WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Ikulu, anayeshughulikia fedha na uchumi Zanzibar, Dk. Mwinyihaji Makame, amesema watumishi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) watarajie kunusa tumbaku kwa kupandishiwa mishahara yao katika mwaka ujao wa fedha.
Dk. Makame, alisema hayo jana wakati akitoa muelekeo wa bajeti ya mwaka wa fedha wa 2007/2008 ofisini kwake, Vuga, mjini hapa.
Alisema serikali imeamua kuongeza viwango vipya vya mishahara, ili kuwapunguzia ukali wa maisha watumishi wake.
Watumishi wa serikali hadi sasa wanalipwa kima cha chini sh 60,000, kiwango ambacho kinalalamikiwa kuwa hakilingani na mahitaji halisi.
“Tunatarajia kuwanukisha tumbaku kwa kurekebisha viwango vya mishahara,” alisema Dk. Makame. Hata hivyo, hakusema ni kiwango gani kitaongezwa.
Dk. Makame alisema wananchi wa Zanziabr katika mwaka ujao wa fedha, watarajie unafuu wa maisha kwa vile mfumko wa bei katika soko la ndani utashuka kutoka asilimia 11.4 hadi chini ya asilimia 10.
Alisema pato la mwananchi wa kawaida linatarajiwa kuongezeka kutoka dola 320 za Marekani mpaka 370, kutokana na mipango iliyopangwa na serikali, ya kupunguza umasikini kwa wananchi wa Zanzibar.
Aidha, alisema pato la taifa katika mwaka ujao wa fedha, linatarajiwa kuongezeka hadi kufikia kiwango cha asilimia 6.6 kutoka asilimia 6.1 mwaka 2006.
“Utekelezaji wa malengo ya uchumi utakwenda sambamba na utekelezaji wa Mpango wa Kupunguza Umasikini Zanzibar (MKUZA), hasa kwa vile lengo letu ni kuwa na uchumi unaomgusa mwananchi,” alisema Waziri Makame.
Alisema serikali inatarajiwa kutumia sh bilioni 279 katika mwaka ujao wa fedha kwa ajili ya kazi za kawaida na maendeleo kwa wananchi wa Unguja na Pemba.
Hata hivyo, alisema deni la serikali bado ni tatizo kwa vile limefikia sh bilioni 200 sawa na asilimia 39.1 ya pato la taifa katika mwaka uliopita ambapo deni la nje lilifikia sh bilioni 130.9.
Hata hivyo, alisema serikali ili iweze kufikia malengo yake, imeweka mikakati mipya ya ukusanyaji wa kodi, ili kuhakikisha Mamlaka ya Kodi Tanzania (TRA) inaongeza ukusanyaji wa mapato kwa asilimia 63 kutoka kiwango kilichopangwa mwaka uliopita.
Aidha, Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB), italazimika kuongeza kwa asilimia 28 ikilinganishwa na lengo la mwaka uliopita.
“Ongezeko hili katika mapato litatokana na kuimarika kwa taratibu za ukusanyaji, kujengewa uwezo watendaji, kuziba mianya ya uvujaji wa mapato na kudhibiti mapato ya sekta ya utalii,” alisema Dk. Makame.
Alisema bajeti ya mwaka huu inazingatia maeneo muhimu ya kiuchumi, hasa katika sekta ya elimu ya juu, kilimo, afya pamoja na uimarishaji wa sekta ya biashara na utalii.
“Bajeti ya mwaka huu ni ya watu, inalenga kupunguza umasikini, na inalenga kuwajengea watu ujuzi na uwezo wa kazi, ili kuwaongezea fursa ya kujiajiri na kuajiriwa,” alisema Dk. Makame.
Alisema bajeti ya mwaka huu imepata baraka kutoka sekta mbalimbali binafsi, kwa vile zimeshirikishwa katika kuandaa, ikiwemo Jumuiya ya Uwekezaji (ZAT), Jumuiya ya Wafanyaishara Zanzibar, jumuiya zisizo za kiserikali, taasisi za elimu ya juu na Serikali ya Muungano.
“Hata kaka zetu wa Serikali ya Muungano nao tumeshirikiana nao pamoja na washiriki wa maendeleo juu ya misaada,” alisema Waziri Makame.
Hata hivyo, alisema serikali katika mwaka wa fedha itazingatia suala la kuimarisha uwanja wa ndege, bandari pamoja na miundombinu na maeneo yenye mchango mkubwa katika pato la taifa.
Aidha, alisema mchango wa serikali kwa kazi za maendeleo utaongezeka kwa asilimia 84.63 mwaka ujao wa fedha.
Viongozi wengine waliohudhuria mkutano huo ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Uchumi Zanzibar, Khamis Mussa na Naibu katibu wake, Joseph Meza.