RAIS Jakaya Kikwete amewataka waandishi wa habari kuachana na kile alichokielezea kuwa ni utaratibu wa kuwachunguza viongozi wastaafu hususan katika masuala madogo.
Kikwete, aliyekuwa akizungumza na wahariri na wakuu wa vyombo mbalimbali vya habari jijini Dar es Salaam jana, alitoa kauli hiyo wakati alipotakiwa kutoa maoni yake kuhusu shutuma zinazoelekezwa kwa Rais mstaafu, Benjamin Mkapa, juu ya uamuzi wake wa kusajili kampuni akiwa Ikulu na kuomba mkopo benki akijitambulisha kuwa mjasiriamali.
Akizungumza kwa tahadhari kubwa, taratibu na akiwa ametulia, Rais Kikwete alisema: “Sina hakika na hilo (kama Mkapa alifanya biashara Ikulu)…kwa maoni yangu, nadhani huu utaratibu wa kuwachunguza viongozi wastaafu katika mambo kama haya si mzuri sana.”
Rais Kikwete alirejea msimamo wake alioutoa siku chache tu baada ya kupitishwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwa mgombea urais kwa tiketi ya chama hicho kwa kusema, anadhani kuwa halitakuwa jambo jema kwake akiwa madarakani hivi sasa, kuanza kuwachunguza viongozi wakuu wastaafu kwa sababu tu ya mambo madogo yanayoandikwa katika magazeti.
Mbali ya hilo, akijigeukia yeye, kwa namna iliyoonyesha kutoafiki kuanza kufanya biashara katika umri mkubwa, Rais Kikwete alisema anaamini akianza kufanya biashara sasa, atakwama.
Bila kutaja jina la mtu, Kikwete (57) alisema rafiki yake mmoja Mwingereza alipata kumshauri kutoingia kwenye biashara akiwa na umri wa zaidi ya miaka 40, kwani atashindwa, ushauri ambao hadi hivi sasa umemjengea imani ya kuamini kuwa yeye hawezi kufanikiwa katika biashara.
Badala yake, Rais Kikwete alisema kwa mtazamo wake, anaona anaweza akafanikiwa iwapo atakuwa ama mkulima wa mazao kama mananasi au mfugaji wa ng’ombe.
Hata hivyo, alisema kwa kuwa yeye si mtu wa kuogopa, iwapo litatokea jambo kubwa ambalo litapaswa kufanywa uchunguzi dhidi ya kiongozi yeyote mstaafu, hatasita kufanya hivyo.
“Likitokea jambo kubwa tutalifanyia uchunguzi, kwani hatuogopi mtu, ingawa nadhani tukianza kufanya uchunguzi kwa kuwa tu mtu ameandikwa magazetini, hilo mimi halinifurahishi,” alisema Rais Kikwete.
Akizungumzia tatizo la wanafunzi 29 Watanzania waliokwama Ukraine baada ya kushindwa kulipia gharama za masomo, Rais Kikwete alisema serikali haiwezi kufanya lolote kuwagharamia kwani walikwenda huko kwa utashi wao.
Aliwataka Watanzania kutambua kuwa, gharama za kumsomesha mwanafunzi mmoja nje ya nchi ni kubwa sana kulinganisha na kumsomesha nyumbani na hivyo iwapo watashindwa kumudu gharama hizo, ni vyema wakazingatia ushauri wa serikali wa kurejea nyumbani na kutafuta vyuo vya hapa.
Mbali ya hayo, mazungumzo kati ya rais na wahariri wakuu ya jana yalikuwa yakilenga mada kuu mbili; ya kwanza ikiwa ni mkakati wa serikali kukabiliana na tatizo la ugonjwa wa Ukimwi kwa kuanzisha kampeni ya kitaifa ya upimaji wa virusi kwa hiari na la pili likiwa ni lile la kuongezeka kwa tatizo la utoro na ujauzito miongoni mwa wanafunzi wa kike katika shule za msingi.
Katika mazungumzo yake hayo, Kikwete alisema kampeni hiyo ya kitaifa ya kupima kwa hiari iliyokuwa ifanyike mwezi huu sasa imeahirishwa hadi Julai 14 mwaka huu.
Aliwataka viongozi wakuu wa serikali, wanahabari, na wananchi kwa ujumla kujitokeza kupima ili kupunguza na ikibidi kumaliza kabisa maambukizi mapya ya ugonjwa huo usio na tiba wala chanjo.
Alisema wakati wastani wa maambukizi ya ugonjwa huo kitaifa ni asilimia saba hivi sasa, lengo ni kuhakikisha kiwango hicho kinashuka ifikapo mwakani hadi kufikia asilimia 6.5.
Kuhusu madai ya baadhi ya viongozi wa dini kusema ugonjwa huo unaweza kutibika kwa maombi, Kikwete alisema iwapo hilo linawezekana, basi ni jambo la heri na faraja kubwa, ingawa wataalamu wa afya wamekuwa wakipingana nalo.