JUZI Watanzania tuliungana na mataifa mengine kuadhimisha Siku ya Mazingira Duniani ambayo kitaifa iliadhimishwa mkoani Mtwara, mgeni rasmi akiwa Makamu wa Rais, Dk. Ali Mohamed Shein.
Wakati kaulimbiu ya maadhimisho hayo kitaifa ikiwa ‘Hifadhi Mazingira: Panda Miti na Kuitunza’, kaulimbiu ya kimataifa ilikuwa, ‘Udhibiti wa ongezeko la Joto na Kutoweka kwa Barafu’ ambayo ilikuwa na lengo la kutukumbusha uhusiano uliopo kati ya uharibifu wa mazingira na mabadiliko ya hali ya hewa duniani.
Umuhimu wa kuhifadhi mazingira umekuwa ukisisitizwa na wanasayansi, wanaharakati na vyombo vingi vya habari duniani kutokana na kuwapo kwa hatari kubwa kwa wanyama, binadamu, mimea na mazingira kwa ujumla iwapo hatari hii haitadhibitiwa.
Kwa mujibu wa sehemu ya pili ya ripoti ya Halmashauri ya Hali ya Hewa Duniani (IPCC) iliyotolewa mjini Brussels katika miaka ya hivi karibuni, wataalamu wa hali ya hewa wameonya kwamba ongezeko la joto duniani litasababisha hasara kubwa na ya haraka zaidi kuliko ilivyokadiriwa awali.
Ripoti hiyo yenye urefu wa zaidi ya kurasa 1,400, lakini iliyozusha majadiliano makali hususan katika maneno yaliyotumika katika muhtasari wa kurasa 21 wenye kuwalenga wanasiasa, wanasayansi kadhaa waliwashutumu vikali wajumbe wa serikali za China, Urusi, Saudi Arabia na Marekani kwa kiburi chao cha kutosikiliza maonyo yanayotolewa juu ya athari hizo ambazo kwa kiasi kikubwa zinaathiri nchi zinazoendelea kama Tanzania ambazo hazihusiki kwa kiasi kikubwa na ongezeko hili huku bajeti zao zikiwa hazitoshelezi katika kukabiliana na hali hii.
Ripoti hii inazungumzia athari kali pale inapotabiri uhaba wa maji unaotokana na uchafuzi wa hewa utakavyoathiri mabilioni ya watu, wanyama na mimea ambavyo vitatokomea kabisa huku kiwango cha maji ya bahari kikiongezeka, hali ambayo ina hatari ya kumeza maeneo ya nchi kavu hususan vikiwamo visiwa.
Takriban asilimia 20 hadi 30 za viumbe vya mimea na wanyama viko hatarini kutokomea duniani ikiwa wastani wa joto duniani utazidi kwa nyuzi 1.5 hadi 2, ripoti ilisema baada ya kufanyiwa marekebisho.
Pia utafiti rasmi uliofanyika mwaka huu umebainisha kwamba joto duniani limeongezeka kwa nyuzijoto 0.6 tangu katikati mwa karne ya kumi na tisa, na kwamba ongezeko jingine la nyuzijoto 1.4 hadi 5.8 linakadiriwa kutokea ifikapo mwaka 2100.
Ili kukabiliana na hali hii, wataalamu wanautaka ulimwengu wenye viwanda vingi kupunguza kiwango cha uzalishaji wake wa gesi za viwandani.
Wakati mchango wa Afrika katika mabadiliko ya hali ya hewa ukiwa si muhimu, lakini ndiyo inayoathirika kwa kiasi kikubwa na mabadiliko haya kutokana na uchumi wake kutegemea maliasili zinazokumbwa na mabadiliko haya huku ikiwa na uwezo mdogo katika kukabiliana na mabadiliko haya.
Hiyo inatokana na gesi inayozalishwa na mataifa yenye viwanda kama vile carbon dioxide na methane kuingia angani na kusambaa duniani kutokana na kuungua kwa fiweli.
Utoaji wa gesi hizi chafu unanyonya na kunasa nishati ya jua na mkusanyiko huu mkubwa wa gesi za viwandani husababisha ongezeko la joto ambalo husababisha mabadiliko ya hali ya hewa ambayo moja kwa moja yanakuja kuathiri viumbe hai na mazingira kwa ujumla.
Mojawapo ya eneo linaloshuhudia matokeo ya mabadiliko haya na ambalo limekuwa likitumika katika mikutano mingi kama mfano hai usiopingika juu ya athari za kuongezeka kwa joto duniani ni Mlima Kilimanjaro, moja ya vivutio vikubwa vya kujivunia Tanzania na dunia ilivyobarikiwa kuwa navyo.
Ukiwa mlima mrefu kuliko yote barani Afrika na wa pili duniani, kilele chake cha kuvutia chenye theluji kimekuwa kikikumbwa na kupungua kwa barafu yake kwa kadiri ya miaka inavyozidi kwenda mbele na iwapo juhudi za makusudi hazitachukuliwa kitatokomea baada ya miaka 15 ijayo.
