Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Meghji atoa mwelekeo wa bajeti tegemezi
Meghji atoa mwelekeo wa bajeti tegemezi
By Habari Tanzania | Published  01/1/1970 | Habari za Kitaifa | Unrated
na Irene Mark


WAZIRI wa Fedha, Zakia Meghji, jana aliwasilisha mwelekeo wa bajeti ijayo ya serikali ambayo inatoa sura ya kuongezeka zaidi kwa utegemezi kwa wafadhili kuliko ilivyokuwa katika mwaka unaomalizika baadaye mwezi huu.

Akisoma mwelekeo wake huo, mbele ya wajumbe wa Kamati ya Fedha na Uchumi ya Bunge, Waziri Meghji alisema bajeti nzima ijayo itakuwa ya sh trilioni 6.06 kutoka sh trilioni 4.8 ya mwaka unaomalizika, kiasi ambacho ni ongezeko la asilimia 26.25.

Aidha, mwelekeo huo uliowasilishwa na Meghji unaonyesha pia kwamba, kiwango cha utegemezi kwa fedha kutoka kwa wahisani kitaongezeka zaidi katika mwaka ujao wa fedha, hali ambayo inazidi kuliweka taifa katika makucha ya wafadhili. Majumuisho yaliyowasilishwa na Meghji yanaonyesha kwamba, katika mwaka ujao wa fedha, fedha kwa ajili ya misaada na mikopo ya miradi ya maendeleo itaongezeka kutoka sh bilioni 809, 631 mwaka jana, hadi kufikia sh trilioni 1.2.

Katika majumuisho hayo, fedha za wafadhili zitakazotumika katika maendeleo ni kiasi cha sh trilioni 1.461 kati ya jumla ya sh trilioni 2.1, kiwango ambacho ni sawa na asilimia 70 ya fedha zote zilizotengwa kwa ajili ya kiasi hicho.

Kama hiyo haitoshi, mwelekeo wa bajeti uliotolewa na Meghji unaonyesha pia kwamba kiasi kikubwa cha fedha katika bajeti ijayo kitatumika zaidi kwa ajili ya shughuli zisizo za kimaendeleo.

Katika mwelekeo huo, Meghji alionyesha kwamba, matumizi yote ya maendeleo ni sh trilioni 2.1, yakilinganishwa na matumizi ya kawaida yatakayofikia sh trilioni 3.96.

Aidha, katika mawasilisho yake, Meghji alisema kwa mwaka ujao wa fedha, serikali imedhamiria kupunguza umaskini wa kipato kwa wananchi wake kwa kuongeza fedha za maendeleo na kasi ya utekelezaji wa MKUKUTA.

Katika hilo, Meghji alisema serikali imetenga sh trilioni 3.966 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na sh trilioni 2.101 kwa matumizi ya maendeleo, tofauti na bajeti iliyopita ambapo jumla ya sh trilioni 2.6 zilitengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida na sh trilioni 1.281 kwa matumizi ya maendeleo.

Alisema kwa kuzingatia hayo, serikali imelenga kukusanya mapato ya ndani ya sh trilioni 3.503 na kupata jumla ya sh trilioni 2.549 kutoka kwa wahisani kama misaada, mikopo ya masharti nafuu na misamaha ya madeni kwa kiasi cha sh bilioni 206.037.

Kuhusu vipaumbele vya bajeti hiyo, Meghji aliwaeleza wajumbe wa kamati hiyo kuwa ni kutekeleza ilani ya uchaguzi ya mwaka 2005 ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), MKUKUTA na miongozo mingine ya kitaifa kwa maendeleo ya wananchi.

“Vipaumbele katika bajeti hii vimezingatia sana Ilani ya mwaka 2005 ya CCM, MKUKUTA, maoni ya waheshimiwa wabunge ya Aprili mwaka huu kule Dodoma na miongozo ya kitaifa kwa maendeleo ya Watanzania wote,” alisema Meghji.

Aidha, suala la kuimarisha miundombinu muhimu ya kitaifa, limepewa kipaumbele likielezewa kuwa ni kichocheo cha kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi.

Kadhalika, sekta ya kilimo, ikiwamo mipango ya maendeleo ya kilimo cha umwagiliaji, utafiti, ukuzaji wa teknolojia na utoaji wa ruzuku ya mbegu na pembejeo za kilimo, nayo ni moja ya maeneo yatakayopewa kipaumbela kupitia bajeti hiyo.

Aidha, kuwezesha utekelezaji wa ujenzi wa nyumba za walimu, ununuzi wa zana za kufundishia, uboreshaji wa masilahi ya watumishi wa umma na uwezeshaji wa ajira katika sekta za huduma muhimu ikiwamo afya na elimu.

Alisema, utekelezaji wa vitambulisho vya taifa na ukarabati wa hospitali za mikoa, zahanati na vituo vya afya ni moja kati ya mambo yatakayopewa kipaumbele katika bajeti hiyo.

Kimsingi, bajeti hiyo imelenga kukamilisha mradi mkubwa wa maji ya Ziwa Victoria kwa mikoa ya Shinyanga na Kahama na kuharakisha utekelezaji wa awamu ya pili ya mpango wa kurasimisha Rasilimali na Biashara za wanyonge (MKURABITA).

Aidha, Waziri Meghji alibainisha kuwa utaratibu mpya wa kurasimisha ardhi na biashara utakamilika na kuanza kutumika Machi mwakani.

Aliongeza kuwa utekelezaji wa awamu ya pili ya mageuzi na maboresho ya sekta ya fedha, utawezesha wananchi kupata mikopo ya uzalishaji, biashara na nyumba ikiwa ni pamoja na mikopo kwa mali za kukodi na kuboresha mifuko ya hifadhi ya jamii.

Meghji alisema kuanzia Julai mwaka huu, utaratibu wa kuhudumia wastaafu utabadilishwa, ili kuondoa kero zinazowasibu wastaafu wanaohudumiwa na hazina.

Wakichangia mada baada ya kupokea makadirio ya bajeti hiyo, wajumbe wa kamati hiyo waliishauri serikali kuboresha makusanyo kwa vyanzo vya mapato vilivyopo na kubuni vipya ili kuongeza mapato.

Aidha, wabunge hao walitaka uwepo utaratibu madhubuti na sheria katika uuzaji wa samaki na dhahabu nje ya nchi, sekta inayoiingizia serikali asilimia 56 katika bajeti.

“Tunafanya vizuri katika biashara za nje hasa upande wa samaki na dhahabu… sasa ikitokea tukayumba kidogo tutaathiri uchumi wetu,” alisema Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Abdallah Kigoda.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  3. Is Tanzania a safe place to invest?
  4. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
  5. Nitaendelea kugombea nafasi za kisiasa- Balozi Karume
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Linda Garner
  4. Nthelezi Nesaa
  5. Marshy Abdu
  6. Prosper Kwigize
  7. Salehe Mmoro
  8. Ramadhan Semtawa
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.