WIZARA ya Miundombinu, ndiyo pekee ambayo bajeti yake imekwama kupitishwa katika ngazi ya kamati husika kabla ya kuanza kwa kikao cha Bunge la Bajeti, wiki ijayo.
Hali hiyo imetokana na uamuzi wa wajumbe wa Kamati ya Miundombinu kukataa kuridhia mwelekeo wa bajeti hiyo baada ya Wizara ya Fedha kushindwa kuwasilisha mabadiliko yaliyofikiwa juzi wakati wa kikao kati ya Waziri Mkuu, Edward Lowassa na wajumbe wa kamati hiyo.
Wajumbe wa kamati hiyo, walikuwa wameyakataa mapendekezo ya matumizi ya wizara hiyo, kutokana na ufinyu wa fungu la fedha lililokuwa limetengwa kwa ajili ya miradi ya barabara.
Katika kikao kilichoongozwa na Waziri Mkuu, juzi, serikali ilikubali kutenga asilimia 15 ya fungu la fedha kutoka katika fungu la matumizi mengine, na kuliingiza katika miradi ya barabara, lakini hadi jana, Wizara ya Fedha ilikuwa haijaweza kuwasilisha nyaraka kuhusu uamuzi huo na kusababisha kamati hiyo kutoipitisha bajeti.
Badala yake sasa, bajeti ya wizara hiyo itapitishwa mjini Dodoma baada ya Wizara ya Fedha kuandaa taarifa za mabadiliko hayo na kuiwasilisha kwenye Baraza la Mawaziri kabla ya kupelekwa kwenye kamati husika na kupitishwa.
Kwa mujibu wa taratibu za kiserikali, mabadiliko yanapotokea kwenye makadirio ya bajeti, ni lazima Wizara ya Fedha iandae waraka kisheria ili kuongeza fedha kwenye wizara inayotakiwa.
Chanzo cha habari kutoka ndani ya kamati hiyo, kiliiambia Tanzania Daima kuwa, baada ya serikali kuridhia ongezeko la asilimia 15 kwenye uendelezaji miundombinu kutoka kwenye matumizi ya ziada, ili kuimarisha barabara, ni jukumu la Wizara ya Fedha kupeleka mabadiliko hayo kwenye Baraza la Mawaziri.
“Kamati imeshindwa kupitisha kwa kuwa hakuna taarifa za mabadiliko zilizoletwa kwetu. Tumeshindwa kupitisha na badala yake kazi hii itafanyika Dodoma,” kilisema chanzo hicho na kuongeza kwamba, kabla ya kufikishwa kwao, ni lazima wizara hiyo izigawe fedha hizo katika matumizi mbalimbali ya maendeleo.
Uamuzi wa kutenga asilimia hizo 15 kutoka kwenye matumizi ya ziada, umeifanya serikali iongeze kiasi cha sh bilioni 393, ambazo ndizo zitakazogawanywa katika miradi ya maendeleo ndani ya wizara hiyo.
“Unajua si fedha zote zitajenga barabara. Katika fedha hizo, inatakiwa kutengwa sh bilioni 80 kwa ajili ya Shirika la Ndege (ATC), sh bilioni 20 zitakwenda kwenye Shirika la Reli (TRC), bilioni 120 zitaingia kwenye Mfuko wa Wabunge na miradi mingine, halafu zinazobaki zinakwenda kwenye barabara,” kilisema chanzo hicho.
Akizungumza baada ya kikao cha kamati hiyo, Waziri wa Miundombinu, Andrew Chenge, alisema uamuzi wa kamati hautakwamisha kupita kwa bajeti yake.
Akitoa ufafanuzi wa kauli hiyo, Chenge alisema wizara yake inasubiri taarifa ya mabadiliko ya fedha kutoka Hazina ili kuendana sawa na makubaliano yaliyofikiwa baada ya ushauri wa Kamati ya Fedha na Uchumi na ile ya Miundombinu na serikali, ya kuiongezea fedha wizara hiyo.
“Hazina hawajasema kama tayari wameshaandaa taarifa ya mabadiliko… zipo taratibu zinazofikiwa kabla ya taarifa hizo kuwasilishwa kwenye kamati,” alisema Chenge na kufafanua kuwa, binafsi hafahamu kiasi kitakachotumika kwa ajili ya uimarishaji wa barabara.
Aidha, Chenge alisema alipokea ushauri wa kutaka fedha za wizara yake ziongezwe kutoka kwa Rais Jakaya Kikwete, hivyo msimamo wa wabunge wa kamati hizo ulikuwa sawa na kauli ya rais.
“Kabla hajaenda Arusha, mheshimiwa rais alinieleza kuwa, fedha za wizara yangu ni kidogo, hivyo alinitaka kutizama upya. Nadhani alizungumza na Waziri wa Fedha kuhusu hilo,” alisema Chenge na kusisitiza kuwa, uamuzi wa kuongeza asilimia 15 ulitokana na ushauri wa Rais Kikwete na msimamo wa wabunge.
Hata hivyo, baada ya mambo kuwawia magumu mbele ya kamati za bunge, Waziri wa Fedha, Zakia Meghji, Waziri wa Mipango, Uchumi na Uwezeshaji, Juma Ngasongwa na Waziri Chenge, walimwendea Waziri Mkuu kwa lengo la kupata ufumbuzi wa msimamo wa wabunge.
Uamuzi wa serikali kutoa asilimia 15 ya fedha kutoka kwenye matumizi ya ziada, utapunguza safari za viongozi, warsha, mikutano, semina, ununuzi wa magari na mambo mengine yanayofanana na hayo.
Waziri Meghji, anatarajia kusoma bajeti ya serikali kwa mwaka wa fedha 2007/08 inayokadiriwa kuwa sh trilioni 6.06 mbele ya wabunge, Juni 14 mjini Dodoma wakati wa kikao cha saba kitakachoanza Juni 12, kiasi ambacho ni ongezeko la asilimia 26 ukilinganisha na ile ya mwaka jana (2006/07).