Wanasayansi katika mikutano yao wamekuwa wakitumia picha iliyochukuliwa katika utafiti wa kwanza katika mlima huo mwaka 1912 kulinganisha na picha iliyochukuliwa miaka ya hivi karibuni ambayo imeonyesha kupungua kwa barafu kwa kiasi cha kutisha.
Februari 2001 katika mkutano wa Chama chga Uboreshaji Sayansi cha Marekani (AAAS), watafiti waliripoti kupungua kwa kiasi kikubwa kwa barafu ya kilele cha Kibo cha Mlima Kilimanjaro kwa asilimia 82 ya barafu kulinganisha na utafiti wa kwanza mwaka 1912, na imezidi kuwa nyembamba.
Kwa mujibu wa tafiti mbalimbali, sehemu kubwa ya barafu iliyobakia katika Mlima Kilimanjaro itatokomea kipindi cha miaka 15 ijayo.
Unapotembelea eneo kuzunguka mlima huo sanjari na kilele chake utajionea athari za uchafuzi wa hali ya hewa duniani.
Eneo la msitu kuzunguka eneo hilo pia limekuwa likipungua kwa mita 500 kipindi cha miaka 100 iliyopita. Wataalamu wa mazingira wanajiuliza iwapo hali imekuwa hivyo, hali itakuwaje kwa miaka 100 ijayo?
Professor Lonnie Thompson wa Chuo Kikuu cha Ohio State ambaye alifanya utafiti katika kilele hicho maarufu, anasema mlinganisho wa sasa na wa zamani umeonyesha asilimia 33 ya barafu ya Mlima Kilimanjaro imetokomea kipindi cha miongo miwili iliyopita na asilimia 82 imepotea tangu 1912.
Aidha, tafiti zilizofanywa katika vilele vingine vya milima vilivyo katika nchi za kitropiki zimetoa matokeo yanayofanana, aliuambia mkutano wa AAAS.
Alionya kuyeyuka kutasababisha athari kubwa hususan kwa usambazaji maji, kilimo cha umwagiliaji, uzalishaji nguvu ya umeme pamoja na utalii.
“Kilimanjaro ni tegemeo namba moja la kuipatia Serikali ya Tanzania fedha za kigeni. Watalii 20,000 huutembelea kila mwaka kwa ajili ya kuangalia uzuri wa kilele chake chenye theluji kilichopo katika nyuzi tatu kusini mwa Ikweta. Lakini inasikitisha haya yote yatakuwa ndoto ifikapo mwaka 2015 iwapo hali itaachwa hivi hivi,” alionya.
Professa Thompson alitumia miaka karibu 20 kufanya utafiti wa maeneo yenye barafu yaliyo katika nchi za kitropili kwenye milima ya Amerika ya Kusini, Afrika, China na Tibet.
“Theluji ni kama mabwawa ya asili,” alisema. “Hutunza barafu wakati wa msimu wa mvua na kuyeyuka wakati wa kiangazi na kutiririsha maji mitoni,” alisema.
Ikiwa na maana kuwa litakuwa pigo kwa viumbe hai katika shughuli zake za kila siku zinazotegemea maji kwa ajili ya kunywa, umwagiliaji, nguvu ya umeme na mengineyo.
Aidha, alisema kupotea barafu ni pigo kwa sayansi ambayo hutumia barafu iliyoganda katika theluji kwa miongo na karne nyingi kuchunguzia hali ya hewa ya huko nyuma.
“Upotevu wa barafu hizi unatishia rasilimali ya maji kwa uzalishaji wa nguvu za umeme, umwagiliaji mazao na usambazaji wa maji katika mnispaa.
Aidha, kuyeyuka kwa barafu hii vileleni mwa theluji husababisha kuongezeka kwa kiwango cha maji baharini,” alisema.
Kazi za Professor Thomspon ni sehemu ya harakati za taasisi ya kimataifa inayoshughulikia mazingira na mabadiliko ya hali ya hewa (IGBP), inayoangalia jinsi mazingira ya ulimwengu yanavyobadilika.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa IGBP, Dk. Will Steffan, shughuli za Thompson zimetoa ushahidi wa kuongezeka kwa mabadiliko ya hewa duniani ambayo yatakuwa janga kuu na kushuhudia kutokomea kwa viumbe visivyoweza kuhimili hali hiyo ya mabadiliko kama ilivyowatokomeza wanyama aina ya Dinosaur huku sasa kukiwa na upungufu wa samaki majini.
Ili kukabiliana na hali hii, jumuiya ya kimataifa inatakiwa iendelee kushikamana katika suala la kuhifadhi mazingira na ongezeko la joto pamoja na kuzibana nchi tajiri zikubaliane na mapendekezo yanayotolewa na wataalamu ili kudhibiti hali hii, ikiwamo upunguzaji wa gesi zinazozalishwa na viwanda vyao.