Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Bandari Dar es Salaam kuwanufaisha waagizaji
Bandari Dar es Salaam kuwanufaisha waagizaji
By Habari Tanzania | Published  06/9/2007 | Habari za Kitaifa | Unrated
na Mwandishi Wetu


SERIKALI imekisikia kilio cha waagizaji wa bidhaa wanaotumia Bandari ya Dar es Salaam, kwa kuanzisha taratibu nafuu kadhaa mpya zitakaomaliza urasimu uliokuwa ukisababisha msongamano wa muda mrefu.

Taratibu hizo mpya zinazotarajiwa kuanza kutumika katika mwaka ujao wa fedha unaoanza mwezi ujao, zitawanufaisha waagizaji wa magari, wawekezaji waliosajiliwa na Kituo cha Uwekezaji nchini (TIC) na walipa kodi wenye rekodi nzuri.

Hali hiyo ilibainishwa na Waziri wa Fedha, Zakia Meghji wakati alipokuwa akiwasilisha mwelekeo wa bajeti ijayo kwa wajumbe wa Kamati ya Fedha na Uchumi ya Bunge.

Chini ya taratibu hizo mpya, Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) kuanzia kipindi hicho, itaanza kuwatambua walipa kodi ambao tayari wameainishwa kama wawajibikaji wazuri katika ulipaji kodi.

Waziri Meghji, katika maelezo yake alisema kuwa, utaratibu huo mpya unalenga kupunguza kero ya ucheleweshaji wa mizigo bandarini.

Meghji alisema tatizo hilo limekuwa ni kero ya muda sasa, hata kufikia hatua ya kupunguza uwezo wa Tanzania kutumia fursa za kibisashara ya kikanda, hasa kupitisha mizigo ya nchi jirani.

Aidha, alisema kuwa, uchambuzi uliofanywa unaonyesha kuwa, tatizo hilo linachangiwa pia na idadi kubwa ya taasisi zinazohusika katika kusimamia uingizaji wa bidhaa nchini, jambo ambalo pia litaangaliwa na kupatiwa ufumbuzi.

Kutokana na hali hiyo, Meghji alisema kuwa, TRA itaanza kutumia utaratibu huo ambao utawezesha bidhaa za walipa kodi hao wazuri kupitishwa moja kwa moja bila ukaguzi.

Aliwaambia wajumbe wa kamati hiyo kuwa, hatua nyingine iliyochukuliwa kukabili tatizo hilo ni kupunguza kiwango cha bidhaa kinachopitishwa kwenye ‘red channels’ (eneo la uangalizi mkali) kutoka asilimia 80 ya awali.

Alisema chini ya utaratibu huo mpya, asilimia 40 ya bidhaa zitapitishwa kwenye milango ya kijani (ukaguzi wa kawaida) na kuondoshwa bandarini moja kwa moja.

Sambamba na hilo, asilimia 40 ya bidhaa nyingine zitafanyiwa ukaguzi wa kawaida bila kufanyiwa upekuzi, zikifuatiwa na ukaguzi wa kina baada ya kuondolewa bandarini.

Chini ya utaratibu huo mpya, alisema, ni asilimia 20 tu ya bidhaa ndizo zitakazofanyiwa upekuzi kabla ya kuondolewa bandarini.

Hatua ya tatu itakayochukuliwa na TRA kukabili tatizo hili, inahusu bidhaa zinazoingizwa na wawekezaji waliosajiliwa na Kituo cha Uwekezaji nchini (TIC).

Meghji alibainisha kuwa, bidhaa hizo zitapitishwa moja kwa moja katika milango ya kijani ambapo asilimia 25 ya bidhaa hizo zitafanyiwa ukaguzi wa kawaida, ukifuatiwa na ukaguzi wa kina baada ya kuondolewa bandarini.

Alisema magari mapya, na yale yaliyotumika kwa kipindi kisichozidi miaka mitano hayatapitishwa kwenye ‘red channel’ kama ilivyokuwa awali.

Aidha, Meghji alisema kuwa, bidhaa maalum zinazohitaji vibali kutoka idara mbalimbali za serikali, zitafanyiwa ukaguzi wa nyaraka pekee badala ya upekuzi kamili wa bidhaa zenyewe, ili kuharakisha uondoshwaji bandarini wa bidhaa hizo.

Alisema TRA sasa itawajibika kutoa uamuzi katika muda wa saa 24 ili kuondosha bandarini bidhaa zote zilizoagizwa kwa kutumia thamani zilizobainishwa kwenye kadhia ya muagizaji, ambazo bei zake hazitapatikana muda huo.

Maelezo hayo ya serikali, yanakuja wakati wafanyabiashara, hasa wale wanaohusika na uingizaji wa bidhaa kutoka nje, wakilalamikia taratibu na urasimu uliopo katika kuondosha mizigo bandarini.

Aidha, wafanyabiashara hao wameonyesha kukerwa na uwingi wa taasisi ambazo zinahusika katika taratibu za uondoshwaji wa mizigo bandarini, na kwa muda mrefu wamekuwa wakieleza kuwa, jambo hilo ni moja ya sababu kubwa zinazokwamisha utoaji wa haraka wa mizigo bandarini.

Kwa ujumla, bandari ya Dar es Salaam, imekuwa ikilalamikiwa kwa urasimu unaosababisha kukosa fursa nyingi za kufanya biashara na nchi ambazo hazina bandari katika ukanda huu wa Afrika.

Hivi karibuni, Waziri Mkuu Edward Lowassa alifanya ziara ya ghafla katika Bandari ya Dar es Salaam na akatoa maelekezo kuhusu haja ya lazima ya kupunguza msongamano wa makontena ya mizigo.

Ziara hiyo ya Waziri Mkuu Lowassa, ilikuja wakati kukiwa na taarifa kwamba, bandari hiyo ilikuwa imeshaanza kuonekana kero miongoni mwa waagizaji wa bidhaa ambao baadhi yao walishaanza kutumia bandari za nchi jirani kama mbinu mbadala.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.