RAIS Jakaya Kikwete jana alilihutubia taifa kupitia katika mazungumzo yake na wahariri na wakuu wa vyombo mbalimbali vya habari.
Mada kuu katika hotuba yake ya jana ilikuwa ni kuhusu kuanza kwa kampeni ya kupima vurusi vya ukimwi kwa hiari inayoanza mwezi ujao na kuongezeka kwa kasi kwa tatizo la utoro na ujauzito wa wanafunzi shuleni.
Kimsingi mada alizozungumzia rais katika hotuba yake hiyo ya jana, zinagusa misingi muhimu kabisa ya kimaendeleo ya taifa lolote lile ambayo ni nguvu kazi, afya na elimu.
Wakati tukitambua umuhimu wa mada zote mbili alizozizungumzia rais, tumeona ni vyema kwa leo tukalizungumzia japo kwa muhtasari tatizo hili la utoro na mimba za kabla ya wakati za watoto wa shule za msingi na sekondari.
Ni ukweli kwamba katika miaka ya hivi karibuni, tatizo hili la watoto wadogo kuzaa watoto limekuwa likitokea katika maeneo mbalimbali hapa nchini.
Ingawa rais amelizungumzia suala hilo akitoa mifano ya maeneo mbalimbali nchini na hususan vijijini, bado ni ukweli kwamba, hata ukiondoka leo ukatembelea katika wodi ya wazazi katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili utashangaa kuwakuta watoto wadogo wa umri wa kuwa ama shule ya msingi au sekondari wakisubiri kujifungua au wakihudumiwa baada ya kujifungua.
Kama hiyo haitoshi, ongezeko hili la kasi linapaswa kudhibitiwa, kwani takwimu za rais za kutoka mikoa mbalimbali nchini zinatisha.
Kwa maelezo yoyote yale, wakati tukikiri kuwa tatizo hili la utoro na ujauzito wa watoto wa shule ni la kushtusha, tunao wajibu wa lazima wa kuanza kuchukua hatua za kukabiliana nalo.
Takwimu kwamba wanafunzi watoro wa shule za msingi mwaka jana kwa nchi nzima walikuwa 44,742 wakiongezeka kutoka 32,469 wa mwaka 2005, si jambo la kukaa kimya, tukiwa mashuhuda na kumsikiliza rais pasipo kuchukua hatua.
Kama hiyo haitoshi, takwimu nyingine kwamba kwa upande wa sekondari, idadi ya wanafunzi waliotoroka iliongezeka pia kutoka watoto 6,912 mwaka 2005 hadi kufikia 7,734 mwaka jana, zinaogopesha hata kulazimisha kuchukua hatua.
Habari kwamba, idadi ya wanafunzi waliomaliza darasa la saba huko Tunduru ilipungua kwa zaidi ya nusu kutoka 7,000 walioanza hadi 3,000 waliofanya mitihani, si jambo ambalo Watanzania wazalendo wanaoipenda nchi yao wanaweza wakaliacha likipita hivi hivi tu.
Kwa sababu ya kutambua kuwa taifa hili liko katika mtego mkubwa kabisa unaoweza kututumbukiza katika hatari ya kuwa taifa lenye wajinga wengi katika karne hii, tunao wajibu wa kujinusuru kama nchi.
Wazazi, walimu na jamii ya Watanzania kwa ujumla tunao wajibu wa lazima wa kuanzisha kampeni ya kitaifa ya kuinusuru elimu yetu kuanzia ya msingi hadi ile ya vyuo vikuu.
Tukiwa sehemu ya jamii hiyo ya Watanzania tunaamini kwamba, iwapo tutaendelea kukaa kimya pasipo kuchukua hatua, basi Tanzania inaweza ikajikuta ikiwa bado haijajiandaa ipasavyo wakati taifa hili litakapoingia rasmi katika shirikisho la Afrika Mashariki, miaka michache ijayo.
Watanzania tunao wajibu wa lazima wa kuhakikisha kuwa kila mmoja kwa nafasi yake, viongozi wa dola na wale wa kijamii kwa kushirikiana na wananchi kwa ujumla, tunao wajibu wa kuanza kuhimizana kwa kuheshimu maadili yetu ya Kitanzania yanayoweka mipaka ya kimahusiano kati ya watu wazima na wanafunzi.
Tunao wajibu wa kutambua kuwa, iwapo tutayaacha matatizo haya ya utoro shuleni na mimba za wanafunzi yakawa maneno ya rais peke yake, basi maadui umaskini, maradhi na ujinga yataendelea kulitafuna taifa hili na kutufanya tuendelee kuwa wasindikizaji katika kila eneo.