UBALOZI wa Marekani nchini umeandaa siku maalumu kwa ajili ya wananfunzi waliopata nafasi za masomo katika vyuo vikuu nchini humo, kupata taarifa za awali kuhusiana na nchi hiyo.
Taarifa iliyotolewa jana na ubalozi huo ilisema kuwa Juni 13 mwaka huu, imetengwa kwa ajili ya kuwapatia taarifa hizo wanafunzi waliopata nafasi za masomo Marekani.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, shughuli hiyo itaratibiwa na kituo cha ushauri kwa wanafunzi cha ubalozi huo.
“Watu waliowahi kusoma Marekani, maofisa wa uhamiaji na wafanyakazi wa kitengo cha ushauri kwa wanafunzi watazungumzia mambo mbalimbali yatakayowasaidia wanafunzi kujiandaa kwa ajili ya safari zao na maisha watakapokuwa Marekani,” inasema sehemu ya taarifa hiyo.
Ofisa Utamaduni wa ubalozi huo, Karen Grissette, alisema mambo yatakayozungumzwa ni pamoja na maisha ya Marekani, mabadiliko ya utamaduni, jinsi ya kumudu masomo ukiwa Marekani, hali ya hewa, jinsi ya kusafiri ndani na nje ya Marekani, jinsi ya kujiandaa kwa safari na unayotakiwa kuyafahamu wakati unajiandaa kurejea nchini.
“Pia kutakuwa na muda wa kuuliza maswali. Wazazi pia wanakaribishwa,” alisema.
Alibainisha kuwa maofisa kutoka kitengo cha uhamiaji, watawaelewesha washiriki masuala kuhusiana na uhamiaji ambayo yanahusisha jinsi ya kuomba visa, vigezo vya kupatiwa visa, jinsi ya kuingia Marekani, unaweza kukaaa kwa muda gani Marekani ukiwa mwanafunzi pamoja na bahati nasibu ya visa.
Kwa mujibu wa mshauri wa wanafunzi, Frida Mwenegoha, programu hiyo itawasaidia wanafunzi wa Kitanzania kujiandaa kwa ajili ya maisha yao ya masomo nchini Marekani.
“Ni vizuri mwanafunzi akafahamu kabla atarajie nini atakapowasili Marekani,” alisema.
Mwenegoha alibainisha kuwa kila mwaka zaidi ya wanafunzi 1,000 kutoka Tanzania wanakwenda Marekani na Tanzania ni nchi ya saba miongoni wa nchi za Afrika kusini mwa Jangwa la Sahara, zinazopeleka wanafunzi wengi nchini humo.