WATUMIAJI wa nishati ya umeme huenda wakalazimika kulipa zaidi kuanzia mwaka ujao wa fedha iwapo serikali itatekeleza azima yake ya kutolipatia Shirika la Umeme nchini (Tanesco) ruzuku.
Badala yake, serikali inalitaka shirika hilo, kupata fedha za kuendesha shughuli zake kupitia mikopo kutoka katika taasisi za kifedha, jambo ambalo linaweza kusababisha shirika lijibane kuwakamua wateja wake ili kuweza kumudu kurejesha mikopo hiyo.
Azima ya serikali kutoipatia Tanesco ruzuku ilibainishwa jana na Waziri wa Fedha, Zakia Meghji, wakati alipokuwa akitoa maelezo kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya serikali kwa mwaka wa fedha 2007/08 mbele ya Kamati ya Bunge ya Fedha na Uchumi.
Meghji, alisema ifikapo mwishoni mwa Juni mwaka huu, serikali inategemea kutumia jumla ya sh bilioni 204.5 kwa ajili ya kulipia mitambo ya kununua na kukodi ya kuzalisha umeme.
Alisema, mitambo hiyo iliingizwa nchini wakati wa tatizo kubwa la umeme lililoikumba nchi mwaka jana, hali iliyosababisha serikali kuidhamini Tanesco ili ipatiwe mkopo kutoka benki.
Katika kipindi hicho, serikali ilitoa ruzuku ya sh bilioni 20 kwa Tanesco pamoja na kuidhamini kukopa kiasi cha sh bilioni 126.5 kutoka benki ili kuepusha madhara makubwa katika uchumi wa taifa.
“Desemba mwaka jana, serikali ilitoa ruzuku ya sh bilioni 20 kwa mwaka uliopita wa fedha na iliidhamini Tanesco kukopa kutoka benki kiasi cha sh bilioni 126.5, hatua hizo kwa pamoja zililenga kuepusha madhara makubwa ambayo yangetokea katika uchumi wa taifa.
“Katika bajeti hii ya fedha…serikali imeamua kusitisha utoaji wa ruzuku kwa shirika la umeme ila tunawataka kwenda kukopa benki na sisi tutawadhamini kwa hilo, lakini si kuwapa ruzuku tena,” alisisitiza Meghji alipotakiwa na waandishi wa habari kufafanua mipango ya serikali kuhusu Tanesco katika bajeti ijayo ya fedha.
Aidha, Waziri wa Fedha, alisema tatizo la umeme lililoikumba nchi hadi mwishoni mwa mwaka jana, halikuathiri ukusanyaji wa mapato ya ndani kwa kuwa serikali iliiagiza Tanesco kutokukata umeme wa viwandani ili kulinda mapato yake.
“Ukweli ni kwamba wote ni mashahidi mwaka jana Serikali ya Awamu ya Nne ilianza na matatizo ya ukame uliosababisha njaa, umeme uliotishia giza kwa nchi yetu lakini tulifanya vizuri.
“Kati ya Julai mwaka jana na Machi mwaka huu, mapato ya ndani yalifikia kiasi cha sh trilioni mbili, sawa na asilimia 81.4 ya bajeti ya mwaka na asilimia 109.7 ya matarajio kwa kipindi hicho,” alisema.
Kumalizika kwa mgawo wa umeme, uwepo wa maji ya kutosha kwa ajili ya uzalishaji wa nishati hiyo muhimu kumeifanya serikali iamini kwamba bajeti iliyopita imetekelezwa kama ilivyopangwa.
Pamoja na hayo, Meghji alisema vianzio vya mapato ya ndani vilifanya vyema isipokuwa ushuru wa bidhaa kwa mafuta ya petroli na VAT kwa bidhaa kutoka nje.
Kuhusu ushuru kwa bidhaa za mafuta, alieleza kuwa baadhi ya bandari hapa nchini hazina mashine za kisasa za kutambua kiasi cha mafuta yanayoingia, hali inayosababisha kuwepo na udanganyifu kwa watumishi wa bandari hizo.
Alisema, tayari serikali ipo kwenye mipango ya kudhibiti hali hiyo kwa bandari zote nchini ili kuongeza mapato.