Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  JK atende anayosema
JK atende anayosema
By Habari Tanzania | Published  06/5/2007 | Habari za Kitaifa | Unrated
TUMELAZIMIKA kuandika maoni haya kutokana na habari kubwa ya leo ambayo inatokana na mahojiano kati ya Rais Jakaya Kikwete na jarida maarufu la Kiafrika la NewAfrican.

Kikubwa kilichogusa fikra na hisia zetu ni maneno mazito aliyoyatoa kiongozi wetu mkuu, hususan katika eneo la uhusiano kati ya serikali yake na vyama vya upinzani na dhamira ya chama tawala, Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika kupigania na kuendeleza mfumo wa vyama vingi.

Kwa maelezo yoyote yale, kauli alizozitoa Rais Jakaya Kikwete wakati wa mahojiano hayo kwamba serikali na CCM havina sababu ya kuua upinzani, haiwezi ikapita pasipo kutolewa maoni.

Lakini kama hiyo haitoshi, kauli nyingine kwamba, malalamiko ya wapinzani kuibiwa kura yamekuwa yakitolewa na wapinzani kwa sababu tu ya kuogopa kupoteza wanachama, haiwezi ikapita pasipo kutolewa maoni.

Kauli hizo mbili, na pengine ya tatu ya kuahidi kuwa mazungumzo ya sasa kati ya CCM na CUF yatamalizika huku pande zote mbili zikiwa zimeridhika, ni nzito na ambayo kimsingi inapaswa kuungwa mkono na kila anayeitakia mema nchi yetu.

Kikubwa katika kauli zote hizo tatu za rais ni ukweli kwamba, ni jambo gumu kwa mtu mfuatiliaji wa mambo kuamini kuwa alizitoa kwa nia njema, ya wazi na iliyo ya kweli.

Tunasema hivyo, nyuma yetu historia ikionyesha bayana kwamba, CCM na serikali yake vimekuwa vikichukua hatua mbalimbali ambazo kimsingi zinaonyesha namna inavyojipanga kuua upinzani huku ikijua kuwa hatua hiyo ni ya hatari.

Mkakati kabambe unaochanganya nguvu kubwa za dola za kuwavuta wapinzani kujiunga na CCM huku sheria na taratibu lukuki za mambo zikivibana vyama hivyo vya upinzani, ni ushahidi tosha kwamba, serikali yetu ina makusudio mabaya dhidi ya upinzani, japo imekuwa ikitoa maneno ambayo hayafanani na matendo yake.

Tunaandika hilo leo wakati ikiwa ni karibu miezi minne sasa tangu viongozi wa vyama vya kidemokrasia barani Afrika (DUA), wakutane nchini na kuzilalamikia serikali zilizoko madarakani katika bara hili, ikiwamo CCM.

Wakati huo sisi wa Tanzania Daima tulieleza dhahiri kuguswa na kilio cha viongozi wa DUA kilichotolewa katika tamko lao la pamoja, lililobeba kilio dhidi ya viongozi wa vyama vinavyotawala katika nchi nyingi Afrika, pamoja na Waafrika wenyewe, ambao wanatawaliwa na vyama hivyo.

Viongozi hao kwa kauli moja walisema matatizo kama umaskini, ujinga na maradhi, yanayowasumbua wananchi wengi wa Bara la Afrika ni matokeo ya uduni wa demokrasia na sera zinazotekelezwa sasa na watawala wa nchi za Kiafrika, ambao mfumo wao wa utawala bado ni wa zama za kale, wa serikali kuu kuhodhi madaraka yote.

Hakuna anayeweza kubisha kwa dhati kwamba katika dunia ya sasa, mifumo ya namna hii ya kiutawala ni kinyume cha matakwa ya sasa ya demokrasia na maendeleo, na ili kuondokana nao, kamwe umuhimu wa kuwapo kwa vyama vingi katika nchi za Kiafrika, tena vyenye nguvu hauwezi kupuuzwa.

Kauli hiyo ya DUA kuwa mfumo wa utawala unaotumiwa na viongozi wengi wa vyama vya siasa walioko madarakani ni wa kuvidhoofisha au kuviua kabisa vyama vya upinzani, inatofautiana kabisa na maneno matamu aliyotoa Rais Kikwete, ambayo watu wenye akili hawawezi kuyaamini.

Kwa sababu hiyo basi, tunapenda kumuasa Rais Kikwete kuyaweka katika matendo, maneno matano aliyomweleza mhariri wa NewAfrican ili malengo yake aliyoyafinyanga ndani ya kaulimbiu ya Ari Mpya, Nguvu Mpya na Kasi Mpya, yaweze kufikiwa na hatimaye kuiondoa nchi hii katika mzigo wa matatizo ya kisiasa, kiuchumi na kijamii ambayo sasa yamegeuka hadithi ya kufikirika isiyokwisha.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.