Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Wazanzibari wabishania muungano
Wazanzibari wabishania muungano
By Marshy Abdu | Published  06/6/2007 | Habari za Kitaifa | Unrated
Wazanzibari wabishania muungano
na Saada Said


MKURUGENZI wa Mashitaka Zanzibar (DPP), Othman Masoud, ametofautiana na Naibu Waziri Kiongozi, Ali Juma Shamuhuna, juu ya masuala kadhaa ya muungano na kero zake.

Tofauti hizo zilitokea jana wakati wa semina ya Mustakabali wa Muungano iliyoandaliwa na Vyuo Vya Elimu ya Juu Zanzibar (ZAHLIFE) katika ukumbi wa Hoteli ya Bwawani mjini hapa.

Wakati Shamuhuna akitoa mada yake iliyowasilishwa na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Mahmoud Thabit Kombo, alisema Wazanzibari hawana mamlaka ya kuhoji muungano.

“Sisi hatuna madaraka wala hatukupewa uwezo wa kuhoji wala kuvunja muungano,” alisema Shamuhuna.

Akichangia mada katika semina hiyo, DPP Masoud alisema kufika umri wa miaka 43 si kigezo sahihi cha kusema kuwa muungano huo hauwezi kuvunjika.

Alisema muungano unaweza kuvunjika kwa kuwa, misingi yake si madhubuti na Zanzibar haina fursa imara ya kiuchumi ndani ya muungano huo.

“Zanzibar haikuingia katika muungano ili ifadhiliwe. Inachotaka ni kuwezeshwa ili iweze kusimamia uchumi wake yenyewe,” alisema Masoud.

Katika mada yake, Shamuhuna alisema hakuna mtu wa kuhoji uhalali wa muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwa sababu umeshakubalika na wananchi.

“Muungano umeshakuwepo kwa muda wa miaka 43 na huo ni muda mrefu kuweza kuhojiwa na mtu yeyote yule kwa sababu umekuwa na kila ishara kuwa umeridhiwa na wananchi,” alisema.

Katika mada yake, Shamuhuna alitoa hoja nyingi na kunukuu baadhi ya vifungu vya katiba na kusema kwamba muungano uliopo ulipita katika taratibu zote za kisheria.

Alisema mbali na kupita katika taratibu zote za kisheria, pia muungano huo uliridhiwa na Baraza la Mapinduzi, ambacho ndicho kilikuwa chombo pekee cha kupitisha maamuzi mazito ya serikali wakati huo.

Lakini akitetea hoja yake, DPP Masoud alitoa mfano wa Uingereza na kusema muungano wake ulidumu kwa zaidi ya miaka 320 lakini uligawika baada ya misingi yake kudhoofika na hilo linaweza kutokea pia Tanzania wakati wowote.

Alisema kwamba matatizo ya muungano wa Tanzania yameshindwa kutatuliwa kwa muda mrefu sasa na kila siku kero hizo hizo zimekuwa zikijadiliwa katika vikao mbali mbali lakini bila ya kuwapo mafanikio ya kutatua.

“Nilisoma ripoti ya mkutano wa nane baina ya Waziri Mkuu mstaafu wa Tanzania, Salim Ahmed Salim na Waziri Kiongozi wa Zanzibar, Seif Shariff Hamad, lakini mpaka leo nikihudhuria vikao vya kero za muungano naona kero zile zile bado zipo pale pale,” alisema DPP.

Masoud alisema kumekuwapo na dharau kadhaa kwa upande mmoja wa muungano (Bara) juu ya masilahi ya Zanzibar hata pale ambapo makosa ya kikatiba na kisheria yameainishwa.

Alitoa mfano wa sheria ya kudhibiti fedha haramu, ambayo mwanzoni ilikubaliwa kuwa isiwe ni ya muungano lakini watendaji kwa upande wa Tanzania Bara walibadilisha wakafanya iwe ya muungano.

Masoud alisema mambo kama hayo yakiachiliwa na wahusika wasipochukuliwa hatua, ndio mwanzo wa kuharibu na kufanya kila mtu kufanya vile anavyotaka yeye na si kufuata kanuni, sheria na taratibu.

“Watu kama hawa lazima wachukuliwe hatua, la sivyo itaonekana kila mtu anaweza kufanya analolitaka kuhusu muungano,” alisema.

Shamuhuna alionyesha kushangazwa na wale wenye kuhoji muungano, kwa kusema wengi ni wale ambao hawaridhiki na hali iliyopo hivi sasa na wanafanya kila juhudi kuudhoofisha muungano.

“Waliopindua wapo na vijukuu vyao vipo, waliopinduliwa wapo na vijukuu vyao vipo na vitaendelea kufanya kila juhudi kuwarudisha madarakani… wanaohoji muungano ni wale ambao ni vijukuu vya walioondolewa madarakani,” alisema.

Akitoa mada katika semina hiyo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano), Dk. Hussein Ali Mwinyi, alisema kwamba Zanzibar imekuwa ikipata manufaa ya muungano na katika kipindi cha utawala wa Awamu ya Nne, tayari baadhi ya kero tano za muungano zimeshapatiwa ufumbuzi wa kudumu.

Alisema katika mwaka wa fedha unaomalizika, Zanzibar imepata zaidi ya sh bilioni 22 zinazotokana na fedha za msamaha wa madeni zinazotokana na wafadhili na fedha za mgawo wa faida unaotokana na Benki Kuu ya Tanzania (BoT), na kwamba mwaka ujao wa fedha Zanzibar imetengewa zaidi ya sh bilioni 27.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.