi zaidi kwa anayedaiwa kuwa mpinzani wake mkuu, Tom Mwang’onda.
“Hizo taarifa hazina ukweli wowote, hana sababu ya kuwaacha wana Mbeya ambao wanampenda, hizo ni mbinu za kuwachanganya watu, waache wahangaike,” alisema mmoja wa watu wa karibu na Prof. Mwandosya.
Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa, kundi hilo limepiga kambi eneo la Uyole, katika hoteli moja maarufu iliyopo eneo hilo.
Taarifa ya Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mbeya, Julius Nswila kwa gazeti hili kuhusu kuahirishwa kwa ziara ya Rais Kikwete mkoani Mbeya, ilieleza kuwa, hakuhusiani na tuhuma zinazotolewa.
Nswila alisema kuwa, ziara hiyo iliahirishwa kutokana na majukumu mengi aliyonayo Rais Kikwete, na kwamba hawezi kuwatenga watu wa Mbeya kwa kuwa ni sehemu ya utawala wake.